Kutafakari kutoka Kum
8,2-3.14b-16a; 1Wak 10,16-17; Yoh 6, 51-58
Tunasherehekea
sikukuu ya Mwili na Damu Ya Kristo kilicho chakula kinachodumu milele, yaani
Ekaristi takatifu. Hii ni sakramenti ya uwepo hai wa Yesu kati yetu. Asili ya
sherehe hii ni Karamu ya mwisho katika Alhamisi Takatifu lakini hali ya ukimya
na tafakari kwa sababu ya Ijumaa Kuu inatuzuia
kusherehekea sikukuu ya Ekaristi kwa furaha kubwa. Kwa hivyo Baba
Mtakatifu Urbano wa IV katika karne ya 13 alianzisha sherehe hii ya Mwili na
Damu ya Kristo. Katika sikukuu hii tunaweza kutangaza hadharani imani na upendo
wetu kwa Ekaristi Takatifu na kujiona kuungana na Kristo anayefanya upya ishara
yake ya upendo kwa ajili ya wokovu wetu na kutualika kwenye karamu ili tuweze
kushiriki furaha yake kubwa na uzima wa milele.
Somo la kwanza ni
uthibitisho kwamba ndiye Mungu mwenyewe anayewalisha watu wake. Muda ambao Watu
wa Israeli waliishi jangwani ulikuwa nafasi ya kumjua Mungu kama Mtoaji ambaye
aliwapatia chakula tofauti na kile cha Misri. Walipokea Mana kutokana na
ukarimu wa Mungu kwa ajili ya kufanya upya nguvu zao za kimwili na kuwaimarisha
kumshukuru Mungu aliyekuwepo miongoni mwao daima.
Kulingana na somo
la pili, Mtakatifu Paulo anasema kwamba chakula ambacho Mungu anawapatia watu
wake wapya ndiye Mwanawe. Yeye anatualika sote tule mwili na kunywa damu yake
ili tuwe wamoja naye. Ingawa sisi ni wengi tumefanyika mwili mmoja kwa sababu
ya Mkate mmoja tunaoumega ulio Kristo mwenyewe. Ndio umoja kati yetu na ahadi
ya kindugu ambayo inaufanyisha ujumbe na ushuhuda wetu uwe wa kweli.
Katika injili
Kristo aliwaalika wasikilizaji wake kuukaribisha ufunuo juu ya utambulisho wake
kama chakula kilichoshuka kutoka mbinguni si kwa binadamu tu bali kwa ajili ya
uhai wa ulimwengu wote. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata
alimtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa
milele (Jo 3, 16)”. Mwana anajitoa kama chakula kinachodumu hadi uzima wa
milele kwa sababu ya mapenzi ya Baba aliye chemchemi ya uzima. Yeye ndiye
anayesababisha uzima ndani ya kila mtu anayempokea Mwanawe.
Tunaongea hapa
kuhusu kiini cha mafundisho ya Yesu kama mwokozi na mkombozi wa ulimwengu,
lakini wasikilizaji wa Yesu hawakuweza kuelewa kwa sababu walijua hali ya Yesu
ya kibinadamu. Waliwajua wazazi wake, yaani Yusufu na Maria na kushiriki pamoja
naye katika shule moja. Hakika hawakuweza kukubali kwamba mwenzao huyu alishuka
mbinguni. Zaidi ya hayo kulingana na mawazo ya Kiyahudi mwili ni mfano wa
udhaifu wa kibinadamu. Lakini ugumu wao wa kufahamu fumbo hilo haukumzuia Yesu
kufunua njia yenye maana kamili kwa maisha yao.
Yesu anaongea
kuhusu uzima bila mwisho unaopatikana kwa wote. Inawezekana kuupokea uzima huu
kwa kuula mwili wake na kuinywa damu yake, kwa sababu yeye ndiye uhai na huishi
ndani ya wale wanaompokea. Yesu anatenda ishara hii ya upendo kwa uhuru kabisa
na kulenga kukaa miongoni mwa wanadamu na ndani ya kila mtu. Hiki ndicho kipimo
cha kupata uzima. Hilo ndilo fumbo la Ekaristi takatifu. Ndiyo zawadi kutoka
kwa Mungu ambaye hataki kuishi mbali na binadamu.
Ekaristi ni
hazina ya kanisa na kiini cha uzoefu wake. Ekaristi inalifanya Kanisa na Kanisa
linaishi kwa sababu ya Ekaristi. Kulingana na Mtaguso Mkuu wa Vatikano wa pili,
“matendo yote ya Kanisa yatoka kwa Ekaristi na kulenga Ekaristi”. Ndivyo hivyo
kwa sote tunaoumega mkate mmoja na kunywa kikombe kimoja. Uzoefu huu ni
ukamilifu wa ushirika wetu na Mungu na msukumo kwa ahadi yetu ya kindugu.
Yesu ndiye
chakula ambacho Mungu alitupa na kuendelea kutupa ili tuwe na maisha kamili.
Kutoka Umwilisho wa Neno mpaka msalaba na Ufufuko, maisha ya Yesu yalikuwa
kujitolea daima kama chakula cha Mungu kwa ajili ya maisha ya watu wake.
Ekaristi takatifu tunayosherehekea inatuhakikishia kwamba ukarimu wa Mungu
haumaliziki, kweli utaendelea hata milele. Kila siku Kristo hufanya upya ishara
yake ya upendo kwa ajili ya wokovu wetu.
Ndiye Yesu
mwenyewe ambaye anatualika kwa karamu ya uzima, akijitoa kama chakula na
kututumikia kama Yule ya pekee ambaye anaweza kujaza moyo wetu unaomtamani
Mungu na uhai wake sawa. Lengo la Ekaristi ni kufananisha maisha yetu kidogo
kidogo kulingana na maisha ya Yule tunayepokea.
“Tunapokula
chakula cha kawaida mwili wetu unaingiza chakula hiki ili uwe na afya nzuri.
Hivyo, chakula kinaingizwa na mwili wetu. Kuhusu Ekaristi, chakula cha uzima,
matokeo ni tofauti: wakati tunampokea Yesu, ni sisi tunaoingizwa naye”. Kwa
maneno mengine, Yesu anatuingiza, anatuchukua kwake ili tuishi naye na kwa
sababu yake. Yeye anakaa ndani yetu nasi ndani yake. Yeye anatuunganisha naye,
kutuhusisha katika ushirika sawa anaoishi na Baba. Katika uzoefu huu
tunabadilika kuwa yule tunayempokea kwa ajili ya ukuaji wa mwili mmoja. Hivyo,
wakati tunaposherehekea Ekaristi kwa kina mahusiano kati yetu yabadilika na
kupata nguvu na sisi tunakuwa vyombo vya umoja, upatanisho na amani kulingana
na hisia za Kristo.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário