Kutafakari kuhusu Law 19,1-2.17-18; 1Kor 3,16-23; Mt
5,38-48
Uumbaji wa mwanadamu ulikuwa ni tendo la
upendo. Wakati Mungu alimwumba alisema: “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura
yetu.” Kwa hiyo, tangu asili binadamu ameitwa kutenda kama Mungu alivyo.
Kutenda kama Mungu ni kupenda. Ahadi yote ambayo mtu anachukua katika safari
yake duniani inapaswa kumwongoza kwenye mwelekeo huo. Hivyo, tunaweza kuelewa
sababu ya agizo la sheria katika Agano la Kale linalosema, “Muwe watakatifu kwa
kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.” Sheria hii ni njia ya utakatifu kwa
Wayahudi. Kwa sababu ya utakatifu wa Mungu, watu ambao wamechaguliwa naye wameitwa
kuwa watakatifu, na njia ya kufikia lengo hili ni “kumpenda jirani yao kama
nafsi yao wenyewe.” Matarajio ya Mungu ni kwamba waweze kutenda kama yeye
alivyo. Andiko la pili linatuambia kwamba Yesu ametupa Roho wake naye huyo Roho
anaishi ndani yetu. Hivyo maisha yetu yamekuwa hekalu la Mungu. Hii
inathibitisha wito wetu kuwa watakatifu, kulingana na mpango wa Mungu tangu
mwanzo. Uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu ni msaada ili matendo yetu yawe matakatifu.
Mafundisho ya Yesu yanalenga kuzaa uhusiano
mpya kati ya watu na Mungu na kati ya watu wenyewe. Yeye anaonyesha kuwa ukamilifu
wa Baba ni msukumo wa ukamilifu wa wana wake. Hili si jambo lisilowezekana,
bali Yesu mwenyewe anajulisha, hatua kwa hatua, jinsi ya kumkaribia Mungu hata
jinsi ya kuishi kama yeye aliyejaa upendo na ukarimu. Maneno haya “jicho kwa
jicho na jino kwa jino” ambayo Yesu aliyataja, unaitwa “Sheria ya Talioni”.
Sheria hii haikulenga kuwa msukumo kwa ajili ya ukatili ama wa kisasi, bali
“ilikusudiwa kuzuia kulipiza kisasi, na hivyo kumlinda mtu aliyefanya kosa
asipewe adhabu kubwa kuliko uzito wa kosa lenyewe.” Kweli sheria hii ilizaliwa
kwa sababu “mara nyingi adhabu ilikuwa kubwa kuliko kosa.” Hata hivyo, njia hii
iliyofundisha na Sheria hii haikuonyesha mapenzi ya Mungu, ambaye aliagiza
“wampende jirani kama nafsi yao.”
Kama nia ya Yesu ni kugundua tena mpango wa
Mungu wa kiasili, anataka kuwafundisha watu kwa njia tofauti. Yeye hawalazimishi
wasikilizaji wake kuchukua ahadi hii, bali ili waweze kumfuata kwa kweli kuna
masharti. Wakati watu wengine wanapenda tu wale wanaowapenda wao, kwa upande wa
wanafunzi wa Yesu ni masharti kuwapenda hata maadui zao na kuwatendea mema wale
wanaowachukia. Huu ni upendo bila mipaka ulio tabia ya upendo wa Kikristo.
Lengo kwa jambo hili ni tuwe watoto wa Mungu ambaye anazitoa zawadi zake kwa
wale walio wema na kwa wabaya. Anafanya hivyo kwa sababu ni tabia yake na kwa
sababu anataka tujifunze kutoka kwake. Ingawa hatustahili zawadi zake, hatuwezi
kuweka mipaka katika ukarimu wake.
Mwanafunzi wa kweli wa Yesu “hashindani na mtu
mwovu”, bali anatoa “shavu tofauti la maisha” na njia tofauti ya kutenda. Hii
inamaanisha kumpa mwingine nafasi ya kufikiri vizuri na kubadilisha matendo
yake. Hii ni pia nafasi ya kutafakari kuhusu uwepo wa uovu ulimwenguni. Hali
hii si kazi ya Mungu, bali matokeo ya uhuru wa binadamu. Mungu mwenyewe ndiye
wa kwanza anayetaka kuufuta uovu duniani na kuwaimarisha wanafunzi wa Yesu
watumie wema wa moyo na matendo mema kwa wengine bila kuzihukumu tabia zao,
yaani, “kutenda mema bila kumchagua mtu.” Kwa msaada wa Mungu tunaweza
kuibadilisha hali ya uovu kwa sababu yeye mwenyewe ana mazoea ya kubadilisha
hali mbaya kuwa hali nzuri na hali ya mauti kuwa hali ya uzima. Kifo cha Mwanae
kilikuwa tendo baya la wanadamu, lakini yeye alibadilisha hali hii mbaya kuwa
manufaa ya wokovu wao. ushuhuda wazi sana ya hili ni wakati Yesu alipokuwa
msalabani akiteswa na maadui wake, akawaombea msamaha kwa Mungu Baba. Pia
aliwatetea kuwa hawakujua walilolifanya.
Kutokana na mfano wa Kristo, anayeitwa pia “nabii
asiye na ukatili”, njia ya kipekee ya kuushinda ukatili ni kujibu kwa ishara za
amani. Yesu anataka kwamba tabia zetu zishinde mwelekeo wa kijamii kwenye
kisasi, ukatili na ukabila. Ukabila unauharibu undugu na kuukanusha utambulisho
wetu wa Kikristo. Kulingana na Baba Mtakatifu Francisco, “kipimo cha utambulisho
wetu kama watoto wa Mungu ni tabia ya huruma.” Kama wafuasi wa Yesu sisi sio
bora kuliko wengine, lakini tunapaswa kutenda tofauti, yaani kulionyesha “shavu
lingine.” “tunapowachukia maadui wetu tunawapa uwezo juu yetu: uwezo juu ya
usingizi wetu, hamu yetu ya chakula, shinikizo letu la damu, afya yetu na
furaha yetu” (Dale Carnegie). Kwa kifupi, Hatuwezi kuruhusu kuwa waovu waamue
jinsi tunavyopaswa kutenda.
Kuna hadithi fulani inayoongea zaidi kuhusu
hayo. “Mwandishi fulani anayeitwa Sydney Harris, anatuambia hadithi ambayo
ilitokea alipoandamana na rafiki yake kwa duka la magazeti. Rafiki yake
alimsalimia mwanagazeti kwa heshima sana, lakini kama jibu, mtu huyo alimtendea
vibaya. Rafiki wa Harris akikubali gazeti lililotupwa kwa njia mbaya kwenye
mwelekeo wake, alitabasamu kwa heshima na kutakia wikiendi njema kwa
mwanagazeti. Baadaye, walipotembea
njiani, mwandishi alimwuliza rafiki yake, akisema, “Mtu huyo una tabia mbaya
kwako daima?” “Ndiyo, kwa bahati mbaya, yeye alivyo.” Na wewe una tabia ya heshima
na ya kirafiki kwake daima?” “Ndiyo, mimi ndivyo.” “Kwa nini wewe ni mtu mwema
mno kwake ikiwa yeye ana tabia mbaya kwako?” “Kwa sababu sitaki kwamba aamue
jinsi ninavyopaswa kutenda.”
Ndiye Yesu mwenyewe ambaye anatualika kutenda vivyo
hivyo. Kulingana naye, uovu hauwezi kuondoa uovu, bali ni wema tu unaoweza
kufanya hivyo. Tupendane kama Yesu alivyo na, kwa njia ya upendo huu, tuweze
kuijenga jamii inayotarajiwa na Mungu kwa watoto wake.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário