sábado, 18 de fevereiro de 2023

UPENDO BILA MIPAKA

 

Kutafakari kuhusu Law 19,1-2.17-18; 1Kor 3,16-23; Mt 5,38-48




 

    Uumbaji wa mwanadamu ulikuwa ni tendo la upendo. Wakati Mungu alimwumba alisema: “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu.” Kwa hiyo, tangu asili binadamu ameitwa kutenda kama Mungu alivyo. Kutenda kama Mungu ni kupenda. Ahadi yote ambayo mtu anachukua katika safari yake duniani inapaswa kumwongoza kwenye mwelekeo huo.

    Hivyo, tunaweza kuelewa sababu ya agizo la sheria katika Agano la Kale linalosema, “Muwe watakatifu kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.” Sheria hii ni njia ya utakatifu kwa Wayahudi. Kwa sababu ya utakatifu wa Mungu, watu ambao wamechaguliwa naye wameitwa kuwa watakatifu, na njia ya kufikia lengo hili ni “kumpenda jirani yao kama nafsi yao wenyewe.” Matarajio ya Mungu ni kwamba waweze kutenda kama yeye alivyo.

    Andiko la pili linatuambia kwamba Yesu ametupa Roho wake naye huyo Roho anaishi ndani yetu. Hivyo maisha yetu yamekuwa hekalu la Mungu. Hii inathibitisha wito wetu wa kuwa watakatifu, kulingana na mpango wa Mungu tangu mwanzo. Uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu ni msaada ili matendo yetu yawe matakatifu.

    Mafundisho ya Yesu yanalenga kuzaa uhusiano mpya kati ya watu na Mungu na kati ya watu wenyewe. Yeye anaonyesha kuwa ukamilifu wa Baba ni msukumo wa ukamilifu wa wana wake. Hili si jambo lisilowezekana, bali Yesu mwenyewe anajulisha, hatua kwa hatua, jinsi ya kumkaribia Mungu hata jinsi ya kuishi kama yeye aliyejaa upendo na ukarimu.

    Maneno haya “jicho kwa jicho na jino kwa jino” ambayo Yesu aliyataja, inaitwa “Sheria ya Talioni”. Sheria hii haikulenga kuwa msukumo kwa ajili ya ukatili ama wa kisasi, bali “ilikusudiwa kuzuia kulipiza kisasi, na hivyo kumlinda mtu aliyefanya kosa asipewe adhabu kubwa kuliko uzito wa kosa lenyewe.” Kweli sheria hii ilizaliwa kwa sababu “mara nyingi adhabu ilikuwa kubwa kuliko kosa.” Hata hivyo, njia hii iliyofundisha na Sheria hii haikuonyesha mapenzi ya Mungu, ambaye aliagiza “wampende jirani kama nafsi yao.”

    Kama nia ya Yesu ni kugundua tena mpango wa Mungu wa kiasili, anataka kuwafundisha watu kwa njia tofauti. Yeye hawalazimishi wasikilizaji wake kuchukua ahadi hii, bali ili waweze kumfuata kwa kweli kuna masharti. Wakati watu wengine wanapenda tu wale wanaowapenda wao, kwa upande wa wanafunzi wa Yesu ni masharti kuwapenda hata maadui zao na kuwatendea mema wale wanaowachukia. Huu ni upendo bila mipaka ulio tabia ya upendo wa Kikristo. Lengo la jambo hili ni tuwe watoto wa Mungu ambaye anazitoa zawadi zake kwa wale walio wema na kwa wabaya. Anafanya hivyo kwa sababu ni tabia yake na kwa sababu anataka tujifunze kutoka kwake. Ingawa hatustahili zawadi zake, hatuwezi kuweka mipaka katika ukarimu wake.

    Mwanafunzi wa kweli wa Yesu “hashindani na mtu mwovu”, bali anatoa “shavu tofauti la maisha” na njia tofauti ya kutenda. Hii inamaanisha kumpa mwingine nafasi ya kufikiri vizuri na kubadilisha matendo yake. Mafundisho ya Yesu yanatuimarisha kutumia wema wa moyo na matendo mema kwa kumwombea mtu mwovu. Kwa msaada wa Mungu tunaweza kuibadilisha hali ya uovu kwa sababu yeye mwenyewe ana mazoea ya kubadilisha hali mbaya kuwa hali nzuri na hali ya mauti kuwa hali ya uzima. Kifo cha Mwanae kilikuwa tendo baya la wanadamu, lakini yeye alibadilisha hali hii mbaya kuwa ni manufaa ya wokovu wetu. ushuhuda wazi sana ya hili ni wakati Yesu alipokuwa msalabani akiteswa na maadui wake, akawaombea msamaha kwa Mungu Baba. Pia aliwatetea kuwa hawakujua walilolifanya.

    Kutokana na mfano wa Kristo, anayeitwa pia “nabii asiye na ukatili”, njia ya kipekee ya kuushinda ukatili ni kujibu kwa ishara za amani. Yesu anataka kwamba tabia zetu zishinde mwelekeo wa kijamii kwenye kisasi, ukatili na ukabila. Ukabila unauharibu undugu na kuukanusha utambulisho wetu wa Kikristo. Kulingana na Baba Mtakatifu Francisco, “kipimo cha utambulisho wetu kama watoto wa Mungu ni tabia ya huruma.” Kama wafuasi wa Yesu sisi sio bora kuliko wengine, lakini tunapaswa kutenda tofauti, yaani kulionyesha “shavu lingine.” “tunapowachukia maadui wetu tunawapa uwezo juu yetu: uwezo juu ya usingizi wetu, hamu yetu ya chakula, shinikizo letu la damu, afya yetu na furaha yetu” (Dale Carnegie). Kwa kifupi, Hatuwezi kuruhusu kuwa waovu waamue jinsi tunavyopaswa kutenda.

    Kuna hadithi fulani inayoongea zaidi kuhusu hayo. “Mwandishi fulani anayeitwa Sydney Harris, anatuambia hadithi ambayo ilitokea alipoandamana na rafiki yake kwa duka la magazeti. Rafiki yake alimsalimia mwanagazeti kwa heshima sana, lakini kama jibu, mtu huyo alimtendea vibaya. Rafiki wa Harris akikubali gazeti lililotupwa kwa njia mbaya kwenye mwelekeo wake, alitabasamu kwa heshima na kutakia wikiendi njema kwa mwanagazeti. Baadaye,  walipotembea njiani, mwandishi alimwuliza rafiki yake, akisema, “Mtu huyo ana tabia mbaya kwako daima?” “Ndiyo, kwa bahati mbaya, yeye alivyo.” Na wewe una tabia ya heshima na ya kirafiki kwake daima?” “Ndiyo, mimi ndivyo.” “Kwa nini wewe ni mtu mwema mno kwake ikiwa yeye ana tabia mbaya kwako?” “Kwa sababu sitaki kwamba aamue jinsi ninavyopaswa kutenda.”

    Ndiye Yesu mwenyewe ambaye anatualika kutenda vivyo hivyo. Kulingana naye, uovu hauwezi kuondoa uovu, bali ni wema tu unaoweza kufanya hivyo. Tupendane kama Yesu alivyo na, kwa njia ya upendo huu, tuweze kuijenga jamii inayotarajiwa na Mungu kwa watoto wake.

 

 Fr Ndega

Nenhum comentário: