domingo, 3 de dezembro de 2017

BWANA WETU ANAKUJA KUTUPA FURAHA NA WOKOVU


Kutafakari kuhusu Isaya 63: 16-17; 64: 1, 4-8; 1Wak 1, 3-9; Mk 13: 33-37


Kulingana na liturjia ya Kanisa Katoliki, tunaanza wakati mpya uitwao Majilio. Wakati huu unatukumbusha Ujio wa kwanza wa Bwana Yesu na kutuandaa ili tusherehekee sikukuu ya kuzaliwa kwake katika Krismasi. Tena Majilio yaimarisha matumaini yetu juu ya kuja kwake mara ya pili katika mwisho wa umri. Ujio wake kama Bwana wa maisha yetu na wa historia hauleti hofu bali furaha. Masomo haya ndio mwaliko wa kukesha ili tutambue na kuzikaribisha ishara za uwepo wa Bwana katika hali yetu ya kila siku. Ndio mwaliko pia wa shukrani maana Bwana anakuja kukutana nasi daima, ili kutupa wokovu wake. Matukio yote makuu yahitaji maandalizi mema na ndani ili kusherehekewa mema. Hivyo ndivyo Majilio kama maandalizi ya tukio kuu la Krismasi.
Katika somo la kwanza, nabii Isaya alimwelekea Mungu maombi ya imani na upendo, akimtambua kama Baba. Nabii huyo anaongelea uaminifu wa Mungu anayewaokoa watu wake, na tena kosa la uaminifu wa watu kwa ajili ya Agano. Upinzani dhidi ya maongozi ya waliotumwa na Mungu uliwafanya watu wajione mbali na Mungu. Maombi ya nabii ni faraja na msaada ili kufufua matumaini katika Bwana ambaye yuko tayari kutoa nafasi mpya kwa yeyote anayetaka kumrudia yeye. Katika somo la pili, Paulo anamshukuru Mungu, kwa sababu ya tendo la neema yake katika jumuiya ya Wakorintho, ambayo imezaa matunda mazuri kama jibu la tendo hili. Jumuiya hii inatarajia ujio wa Bwana sio kwa njia yoyote bali kwa imani halisi iliyo maonyesho ya ahadi yao kwa karama ilizopokea. Matakwa ya Mtakatifu Paulo ni kwamba jumuiya hii iendelee kwa imara katika ujumbe uliotolewa kuhusu Yesu na kukua katika imani kwake anayeaminika.
Katika Injili, Yesu anazungumza kuhusu fumbo la Kuja kwake. Ni sehemu ya mpango wa hekima na wema wa Baba. Ikiwa tunachukua mwanzo wa  sura ya kumi na tatu ya Marko, tunatambua kwamba Yesu anaongea kuhusu uharibifu wa hekalu la Yerusalemu na kuendelea kwa kuongelea dhiki ya mti huu. Tena anajali kuhusu nabii wa uongo na haja ya uvumilivu katika ushuhuda mpaka upeo ili kupokea wokovu. Wokovu ndio zawadi ya ujio wa Bwana ambao, kulingana na andiko hili hakuna yeyote ambaye anajua wakati kamili wa tukio lake. Wote wanaalikwa kukesha. Baadhi ya mifano inatusaidia kuingia vizuri katika mwendo wa ujio huu:
Kipengele cha kwanza ni wazo wa wakati. Tuko na maneno mawili ya Kigiriki ili kuongea kuhusu wakati, yaani Kronos na Kairos. Neno ambalo andiko hili linatumia ndilo Kairos linalomaanisha wakati mwafaka, nafasi ambayo Bwana anatupa. Bwana haji ili kuadhibu bali kuleta furaha: tuwe macho ili kuchukua nafasi ya kuwa wenye furaha! Kipengele cha pili ni mtu mwenye kusafiri. Huyo ndiye Yesu aliye Mwenye nyumba na Bwana wa historia. Cha tatu ni watumishi. Katika biblia, watumishi ni wale ambao walitoa maisha yao kwa ajili ya mpango wa Mungu. Cha nne ni nyumba: ndiyo jumuiya ya wanafunzi ambao waliingia katika ufalme kwa sababu walikubali pendekezo la nane heri. Bwana alimkabidhi kila mtu mpango wake na kutaka kuwazawadisha watumishi ambao wanakesha ili kushiriki naye furaha yake.
Cha tano ni Bawabu. Huyo ndiyo dhamiri ya kila mtu ambayo inapaswa kukesha ili kuepuka ingizo ya mtu mgeni yeyote ambaye anataka kuwa mwenye nyumba. Tunaalikwa kuwa macho ili tutambue Bwana anapokuja na kuufungua mlango kwake peke yake. Yeye anataka kukutana nasi na kutaka tena tubaki katika ushirika naye. Anatarajia kukaribishwa vizuri, kulingana na maneno yake mwenyewe: "Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami” (Apocalypse 3, 20). Kipengele sita ni usiku. Usiku ni ishara ya giza na dhambi. Wakati tunaposema kwamba Bwana anakuja usiku inamaanisha kwamba anakuja kama mwanga ili kufukuza giza, chambi, huzuni na kuanzisha hali mpya kabisa.  
Basi, Kuja kwake Bwana badala ya kuwaogopesha watu, kunayaimarisha matumaini katika wokovu wake, kwa sababu yeye ni Mwokozi na kuja ili kuokoa. Safari ya Kikristo ni safari ya furaha ili kukutana naye kwa sababu yeye huja daima kukutana na sisi. Uwepo wake ni dhamana ya ulinzi, kulingana na maneno yake mwenyewe: “Nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia ulimwengu mzima... Naja kwako upesi (Apoc. 3, 10b-11a). Kutoka upande wetu ni muhimu kuwa macho kwa kuja kwake ili kumkaribisha kwa upatikanaji na uaminifu. Maonyesho halisi ya makaribisho huu ndio utumishi wetu katika jumuiya kwa ukarimu na furaha.

Hivyo, Majilio ni wakati wa kufanya upya ahadi yetu na Bwana, katika mwendo wa mabadiliko daima. Kuhusu hili, Bwana anatuambia tena: "Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo. Lakini ninalo jambo moja dhidi yako: wewe hunipendi tena sasa kama pale awali. Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukatubu na kufanya kama ulivyofanya pale awali” (Ufu 2, 3-5a). Kusali zaidi na kupatikana ni tabia za mwanafunzi wa kweli anayejua Bwana wake naye uko tayari daima ili kumkaribisha. Kukesha kwa uaminifu na ukarimu ni ishara halisi ya matarajio yetu kwa ujio wa Bwana.

Fr Ndega

Nenhum comentário: