Matendo 2, 14a.36-41;
1Pt 2,20b-25; Yoh 10,1-10
Tunaadhimisha Jumapili ya Mchungaji
mwema na Jumapili ya miito. Jumapili hii ni mwaliko kumshukuru Mungu kwa zawadi
kuu ya wito na kumwomba ili aendelee kulibariki Kanisa lake kwa miito mingi.
Pendekezo la Jumapili hili linatoka kwa baba mtakatifu Paulo wa VI. Yeye
alilialika Kanisa zima kuchukua ahadi kwa ajili ya wito. Maombi kwa ajili ya miito
ni pia utiifu kwa mwaliko wa Yesu ili tuombe kwa mwenye mavuno ili atume
wafanyakazi kwa mavuno yake kwa sababu mavuno ni makubwa, lakini wafanyakazi ni
wachache (cf. Mt 10, 37-38). Wito ni zawadi ya Mungu. Tena ahadi ya kuiombea miito
ni zawadi yake. Huu ndio utekelezaji wa ubatizo wetu. Kilimo cha wito huanza
katika familia na yule anayealika hutarajia jibu kwa ukarimu kutoka kwa wanaoalikwa.
Katika somo la kwanza mitume wanatangaza
kwa shauku fumbo la pasaka ya Kristo kwa nguvu wa Mungu, kama mwaliko wa
mabadiliko ya maisha. Nguvu ya maneno yao yalitoka kwa Roho Mtakatifu akitenda
maishani mwao na kusababisha kutubu. Kwao kila kipindi kilikuwa nafasi mpya ya
kushuhudia maisha mapya aliyotoa Yesu kwa wote hata “kwa ajili ya wanaokaa
mbali na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake”. Ndiye
Kristo ukamilifu wa ahadi za Mungu na kupitia yeye watu wana uhakika wa kupata
wokovu. Yeye ametufanya kuwa watoto wa Mungu na kutualika kuwa na uhusiano mwema
na Mungu kama wana kondoo na mchungaji wao. Tukiufuata mfano wake tunaweza kuwatenda
wengine mema na kuishi kama wamoja.
Yesu ndiye Mchungaji Mwema kwa sababu
anawapenda wana kondoo wake naye yuko tayari kufa kwa ajili yao. Anawajua wana
kondoo wake na kuwaalika kuisikiliza sauti yake ambayo yanawaongoza kupata
ukamilifu wa maisha yao. Uhusiano wa upendo kati ya Mwana na Baba ndio rejeo la
uhusiano kati ya Yesu na kundi lake. Uhuru wa Yesu wa kutoa uhai wake kwa ajili
ya kundi lake ni maonyesho ya upendo wake. Akitumia mfano huu Yesu anataka
kuongelea uhusiano kati yake na wanafunzi wake. Msingi wa uhusiano huu ni
imani, upendo, upole nao unasababisha maisha kamili kwa wafuasi wake. Kama yeye
anawajua wana kondoo wake, anatarajia kwamba wako tayari kumjua na kuyafuata
mafundisho yake. Kosa la kujua njia na sauti ya mchungaji ni hatari kwa sababu
linaweza kusababisha mgawanyiko wa kundi na hasara ya utambulisho wa mfuasi.
Njia ya Yesu ya kuongoza na kutunza ni kipimo cha walio na jukumu la kuwaongoza
watu.
Yesu ni mlango wa uhusiano mwema kati
ya watu na Mungu. Mlango huu unamaanisha vipengele vitatu. Cha kwanza, Yesu
ndiye njia inayotuongoza kwa Baba;
uwepo wake unatuhakikishia mkutano na Mungu. Cha pili, Yesu ndiye ukweli wa Mungu kwa binadamu na ukweli
wote wa binadamu kwa Mungu; “kila mtu wa ukweli humsikiliza” (Yoh 18,37) na
kuruhusu kuongozwa naye kwa ajili ya kupata ukweli kamili. Yesu ndiye uhai unaotolewa kwa hiari ili kundi lake
lipate maisha mengi. Katika Yesu aliye Mchungaji Mwema, Mungu anaonyesha ulinzi
na utunzaji wake kwa ajili ya watu wake. Upinzani dhidi ya sauti ya Yesu ni
upinzani wa kuifanya mapenzi ya Mungu na kuishi uhusiano wa upendo naye. Jibu
yeye analotarajia kwa mwaliko wake siku hizi ndio uangalifu kwa msukumo wake
ili tuweze kutenda kwa hekima katika mazingira yote.
Yesu ni mchungaji mwema kwa sababu anayajua
mahitaji ya wana kondoo wake na jinsi ya kuwatunza. Hakuna jambo lingine ambalo
anatarajia kwa kundi lake isipokuwa maisha mengi na kamili. Wito wetu unapata
mafanikio yake wakati tunaweza kutambua sauti ya Bwana kati ya sauti nyingi
zinazojaribu kutuongoza. Kupitia neno lake, sakramenti na mafundisho ya
wachungaji wetu Mchungaji Mwema Yesu anaendelea kuwaongoza na kuimarisha kundi
lake. Tunaalikwa kuruhusu kuongozwa katika roho ya upole na ushirika. Hata sisi
pia kupitia ubatizo tuko na jukumu la kuwaongoza wengine kwa kuwasaidia
wachungaji wetu wafanye kazi yao vizuri. Tunaalikwa kutenda kama wanafunzi wa
kwanza, ambao waliuchukua wito kwa furaha na kwa hamu kwa manufaa ya Watu wa
Mungu ndilo kundi la Yesu.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário