Kutafakari
kuhusu Eclo 15,15-20; 1Cor 2,1-10; Mt 5,17-37
Mungu anayaongoza
mambo yote duniani kulingana na mpango wake wa hekima na wema. Hakuna lolote
ambalo linakosa mtazamo wake wa upendo. Yeye anauheshimu uhuru wa wanadamu naye
anapopendekeza kwao njia ya kupata uzima, anatarajia waweze kuchagua vizuri na
kuishi milele. Kulingana na Paulo, hekima ambayo ilikuwepo na Mungu tangu
milele imo ndani yetu na kutuongoza katika maamuzi yetu. Fumbo hili Mungu
aliwaandalia wanaompenda na kutufunulia kwa Roho Mtakatifu. Kutambua hili ni
sharti ili tuweze kufanya tofauti katika hali zetu.
Injili ya Mathayo
inamjulisha Yesu kama “Musa mpya” na mafundisho yake ni mapya kabisa. Hatuwezi
kusema kwamba kuna kupasuka kati ya mafundisho yake na yale ya
mababu wa zamani, bali mwendelezo. Lakini, ingawa hayo ni mwendelezo, ndiye
Yesu anayetafsiri kwa njia kamili mambo yote yaliyosemwa. Kwa hivyo, aliwaalika
wasikilizaji wake wamsikilize akisema, “Lakini mimi nawaambieni...”
Alisema hayo kwa sababu alikabiliana na ugumu wa mioyo ya baadhi ya watu. Hata
hivyo, aliyaheshimu maandiko ya Agano la Kale na tena
aliwashauri watu wayaheshimu maandiko hayo. Basi Agano la Kale linaendelea kuwa
muhimu kwa Wakristo, kwa hivyo Yesu alisema kwamba Yeye hakuja kutangua Torati
au Manabii. Kweli yeye amekuja kukamilisha ahadi zilizotolewa kwa njia ya
maandiko haya. Yeye yu uthibitisho mkuu wa uaminifu wa Mungu kwa ahadi zake.
Yeye “alitaka
kurekebisha mambo makubwa zaidi,” akigundua tena mpango wa
Mungu wa kiasili. Mpango huu ni ufunuo wa upendo wake ambao hawezi kuutegemea
mtazamo wa kipungufu wa binadamu. Yesu anasisitiza kwamba haki ya
wanafunzi wake inapaswa kuishinda ile ya Mafarisayo na Waandishi wa sheria.
Katika Mathayo, haki inamaanisha mapenzi ya Mungu na wenye haki ni wale
wanaofanya mapenzi yake. Mapenzi haya ni kwamba watu waweze kuishi ukarimu bila
kipimo, wakifanya zaidi kuliko kuitii sheria, yaani, uhusiano wa heshima na
upatanisho. Kidogokidogo wanafunzi wa Yesu walikuwa wakitambua kwamba matarajio
ya Yesu yalikuwa kuanzisha uhusiano mpya kati ya watu na Mungu na tena miongoni
mwa watu. Yeye anataka “watu wawe na utii unaotoka moyoni, na siyo utii wa
unafiki kwa sheria tu za nje tu.”
“Yesu anataka sheria zetu ziendane na matendo yetu. Utii wa sheria tu,
pasipo matendo ya kweli, hauwezi kutusaidia lolote katika maisha yetu. Ni
mioyoni mwetu, na kwa upendo kama wa Yesu, ndipo tutaweza kutimiza amri za
Mungu kwa maneno na matendo”. Hivyo, ni Injili ya Yesu inayopaswa
kuwa sheria katika uhusiano wetu wa kibinadamu. Ikiwa tunataka kuwa na
uhusiano mwema na Mungu hatuwezi kuwapuuza wengine ama kuwa na
uhusiano mbaya nao. Kulingana na mtazamo mpya wa Yesu, njia ya mtu ya kuishi inaweza kusababisha
mauti ya mwingine bila haja ya kutumia bunduki. Kuwa na hasira na mtu na kuionja
hisia hii kwa muda mrefu ni kumwua mtu huyo moyoni mwako. Kwa Yesu hayo ni
mauaji ya kweli. Kutoheshimu ni mwanzo wa mauaji hayo.
Tunaalikwa
kuwa macho kwa sababu kila wazo, neno na tendo ambalo halilengi kutimiza
mapenzi ya Mungu kama alivyofikiri Yesu linampa yule Mwovu nafasi na kuharibu
maisha yetu ya kifamilia na kijumuiya. Uhuru wetu unatuongoza kuyatumia maneno
kama chombo cha kujenga undugu, mfano maneno ya upendo, ya faraja, ya tumaini,
n.k.; au tena kama chombo cha kuharibu, mfano maneno ya dharau na ya uvumi. Uvumi
kuhusu mtu fulani huondoa heshima yake. Kuna hadithi moja inayoyahusu mawazo ya
Yesu na kutusaidia kushinda hali mbaya ya uvumi. “Siku moja mtu mmoja
alimwendea Socrates mwanafalsafa wa Kigiriki na kumwambia, “sikiliza umbea juu
ya rafiki yako.” Socrates alisema, “Ngoja, ujumbe unaotaka kunipa je
umeupitisha kwenye vipimo vitatu?” Vipimo vitatu ni vipi?” Socrates alijibu,
“Je unayotaka kuniambia ni ukweli?” Mtu huyo alijibu, “kusema kweli nimesikia
toka kwa mtu mwingine.” “Je unayotaka kuniambia ni jambo la upendo?” Mtu huyo
akasema, “Si la upendo hasa, kusema kweli ni kinyume.” Mwishowe, Socrates
aliuliza, “Je ni jambo la lazima?” Mtu huyo alijibu, “Si lazima hata kidogo.”
Socrates alimalizia kwa kusema, “kama jambo unalotaka kuniambia halina ukweli,
si la upendo na si la lazima achana nalo.”
Tunaalikwa kuongea
kwa bidii kwa sababu maneno yanagusa ndani kabisa na kuongoza uhusiano wetu na
Mungu na pia kati yetu. Ikiwa maneno yetu anasababisha uchungu kwa wengine,
sharti kwetu ni upatanisho. Hatuwezi kuishi uhusiano wa kweli na
Mungu wakati hatupatanishi na mtu ambaye tumemkosea au ametukosea. Kulingana na
Yesu, ninapaswa kuchukua jukumu la upatanisho, hata ikiwa sina hatia. Nataka
kumaliza kwa kutumia kitikio ya wimbo fulani kutoka Brazil: “Neno ni
kama lulu ndiyo, yeyote anayejua thamani yake anaongea kwa bidii; neno ni kama
moto ambayo inachoma hadi mwisho, yeyote anayejua yale anayosema atakuwa mwenye
furaha mno.”
Fr Ndega
Marekebisho: Serah Thuo
Nenhum comentário:
Postar um comentário