Kutafakari kuhusu Isa 49,14-16; Mt 6,24-34
“Kwa njia yake ya
kututunza Mungu yu mama kuliko baba”. Maneno haya yalisemwa na baba mtakatifu
Yohane Paulo wa Kwanza na kuonyesha mtazamo tofauti kuhusu hali ya Kimungu,
kulingana na andiko la kwanza la tafakari yetu (Isa 49,14-16). Mungu ni kama
mama ndiye mpole na mwangalifu. Yeye hawezi kutusahau kwa sababu sisi tu watoto
wake wapendwa na maisha yetu yanathamini sana kwake. Anataka tuonje upendo wake
wa kimama nasi tuweze kujikabidhi mikononi mwake kwa imani kubwa. Mtakatifu
Yohane Calabria alikuwa na haya ya kusema, “Riziki ya Mungu ni kama mama mpole
anayepatia mambo yote kwa manufaa yetu sisi. Tujione kuongozwa na mikono yake
ya kimama.” Yeyote anayeishi imani kama hiyo anaweza kuenda mbele akitangaza Ufalme
wa Mungu kama kipaumbele katika maisha yake.
Kwa wale walioamua
kumfuata Yesu ni lazima kupanga maisha yao kulingana na hali mpya ambayo walichukua.
Hawawezi kutumikia mabwana wawili. Kumtumikia Mungu ni muhimu kuliko mambo
yote. Hivyo, baada ya kukutana na Kristo, pesa na mali zingine hazina maana
tena maishani mwao kama ilivyotokea kabla ya mkutano huu. Ilikuwa hivyo mwanzoni
mwa wito, yaani Yesu aliwaita; mara waliacha kila kitu... Lakini tunajua
kwamba, wakati wa safari, mara nyingi walikuwa na hofu na mashaka kuhusu kesho,
mfano Petro alipomwambia, “Na sisi je? Tumeacha yote, tukakufuata wewe;
tutapata nini basi?” (Mt 19,27). Yesu alijua mahitaji yao na kwa hivyo, akawahakikishia
maisha mapya ambayo yanajumuisha mambo hayo yote kwa njia tofauti na iliyo
bora, pamoja na kujitolea kwao kwa ajili yake. Kulingana na Mtakatifu Augustino, “Petro
aliacha ulimwengu wote na akapata ulimwengu wote. Walikuwa kama wale ambao hawakuwa
na kitu, wakati huo wana kila kitu.”
Umuhimu wa mafundisho
ya Yesu katika andiko hili ni utunzaji wa Mungu kwa ajili ya watumishi wake.
Yeye ndiye Baba mwema anayejua mahitaji ya wanae na kuwasaidia bora kuliko
anavyofanya kwa ajili ya ndege na maua ya mashamba. Yesu aliwaalika kufungua
macho na kuangalia kandokando yao. Katika Vyote kuna ishara za upendo ya Baba
huyo ambaye anashughulika hata kwa mambo madogo. Anayaongoza mambo yote
kulingana na mpango wake wa hekima na wema. Hakuna jambo ambalo linakosa
mtazamo wake wa upendo. Hivyo, tunaalikwa kufikiria kwamba tuko mikononi mwake ambapo
ni pazuri. Maandiko Matakatifu yanashuhudia hivyo, yaani “Mpaka sasa hivi Bwana
ametusaidia”, na tena “Ni nani aliyetumaini Bwana akaaibika?.” Ushuhuda huu
unatualika “kunaangalia ya nyuma na kuona jinsi Mungu alivyotutendea mema na
hivyo tunaweza kuona yale anayotufanyia sasa. Hivyo, tunaweza kuangalia mbele
kwa matumaini na imani kwamba Mungu atatutendea vile alivyotutendea”. Hii ni
njia yake ya kutenda.
Yesu hakanushi kwamba baadhi ya mambo ni muhimu kwa
maisha. Lakini anajua pia kwamba mtu anayeishi kwa wasiwasi na kusumbulika anakosa
uangalifu katika yale yasiyo muhimu sana. Ikiwa Mungu Baba anajua kwamba tunahitaji mambo hayo yote
na kutusaidia, tunaalikwa kujisalimisha mikononi mwake kwa imani kubwa na
kuzitumia juhudi zetu kwa ajili ya kujenga ulimwengu bora kila siku. Mtakatifu
fulani alisema: “Tufanye tunayopaswa kufanya kama yote yanatutegemea sisi, kwa
kumwamini Mungu kama yote yanamtegemea Mungu.” Mtakatifu Yohane Calabria aliishi
hali hii kwa hamu sana. Ugunduzi wake wa injili ulikuwa ugunduzi wa ubaba wa
Mungu. Kwa Yohana Calabria, Mungu ni Baba na Mtoaji daima ingawa hatujaishi
kama watoto daima. Alichukua maneno ya mstari wa 23 kama mpango wa maisha kwake
na kwa Familia yake ya Kiroho, yaani, “Mtafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki
yake na hayo yote mtapewa kwa ziada.” Kwa mtakatifu huyo, hapo tuko na njia
halisi ya kumjibu Mungu anayewapenda na kuwalinda wana wake bila kumsahau hata mmoja wao. Kwa hivyo, kama kutafuta kwa ufalme wake
kunayaongoza maisha yetu, “matatizo yote yapaswa kufikiriwa na kusomeka kwa maelewano
na ubaba wake” na kamwe nje yake.
Mungu anatupenda,
yeye anatujua na kwa hivyo anatutunza. Kwa utunzaji wake
maalum, yeye ameshiriki zawadi zake nasi, akitarajia tuweze kufanya vivyo hivyo
kwa ajili ya wengine ili undugu kati yetu uwe maonyesho ya ubaba wake. Basi, tunaalikwa kuchukua historia yetu ya maisha na kutambua kwamba
tumepokea sana. Ingawa sisi hatupokei daima yale tunayomwomba yeye, tuwe na
uhakika kwamba yeye ametupatia daima tunayohitaji. Hivyo, tufanye upya imani
yetu katika riziki yake kwa maana yeye yu BABA, MAMA, YOTE naye hawaachi
wale wanaomtumainia.