Kutafakari kuhusu Is 58,7-10; 1Cor 2,1-5; Mt 5, 13-16
Kulingana na
tafakari hii Mungu alituita na kutuchagua ili tuwe vyombo vya wokovu wake. Kazi
hii inapofanyika kwa ajili ya utukufu wa Mungu inaangaza gizani na kutoa maana
kwa dunia nzima.
Kulingana na
andiko la kwanza, baada ya kuacha utumwa wa Babeli, Watu wa Israeli walialikwa
kupanga maisha yao kulingana na utambulisho wa kuwa nuru ya mataifa kwa ajili
ya utukufu wa Mungu. Mambo yote ambayo waliweza kufanya kwa ajili ya kumheshimu
na kumtukuza Mungu yalipaswa kuandamana na matendo ya haki. Hivyo, kufunga na
kusali kwao bila ahadi/mshikamano na hali ya wenzao ni bure.
Mtakatifu Paulo alitambua
kwa unyenyekevu udhaifu wake mbele ya ukuu wa kazi ya kuinjilisha. Yeye
anatenda kwa bidii ili fumbo la Kristo aliyesulubiwa lifunuliwe kwa uaminifu
akishinda kishawishi ya tafsiri kulingana na akili na hekima ya kibinadamu. Yeye
anasisitiza kwamba ni nuru ya Roho Mtakatifu ambayo inamwongoza katika kazi hii.
Maneno haya ya Mt. Paulo yanayahusu mawazo ya Mtakatifu Yohana Calabria, yaani,
“Kazi ni ya Mungu. Yeye ndiye anayetenda mambo yote. Sisi tu vyombo vyake. Yeye
atatutumia tutakapopatikana.”
Katika injili
tunaendelea kutafakari kuhusu hotuba ya Yesu mlimani. Mara iliyopita Yesu
alipendekeza njia kamili ya kupata furaha ya kweli. Njia hii inafunua nafsi
yake mwenyewe na ukaribu wa Mungu. Maisha ya wanafunzi wake yana thamani sana
kwake. Haya ni utabiri wa wakati mpya na, kwa hivyo, ni kama chumvi na nuru. Je,
katika uzoefu wetu nyumbani, chumvi inatumika kwa maana gani? Hii ni msaada kwa
ajili ya chakula ili kiweze kuonja vizuri. Chumvi ikiwa nyingi sana haifai, na
tena ikiwa kidogo sana, chakula hakiwi kitamu. Nuru ilitengenezwa ili itie nuru
na kufikia lengo lake wakati inapotoa nguvu na uhai kwa vyote. Ilitokea hivyo
tangu mwanzo, yaani, wakati Mungu aliposema “nuru ifanyike”! Nuru ilifanyika na
uhai ukatokea. Hivyo, bila chumvi chakula hakiwezi kuwa kitamu, na bila mwanga
kunakuwa na giza, na giza ni ishara ya kifo.
Mifano ya chumvi
na nuru inatusaidia kuelewa maana ya ufuasi kwa Yesu. Wanafunzi wa Yesu
hawakuwepo kwa ajili yao wenyewe tu, bali kwa ajili ya jumuiya nzima. Hao wanatenda
yaliyo mema katika jamii, na kusaidia kuyahifadhi mambo yaliyo mazuri katika
jamii hiyo. Ubatizo wetu unatusukuma tutoe ushuhuda kwa matendo yetu popote
tunapoishi na kufanya kazi, yaani, yasemwa kwetu: “Mtoto fulani, umeangazwa na
Kristo aliye Mwanga wa ulimwengu. Tembea kama mtoto wa nuru.”
Kuwepo kwa Kristo
duniani kutakuwa na manufaa pale tu, sisi wafuasi wake, tutakaposhirikiana na
wenzetu. Furaha ya mkutano wetu na Bwana haiwezi kufichika. Yapaswa kushirikika
na kutangazika. Uamuzi wa kuificha nuru inaonekana iwe tabia ya unyenyekevu,
lakini inaonekana pia iwe aibu ama kosa la ujasiri na shauku. Hivyo, nuru
haiwezi kutimiza lengo lake. Wakati matendo yetu yatendeka kwa ajili ya Mungu
hatuna sababu ya kuyaficha hayo. Hata tunapokuwa na ugumu wa kufikiria thamani
ya uwepo wetu katika jamii na jumuiya zetu, wazo hili halifuti utambulisho wetu
wa kuwa chumvi kutoa maana na kuwa nuru kutoa uhai.
Katika Biblia,
Mungu ndiye chanzo cha Mwanga na ni kwa kushirikiana na Mwanga huu, ndipo
viumbe wake wameweza kuishi na kuwa nuru ya ulimwengu. Kwa sababu ya uhusiano
wake na Baba, Yesu ni mwanga wa Mungu duniani unaotuvuta kwake. Uhusiano wetu
na Yesu unatufanya tuwe watoto wa nuru. Nuru huangaza kwa sababu inaungana na
shina lake daima. Hii ni maana ya nguvu yake. Kuhusu hayo Yesu aliwaambia
wanafunzi wake, “bila mimi hamwezi kufanya chochote. Yeye hakusema, yaani “hamuwezi
kufanya nusu ama sehemu ya kazi yenu, bali alisema “hamwezi kufanya chochote”. Ni
sharti kwetu tubaki kuunganishwa naye ili tuweze kutimiza lengo la maisha yetu.
Hivyo, ni lazima tuwe karibu zaidi na Mungu ambaye ndiye chanzo cha mwanga na
uhai wote. “Tutauleta mwanga wa Mungu kati ya wengine iwapo mwanga huo uko
tayari mioyoni mwetu.” Mabadiliko ambayo tunataka kupendekeza kwa wengine
tunapaswa kuonja kwanza. Kwa kuangaza tunahitaji kuangazwa na nuru. Kila siku
tuko na nafasi ya kusoma na kusali neno la Mungu. Ikiwa tunafanya mazoezi hayo
kwa bidii tutapokea chumvi tunayohitaji tutoe ladha na tena tunaweza kupata
nuru kwa maisha yetu ya kila siku kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
Fr Ndega
Mapitio na Marekebisho: Serah Thuo
Nenhum comentário:
Postar um comentário