Kutafakari kuhusu Is 45: 1,4-6; 1 Thes 1: 1-5; Mt 22:
15-22
Maandiko haya yatualika kutafakari kuhusu vipengele
viwili vya msingi: cha kwanza, ni kuhusu hisia yetu ya kuwa mali ya Mungu kama
wana wa watu wake; cha pili, ni kuhusu jukumu letu katika maendeleo ya Taifa
letu kwa kupitia malipo ya kodi halali. Kama Wakristo, tunakiri umuhimu ya
kodi, lakini tunajua pia kuwa kodi ama pesa sio rejeo la maisha, ni msaada tu.
Hatutaki ichukue nafasi ya Mungu maishani mwetu.
Somo la Kwanza ni mtazamo wa imani kuhusu ushindi wa
Koreshi, mfalme wa Uajemi, ambaye aliwakomboa Wayahudi kutoka mamlaka ya
Babeli. Kulingana na Isaya, ushindi wote wa Koreshi haukuwa uwezo wake, bali
tendo la Mungu ambaye alimchagua Koreshi kama mjumbe wake ili kufanya Jina la
Bwana lijulikane kwa Mataifa yote na kuyaalika kumwamini Mungu. Ingawa Koreshi
alikuwa mfalme ambaye hakumjua Mungu wa Israel, alichaguliwa kwa ajili ya kuwa
ni chombo cha ukombozi. Wayahudi waliweza kurudi nyumbani na kuishi utambulisho
wao kama Watu wa Mungu kwa uhuru kabisa.
Paulo na wenzake wa kuinjilisha wanatambua Vipawa vya
Mungu katika Jumuiya ya Wathesalonike, hasa fadhila za imani, upendo na
tumaini. Paulo aliwaelekeza maneno ya kutia moyo ili waweze kuendelea safari
yao kwa shauku kama wachaguliwa wa Mungu ili kufanya kazi kubwa kwa kupitia
ushuhuda wao. Ndiye Roho ambaye anasababisha matokeo mema ambapo watu
wanachukua ahadi kwa ajili ya kazi ya Mungu.
Katika injili, tuko na vikundi viwili vilivyopingana wao
kwa wao, lakini walipata kukusanyika na kukubaliana ili kumpinga Yesu. Hao
walimjia Yesu na kumsifu kwa fadhila zake, yaani walisema kwamba Yesu ni mtu wa
kweli, anayefunza njia ya Mungu kulingana na ukweli. Ingawa waliuongea ukweli
kuhusu Yesu, hawakukubali njia ya maisha ambayo Yesu alipendekeza. Jambo la
mazungumzo yao ndilo kodi, yaani “Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?”
Yesu alitambua nia mbaya katika swali hili. Akisema “ndio” angechukuliwa kama mshirika wa utawala wa Warumi dhidi ya
Wayahudi. Akisema “hapana” angechukuliwa kama mwasi. Basi, Yesu aliiomba sarafu na baada ya kuitazama, aliwaambia
kwa hekima, yaani: “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari na mpeni Mungu kilicho
cha Mungu”.
Kutokana na maoni yenyewe ya wapinzani wa Yesu tuko na
kipengele kimoja muhimu sana kuhusu utambulisho wa Yesu na kazi yake, yaani
yeye ndiye mtu wa kweli. Mafundisho yake yana nguvu ya kusababisha hali mpya
maishani mwa watu kwa sababu ya ukweli. Wanafunzi wa Mafarisayo na wengine
wanapaswa kukiri kwamba ukweli kama huu hawawezi kuukuta katika mafundisho ya
viongozi wao. Akifundisha, Yesu analenga kuwakomboa kutoka unafiki na wazo la
uongo juu ya mapenzi yake ambao unawavuruga kuwa na uhusiano mwema na Mungu.
Wakati Yesu
alipochukua sarafu aliona picha ya Kaisari. Mtawala huyo wa
Roma alipiga chapa picha yake katika fedha kwa kusisitiza utawala wake juu ya
watu wengi, alijiona kama amestahili heshima ya mungu. Kwa hivyo, Yesu
aliwakumbusha kuhusu amri ya kwanza ambayo inakataza kufanya sanamu ya Mungu kwa
sababu ya hatari ya ibada ya sanamu. Kwa jibu lake Yesu alianzisha tabia kamili
kumhusu Kaisari na tabia kamili kumhusu Mungu. Watu walio wa Mungu wanamchukua
Mungu kama kipaumbele juu ya kila kitu.
Mahali pa kwanza katika maisha yetu ni kwa Mungu. Wakati
hatuko na tabia kamili katika uhusiano wetu na Mungu tunakosa pia tabia kamili
kuhusu mali, pesa na kadhalika. Yesu hakukataa umuhimu wa malipo ya kodi halali na tena heshima kwa serikali,
kinyume, aliweka kama sehemu ya utambulisho wa wanafunzi wake kushirikiana na
maendeleo ya jamii. Lakini anatukumbusha kwamba Mungu peke yake anastahili
kuabudiwa. Hata serikali yetu inaweza kufanya mapenzi ya Mungu ikiwa inatumia
mamlaka yake kwa ajili ya kusaidia maisha ya heshima kwa wote. Tunaalikwa
kufanya upya ahadi yetu kama wana wa Mungu na mali yake na kusaidia maendeleo
ya haki na amani katika jamii yetu.
Fr Ndega
Mapitio ya kiswahili: Christine
Nenhum comentário:
Postar um comentário