Sf 2,3;3,12-13; 1Cor 1, 26-31; Mt 5, 1-12
Maisha kamili yanaitegemea furaha ya
kweli ambayo Yesu pekee yake anaweza kutuletea. Yeye alifanya hivyo kupitia
kuhudhuria hali yetu ya kibinadamu akianzisha njia kamili ya kuishi. Njia hii
inamhusu Mungu nayo inapitia unyenyekevu na haki. Mungu mwenyewe hana macho
kwa waliotenda udhalimu wala kwa wanafiki bali kwa wanyenyekevu. Yeye yu makini
sana kwa kilio chao naye yuko tayari kuwatendea mema kwa maana maisha yao yanathamini
sana kwake. Kupitia Yesu anaonyesha upendo maalum kwao ambao wanamtumainia yeye
peke yake.
Katika andiko la Kwanza, nabii Sefania
anatambua ndani ya maskini na wanyenyekevu uwezo mkubwa wa kumtafuta Mungu na
kumtegemea yeye katika mambo yote. Mungu anaijua hali ya maskini na ya wanyenyekevu
naye anaguswa na mahitaji yao. Maisha ya maskini na ya wanyenyekevu yanashuhudia
kwamba kimbilio ambalo linatuhakikishia usalama sio pesa wala ulaji, bali ni
Mungu peke yake. Kweli Mungu anapatikana kwa wanaotaka kukutana naye, lakini ni
wanyenyekevu wa moyo tu wanaoweza kuuona uso wake, yaani kufanya uzoefu wa
uwepo wake.
Mtakatifu Paulo anasisitiza kuhusu
tofauti kati ya mawazo ya Mungu na ya mawazo ya kidunia. Kulingana na mawazo ya
kidunia ndio wenye umaarufu, wenye nguvu na matajiri waliotambuliwa kama watu
wenye thamani. Badala yake, Mungu anawathamini na kuwasaidia waliodharauliwa na
dunia hii yetu, yaani maskini na wanyenekevu. Kama wafuasi wa Kikristo,
hatujaitwa kuifuata hekima ya kibinadamu wala kuutafuta umaarufu wa kidunia. Wito
wetu unatoka kwa Mungu na kupaswa kuyafuata mawazo yake na njia zake kama
Kristo alivyo.
Andiko la injili ni mwanzo wa ile
iliyojulikana kama “Hotuba ya mlimani” iliyotangazwa na Yesu. Hotuba hii kabisa
inajumuisha sura tatu, yaani kutoka 5 mpaka 7. Kwanza kabisa ni muhimu sana
kuifahamu nia ya Mathayo alipoandika toleo lake. Yeye aliandika kwa Wayahudi na
kwa hivyo, alimjulisha Yesu kama “Musa Mpya” na aliye utimilifu.
Mambo yote ambayo yanamhusu Kristo yanaileta hali mpya. Hivyo, Mlima wa “heri
nane” unatukumbusha hali ya Mlima wa Sinai; ujumbe huu wa “Heri nane” ni
mafundisho mapya kuhusu Amri za zamani; upendo wa kindugu ni haki mpya ambayo inashinda
haki ya walimu wa Sheria na Mafarisayo, n.k.
Katika biblia, mlima ni mahali
muhimu sana. Huko Mungu anajifunua mwenyewe na kufanya agano na Israeli. Tena
huko baadhi ya viongozi waliweza kukutana na Mungu na kupokea kutoka kwake miongozo
kwa maisha yao na ya watu waliokabidhiwa kwao. Yesu alichagua mahali huko kwa
hotuba yake ya kuuanzisha ufalme wa mbinguni, yaani mapendekezo ya kupata
furaha ya kweli kulingana na matarajio ya Mungu. Huu ni mpango wa maisha ambao
Yesu aliishi kwanza kabla ya kupendekeza kwa wote. Kwa kifupi, ndani ya Heri nane
tunaweza kukuta nafsi ya Yesu mwenyewe katika uhusiano wake na Mungu. Katika
yeye na kwa sababu yake sisi tu wenye heri.
Wakati Yesu alipotangaza Ufalme
wa Mungu kwa mara ya kwanza, aliamua kuhubiri maneno ya faraja kwa wale waliokuwa
na mahitaji na mateso mengi na kumtumainia Mungu, yaani walio kipaumbele katika
Ufalme. Kweli, huko hawakwako wenye nguvu ama matajiri, bali maskini kwa aina
mbalimbali. Tunahitaji kuchukua andiko hili la Mathayo pamoja na lile la Luka
(6, 20-26) linalofanana zaidi na yale aliyofundisha Yesu. Hali ya maskini
inagusa sana moyo wa Yesu naye alifanyika mwili akikubali hali hii ili kuonyesha
ukaribu wa ufalme wa Mungu hasa kwa ajili ya wanaofunguliwa kwa mpango wa Mungu
kuyahusu maisha yao. Ufalme wa Mungu ni wao.
Watu Hawa walionyeshwa na nyuso nyingi,
yaani, “walio maskini wa roho ndio wasio na tamaa ya makuu bali wanaweza
kuyasalimisha maisha yao mikononi mwa Mungu; wenye huzuni ndio wanaoguswa na uchungu
wa wenzao; wenye upole ndio wanaoishi kwa ushirika na moyo wa Mungu; wenye njaa
na kiu ya haki ndio wanaojitolea kwa kujenga jamii nzuri; wenye rehema ndio wanaoguswa
na huruma ya Mungu ili wawe chombo cha huruma hii; wenye moyo safi ndio wanaoweza
kumjua Mungu; wapatanishi ndio wanaosaidia uzoefu wa kindugu katika jumuiya
zetu; wanaoteswa kwa ajili ya haki na kwa jina la Yesu ndio walio mashahidi wa
wema wa Mungu kati yetu. Ufalme wa mbinguni ni tuzo yao.
Sisi, tulio wafuasi wa Yesu,
tunaalikwa kuchukua ujumbe wa “Heri nane” kama mpango wa maisha. Hatuhitaji
njia nyingine ya kuishi kwa ajili ya kupata furaha ya kweli. Mambo yote Yesu
aliyotaka kusema kwa wanaotaka kumfuata yapo hapa. Mungu anataka tuwe wenye
furaha, lakini njia zake zina masharti yaliyo Heri nane yanayotualika tuweze
kubadilisha njia ya kuona na ya kuishi. Hii ni njia ngumu, lakini hatuko pekee
yetu. Mungu yu pamoja nasi kwa sababu hawaachi wale wanaomtumainia yeye. Maisha
yetu yana thamani kubwa kwake. Jibu linalompendeza ni tuweze kuishi kwa uaminifu
yale aliyoishi na kuyafundisha Yesu. Huu ni utabiri wa wakati mpya. Ingawa
ufalme upo katika Yesu, yeye mwenyewe anatambua thamani za ufalme huu duniani
na katika hali ya jumuiya zetu. Neema yake ituimarishe tuwe vyombo vya thamani
za ufalme huu.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário