domingo, 21 de maio de 2017

UPENDO WA KWELI UNAONYESHWA KWA ISHARA HALISI


Kutafakari kutoka Mdo 8,5-8.14--17; 1Pt 3,15-18; Yoh 14, 15-21


        Maandiko haya yanaanza kuongea kuhusu kazi ya Roho Mtakatifu aliye upendo wa Baba na Mwana naye anatolewa ili aandamane na kazi ya jumuiya ya wanafunzi wa Yesu ili wapate kujua kamili kuhusu ufunuo wake. 
         
        Kulingana na somo la kwanza baada ya mateso dhidi ya Kanisa katika Yerusalemu, watumishi wengi walikimbilia maeneo mengine ili kuinjilisha. Shemasi Filipi alifanya kazi katika Samaria na kupata mafanikio, yaani Wasamaria walikaribisha neno la Mungu kwa furaha kubwa. Ishara za ajabu alizotenda Filipi zilithibitisha ukweli wa maneno yake. Pedro na Yohana walifunga safari kutoka Yerusalemu kwenye Samaria ili kukutana na Filipi kama ishara ya ushirika wa Kanisa zima, linaloongozwa na Roho Mtakatifu, limejaa matunda mengi kwa wokovu wa watu.

         Uinjilisti hauna mipaka na kulenga kuondoa ukuta wa utengo ambao hugawanya watu. Kazi hii inaimarishwa na Roho Mtakatifu aliyetolewa sio kwa uzoefu umefungwa wa kikundi kimoja tu bali ni zawadi kwa wote. Kupitia yeye waliomfuata Yesu wako tayari daima “kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yao”. Lakini hii ndiyo kazi ya kufanywa kwa upole na heshima ili mapenzi ya Mungu yakafanyike. Wamisionari ni vyombo tu. Kweli ndiye Mungu mwenyewe anayefanya kazi kwa Roho wake akisababisha mabadiliko na furaha kubwa maishani mwa watu.  

       Katika injili tunaendelea na hotuba ya mwisho ya Yesu. Yeye aliongea na wanafunzi wake moyo kwa moyo, akionyesha hisia zake za ndani kwa ajili yao. Hotuba hii inadhihirisha uhusiano wa ndani kati ya Yesu na Baba na pendekezo la Yesu kwa wanafunzi wake ili waweze kuwa ufanisi katika utume wao.  

         Aliposema, “mkinipenda, mtazishika amri zangu,” aliwaomba ahadi kwa ajili yake kwa njia halisi kwa sababu upendo ni halisi, yaani wakati mtu anaposema kwamba anapenda mwingine anapaswa kuonyesha ishara halisi ambazo zinathibitisha upendo huu. Ishara halisi Yesu anazotarajia kutoka kwa wanafunzi wake ni kupendana na kutumikiana kama Yesu alivyofanya. “Huu ni upendo ambao unamfanya mtu kuyatoa maisha yake kwa ajili ya wengine.”

         Yesu hatawaacha wanafunzi wake kama walio yatima bali ataendelea miongoni mwao kwa njia tofauti. “Hatakuwa nao kimwili, lakini wataweza kuuhisi uwepo wake kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ataendeleza yale yote aliyowafundisha na kuwaongoza hadi kuelewa kikamilifu maana ya mafundisho ya Yesu katika wakati zao wenyewe. Sio watu wote walio tayari kupokea zawadi hii, bali ni wale mitume ambao waliandaliwa kuipokea katika maisha yao kwa njia ya Yesu. Mwombezi huyo ni “Roho wa Kweli” atakayetoa ushuhuda kwa Yesu na kuwaongoza mitume wake katika kweli yote.” Yeye ni pia Roho wa Umoja atakayehakikisha umoja wao hasa wakati wa mateso. Msemo fulani wa Kiafrika unasema: “umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu”.


        Ahadi ya Yesu ya kurudi kwa ajili yao inamaanisha kuendelea kuwepo, lakini kwa njia ya ndani, yaani kupitia upendo. Ndio upendo kati ya Yesu na wanafunzi wake ambao utawafanya watu wasadiki. Ndio kwa upendo ambao Mungu anatupa kwa Roho wake kwamba tunaweza kuendeleza kazi ya Yesu. Tunaishi katika ulimwengu ambao upendo umepoteza maana yake ya kiasili, yaani mtu anasema, ninapenda ikiwa naweza kuchukua nafasi juu ya mwingine” ama “napenda mpaka wakati fulani” ama “nawapenda baadhi ya watu tu, lakini sipendi wengine”. 

      Yesu anatuzungumzia sisi kuhusu upendo tofauti; ndio upendo wa kweli. Ukweli wa upendo huu unaonyeswa na uwezo wa kujitolea na kutumikia bila kufanya ubaguzi wa watu. Mtu anayependa kweli anataka tu manufaa ya mtu anayempenda. Ndio kwa upendo huu ambao Yesu anatualika siku ya leo. Huu sio upendo ambao unaniongoza kufanya lile ambalo linanipendeza tu bali unaniwezesha mimi kujisalimisha kwa ajili ya wengine. Ndio upendo ambao unatufanya kuacha ubinafsi wetu na kuenda kukutana na wengine katika mahitaji yao. Huu ni upendo ambao unafanya kazi yetu iwe ufanisi daima naye Roho Mtakatifu tu anayeweza kuuimarisha upendo huu mioyoni mwetu. Kwa hivyo, uje Roho Mtakatifu!   

Fr Ndega

Nenhum comentário: