Kutafakari kuhusu Mdo 1, 1-11; Waef 1, 17-23;
Lk 24, 46-53
Siku ya leo
tunasherehekea kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye alifanya kazi miongoni
mwa wanadamu kwa miaka mitatu. Kupaa ni hitimisho ya kazi yake, lakini
anaendelea kuwepo ulimwenguni kupitia Roho wake. Basi, sikukuu hii inatufafanulia
fumbo la kuaga na uwepo wa Yesu kwa sababu yeye hakumwacha Baba alipokuja kwetu
wala hakutuacha alipomrudia Baba. Kupaa kwake kunaongea kuhusu njia mpya ya
uwepo wake miongoni mwetu kwa kutangaza hatua mpya ya kazi yake. Huu ni wakati
wa Kanisa lililo jumuiya ya wanafunzi wa Yesu. Ujumbe muhimu kuhusu hali hii ni
wazi sana hasa katika maandiko mawili ya Luka, yaani, Injili na kitabu cha Matendo
ya Mitume. Katika Injili yeye anajulisha vitendo vya Yesu, na katika Matendo ya
Mitume anajulisha vitendo vya wanafunzi wake waliosaidiwa na Roho wake
Mtakatifu.
Kuonekana kwa Yesu
kwa muda fulani kuwaimarisha wanafunzi wake kugundua tena maana ya uanafunzi, wakishinda
hofu na mashaka kuhusu hali ya ufufuko wake. Uzoefu huo ulikuwa mpya sana kwao
naye Yesu alifahamu kwamba alipaswa kuwa na utulivu kwa sababu ya imani yao
ndogo. Mwendo ulikuwa wa muda mrefu, lakini wenye ufanisi sana, ukisababisha
mabadiliko makubwa maishani mwa wanafunzi, yaani, kutokana na uzoefu wa wanaume
wenye hofu kuwa mashahidi wenye ujasiri.
Katika maneno
yake ya mwisho, Yesu aliwasaidia kufahamu uhusiano kati ya yale aliyoyatenda na
kufundisha na yale yaliyoandikwa na manabii wa zamani. Habari ya toba na
ondoleo la dhambi linapaswa kuwa umuhimu wa ujumbe wa waliotumwa kwa jina la
Yesu aliye uso wa huruma ya Mungu Asiyeonekana. Uzoefu wao na Yesu uliwawezesha
kuwa wanafunzi wa kweli, lakini walipaswa kuingoja nguvu kutoka juu ili waweze kuwa
mashahidi wa Bwana Yesu tangu Yerusalemu mpaka mwisho wa nchi. Roho mmoja aliyekuwepo
katika mwanzo wa uumbaji na wakati wa utume wa Yesu ataiongoza kazi ya wanafunzi
wake.
Yesu aliyashiriki
mamlaka yake na wanafunzi wake ili wawatumikie watu, wakiwatendea mema. Kutokana
na mfano wa kujisalimisha kwa Kristo ushuhuda wao wa kwanza ni kujitolea bila
kipimo. Wanafunzi walitumwa kama wajumbe
wa habari njema kwa mataifa yote kwa sababu injili haina mpaka. Yesu alikuwa
amewaahidia kuandamana nao mpaka upeo. Ingawa uwepo wake wa kimwili hauwezi kuonekana
tena, Roho wake anawahakikishia kwamba hawatendi peke yao katika kazi. Uwepo wa
Roho wa Yesu ulifanya maneno yao yawe ufanisi kupitia ishara nyingi na matendo
mazuri.
Kulingana na
Mtakatifu Paulo, Roho ambaye aliwapewa kwa jumuiya ya kwanza ni Roho wa umoja.
Kupitia Roho huyo tunaweza kumjua Mungu vizuri na kuishi katika umoja miongoni
mwetu kama anavyotarajia Bwana wetu. Kila mtu anaitwa kuchukua ahadi hii ya
umoja kama maana ya utambulisho. Katika jumuiya ya Kikristo tumezipokea zawadi
nyingi kutoka kwa Mungu ili tuwe zawadi sisi kwa sisi, na kusaidia kujenga mwili
mmoja, ambao ni takatifu na hai kwa sababu ni Roho mmoja anayetenda ndani yake.
Hili ni fumbo la uwepo wa Yesu katika kanisa lake ambalo ni mwili wake mwenyewe
naye yu kichwa cha mwili huu.
Malaika
waliwaambia wanafunzi wa kwanza na kutuambia pia siku ya leo: “mbona mmesimama
mkitazama mbinguni?” Hakika kama Wakristo tunahitaji kurudisha mtazamo wetu kwa
Yesu aliye mfano wetu na kichwa chetu ili tuendelee kazi yake kwa uaminifu,
lakini hatuwezi Kubaki wamesimama kutazama mbinguni kama ishara ya uvivu na utazamaji
na kipooza. Bwana anatutaka tuwe waangalifu na wenye ufanisi kama
ilivyoandikwa: “Wabarikiwa watumishi wale ambao watakuwa wakitumikia Bwana wao
atakaporudi”. Maisha ya Kikristu ni kutafakari na kitendo, imani na matendo.
Ishara za uwepo ufanisi wa Yesu zinaonyeshwa kupitia mapendo ya wale wanaomwamini
na kuzifuata nyayo zake. Roho Mtakatifu afanye uwepo wa Yesu uwe ufanisi katika
maisha yetu na kazi zetu ili tuendelee utume wake kwa uaminifu.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário