Nabii Amosi
alichaguliwa na Mungu ili kutabiri katika hali ngumu ya watu wa Israeli (Ufalme
wa Kaskazini), yaani, kukosekana kwa usawa wa kijamii, udhalimu dhidi ya
maskini na matumizi ya dini kulingana na mvuto binafsi wa mfalme. Wakati wa
mfalme Yeroboamu wa II, pamoja na hekalu kuu la Yerusalemu (Ufalme Kusini) lilikuwako
pia hekalu lingine lililoitwa Betheli (Kaskazini). Amosi alipoanza kazi yake
katika mahali huko, alikutana na kuhani wa hekalu la Betheli, aliyeitwa Amazia,
ambaye alifanya upinzani dhidi ya unabii wa Amosi. Amazia ni aina ya mtu
aliyelipwa ili kudumisha mfumo wa hekalu na kuhalalisha mfumo wa kidhalimu wa
mfalme. Ingawa Amosi alitendewa vibaya, tabia yake ni tofauti, yaani
alipendelea kumwelezea Amazia maana ya wito wake. Ujumbe wa Amosi kama nabii
hautegemei malipo, bali ni maonyesho ya ukarimu na mapenzi ya Mungu anayeruhusu
kuguswa na hali ya maskini na ya wanaoteseka.
Somo la pili ni wimbo
wa shukrani kwa Mungu ambaye ametubariki sana katika Kristo tangu mwanzo wa
ulimwengu ili tuwe watoto wake. Kwa ujumbe wa Yesu Kristu tumesamehewa dhambi
zetu ili tuweze kuishi wito wetu kwa utakatifu. Wito huu ni sehemu ya mpango wa
hekima na wema wa Mungu ambaye katika Kristo ametuchagua ili tuwe watu wake
mwenyewe. Roho wa Mungu anatusaidia kuishi wito wetu kwa uaminifu na kutupatia
utimizaji wa ahadi yake. Kulingana na Baraza ya Vatikano ya II utakatifu ni
wito wa wote tangu ubatizo wetu na Mt Yohana Calabria anasema kwamba “hatuhitaji
kufanya mambo ya ajabu ili tuwe watakatifu. Tunaweza kuwa watakatifu kupitia
hali ya kawaida. Yatosha nia zetu ziwe takatifu katika mambo yote.”
Baada ya kukataliwa
kijijini chake, Yesu aliendelea na ujumbe wake vijijini vingine kandokando huko
ambapo alikaribishwa vizuri sana. Aliweza kufanya kazi yake peke yake, bali
hakutaka. Kwa hivyo aliwaita Mitume kumi na wawili kama washirika. Kabla ya
kuwatuma kwa ujumbe, aliwaita ili kubaki naye, yaani aliwapendekezea uzoefu wa nafsi
yake. Uzoefu huu ni wa msingi kwa mafanikio ya kazi. Wakati huu alishiriki nao hisia
yake kuhusu hali ya watu walioteseka kwa sababu ya nguvu za maovu na ya
magonjwa mengi. Mamlaka ambayo Yesu alishiriki nao yalilenga kuwaimarisha watu
ili waweze kushiriki kikamilifu katika jamii. Hatimaye, aliwapa maelekezo hasa
kuhusu mahitaji ya njia ya unyenyekevu wa maisha na kuwatuma wawiliwawili.
Ndiye Yesu aliyechukua
nafasi ya kuwaalika wanafunzi. Hakuwatafuta wenye nguvu au wenye umaarufu
katika jamii. Aliwachagua watu wanyenyekevu, wafanyakazi na walio makini kwa ufunuo
wa Mungu kupitia Mwana wake. Yaliyomo ya maelekezo Yesu aliyowapa yanaufuata
mwelekeo tofauti kabisa na matarajio ya binadamu. Kwa mafanikio katika kazi,
mitume walipaswa kushinda baadhi ya tabia za binadamu ambazo zipo sana maishani
mwetu: dhidi ya tabia ya kutenda kwa njia ya kibinafsi, tunaalikwa kutenda
pamoja na kusaidiana katika jumuiya na kwa manufaa ya jumuiya. Kazi ya
kuinjilisha sio kazi ambayo mtu anachukua peke yake bali ndiyo kazi ya
kijumuiya. Dhidi ya tabia ya kutawala, Yesu anashiriki nasi uwezo wake ili
tutumikie watu; dhidi ya tabia ya kuwa na mali, Yesu anatupendekezea kujinyima,
unyenyekevu na ukarimu.
Kama wanafunzi wa
kwanza tunapaswa kufahamu kwamba tajiri yetu ndilo ujumbe ambao Mungu
anatukabidhi. Siyo mali ambayo inaweza kutuhakikishia usalama, bali ndiye Yule
ambaye aliyetualika, akatutuma na kuandamana nasi. Dhidi ya tabia ya
kulazimisha, tangazo letu ni pendekezo, pendekezo la toba na la mabadiliko ya
maisha. Ikiwa mtu fulani hataki kupokea ujumbe wetu, hatuwezi kumlazimisha bali
kuheshimu uhuru wake kwa sababu ni kwa uhuru ambao mtu anaweza kukubali
pendekezo la Yesu na kumfuata. Wakati tunapokabiliana na upinzani dhidi ya kazi
yetu Yesu anatarajia tuweze kushinda hofu na kufanya upya imani yetu katika
Riziki ya Mungu ambaye hawaachi wale wanaotumainia yeye. Njia yetu ya kuishi
inaongea zaidi kuliko maneno yetu. Pendekezo la toba ambalo tunawatangazia wengine liwe maonyesho ya mabadiliko
ambayo tumeona kwa kupitia uzoefu wetu wa huruma ya Mungu. Mungu anataka kuyapatia
maisha mengi kwa watu wake na kuamua kututumia kama washirika wake. Tuko
tayari?
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário