Mit 8: 22-31; Rum 5: 1-5;
Yoh 16,12-15
Utatu Mtakatifu
ni fumbo la Mungu aliye ushirika wa Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, yaani
fumbo la upendo. Upendo ni utambulisho wa Mungu. Hivyo, “Mungu ni Utatu kwa
sababu ndiye upendo”. Yeye ni Mungu wa kipekee lakini haishi peke yake kwa
sababu alitaka kuwa ushirika wa upendo. Uumbaji wote ni uenezi wa nafsi yake na
fumbo lake. Viumbe vyote vinaitwa kuingia katika ushirika huu wa upendo na kuwa
maonyesho ya wema wake. Tunaposema ishara ya msalaba, yaani, “Kwa jina la Baba
na la Mwana na la Roho Mtakatifu”, tunakiri kwamba nafsi yetu ndiyo makao ya
uwepo maalum tangu ubatizo wetu. Ndio uwepo wa upendo na kutuomba uhusiano wa
upendo nawe. Inawezekaje Mungu Mkubwa mno akae ndani yetu wadogo mno?
Hilo ndilo fumbo
kubwa kuliko yote ya imani yetu. Kutoka ufunuo wa Yesu tunapata kujifunza mengi
na kuendelea kwa msaada wa Roho Mtakatifu ili tujihisi kuhusishwa katika fumbo
hili hata bila kufahamu kamili. Kuna hadithi fulani inayoongea zaidi kuhusu
hali hii: “Siku moja Mtakatifu Agostino alikuwa akitembea katika pwani ya
bahari, akijiuliza swali kuhusu fumbo la Utatu Mtakatifu, akisema, “inawezekanaje
Mungu kuwako kama Mmoja na Utatu wakati huo huo? Ghafla, alimwona mtoto mdogo
aliyefanya shimo katika mchanga na kukimbia kwenye bahari, akichukua maji
kidogo na kuyaweka shimoni. Baada ya kuangalia mchezo huu wa mtoto mdogo kwa
mara nyingi, Agostino aliamua kumwuliza maana ya mchezo huo. Mtoto mdogo
akamjibu akisema: “Najaribu kuweka maji yale yote ndani ya shimo hii”. Ameshangaa
sana, Agostino akasema: “Hutapata kufanya hivyo kamwe!” Kisha, mtoto mdogo akamwambia
akisema: “ni rahisi kwangu kuyaweka maji yale yote shimoni kuliko wewe ukapate
kufahamu fumbo la Utatu Mtakatifu kwa akili yako. Mwishowe, mtoto mdogo alitoweka
na Mtakatifu Agostino akajiambia mwenyewe: “Labda mtoto huyo alikuwa malaika
fulani!”
Hadithi hii inatufundisha
hali muhimu sana, yaani, fumbo la Utatu Mtakatifu sio fumbo la kufahamika bali
la kukaribishwa. Ikiwa tunajifungua zaidi kwa fumbo hili tunaweza kuhisi zaidi fumbo
hili ndani yetu. Ujumbe wa masomo ya leo unatusaidia katika mwendo huu. Katika
somo la kwanza hekima anajifunua kama nafsi ya Mungu. Hekima hii ni Mwana wa
Mungu ambaye yuko pamoja na Mungu milele na kutenda naye kabla ya kuumbwa ulimwengu.
Yeye ni Akili ya Mungu na viumbe vyote vilivyokuwako viliumbwa kwa njia yake,
pamoja naye na ndani yake. Yeye ni ukamilifu wa viumbe vyote. Somo la pili
linatuambia kwamba Mwana alitushirikisha katika utukufu wake na Baba. Kupitia
yeye tulipewa Roho Mtakatifu ili tuishi kama watoto. Tendo la Roho huyu limemimina
mioyoni mwetu pendo la Mungu likithibitisha kwamba sisi ni watoto wake na hivyo
tunaweza kumwita Baba yetu kwa uhuru kabisa. Ikiwa sisi ni watoto sisi pia ni
warithi pamoja na Yesu kwa kupokea uhai wake wa kimungu. Ndiyo hali hii ambayo ubatizo
wetu unatufanya kuishi.
Umuhimu wa ujumbe
ambao Yesu ametukabidhi ni kwamba yeye ndiye ukweli wa Baba na kutenda kwa Roho
Mtakatifu. Mungu ndiye Utatu na hutenda pamoja kwa ushirikiano kamili. Yesu,
aliyetumwa na Mungu Baba, alitangaza ukweli akiwahusisha watu katika ushirika sawasawa
anaoishi Baba na Roho Mtakatifu. Utimizaji wa ahadi kuhusu ujio wa Roho huyo
unatuhakikishia umoja wetu, kutuunganisha kama wana wa familia moja. Kupitia
Roho huyo tunaangazika ili tuweze kukumbuka mafundisho ya Yesu na kuyatangaza
kwa uaminifu. Wakati sisi hupendana tunaonyesha ukweli wa uhusiano wetu na
Mungu na hali ya Mungu mwenyewe kama Utatu Mtakatifu. Tunapoishi uhusiano wa kweli
na Yesu vivyo hivyo tunahisi ndani yetu tendo la Baba na Roho wake. Uzoefu wetu
wa Yesu katika Ekaristi ni uzoefu wa Utatu Mtakatifu. Mungu anatumikia anakaa
kati yetu na ndani yetu. Yeye anatuunganisha naye na miongoni mwetu. Hili ni
fumbo la ushirika ambao Mungu ametuhusisha kwa maana anataka tuwe washiriki
katika uhai wake mwenyewe. Kwa hivyo, tuombe atukuzwe Mungu Baba na Mwana na
Roho Mtakatifu...
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário