Kutafakari kutoka Sf 2,3;3,12-13; 1Cor 1,
26-31; Mt 5, 1-12
Tafakari yetu inasisitiza kwamba njia
kamili ya kumtafuta Mungu inapitia kwa unyenyekevu na haki. Yeye hana macho kwa
waliotenda udhalimu wala kwa wanafiki bali kwa wanyenyekevu na kwa maskini. Yeye
yu makini sana kwa kilio chao naye yuko tayari kuwatendea mema kwa maana maisha
yao yana thamani kubwa kwake. Kupitia Yesu, yeye anatoa maneno ya faraja
akionyesha upendo maalum hasa kwa maskini na wanyenyekevu kwa sababu wanamtumainia
yeye.
Katika andiko la Kwanza, nabii Sefania
anatambua ndani ya maskini na wanyenyekevu uwezo mkubwa wa kumtafuta Mungu na
kumtegemea yeye katika mambo yote. Mungu anaijua hali ya maskini na ya wanyenyekevu
naye anaguswa na mahitaji yao. Maisha ya maskini na ya wanyenyekevu yanashuhudia
kimbilio ambalo linatuhakikishia usalama sio pesa wala ulaji/ukusanyaji, bali
ni Mungu peke yake. Kweli Mungu anapatikana kwa wale wanaotaka kukutana naye,
lakini ndio wanyenyekevu wa moyo tu wanaoweza kuuona uso wake. Bila tabia hii
ni ngumu tukubali mipango ya Mungu kwa maisha yetu. Kulingana na Mtakatifu Paulo,
sisi tulio jumuiya ya Kikristo, hatujaitwa kuifuata hekima ya kibinadamu wala
kuutafuta umaarufu wa kijamii. Wito wetu unatoka kwa Mungu na kuyafuata mawazo
na njia zake kama Kristo mwenyewe alivyo.
Andiko la injili ni mwanzo wa ile
iliyojulikana kama “Hotuba ya mlimani” iliyotangazwa na Yesu. Hotuba hii kabisa inajumuisha
sura tatu, yaani, ya 5 hadi ya 7. Kwanza kabisa ni muhimu sana kuifahamu nia ya
Mathayo alipoandika toleo lake. Yeye aliandika kwa Wayahudi na kwa hivyo, alimjulisha Yesu kama “Musa Mpya”. Mambo yote ambayo yanamhusu Kristo
yanaileta hali mpya, yaani, Mlima wa “heri nane” unatukumbusha hali ya Mlima wa
Sinai; ujumbe huu wa “Heri nane” ni mafundisho mapya kuhusu Amri za zamani;
upendo wa kindugu ni haki mpya ambayo inashinda haki ya walimu wa Sheria na Mafarisayo,
n.k. Tuko mbele ya hotuba ya kuuanzisha ufalme, yaani mapendekezo ya kupata
furaha ya kweli kwa njia tofauti kabisa na matarajio ya jamii. Huu ni mpango wa
maisha ambao Yesu aliishi kwanza kabla ya kupendekeza kwa wote. Nyuma ya heri
nane tunaweza kukuta nafsi ya Yesu mwenyewe katika uhusiano wake na Mungu aliye
Babaye.
Wakati Yesu alipotangaza
Ufalme wa Mungu kwa mara ya kwanza, aliamua kuhubiri maneno ya faraja kwa wale waliokuwa
na mahitaji na mateso mengi na kumtumainia Mungu, yaani walio kipaumbele katika
Ufalme. Tunahitaji kuchukua andiko hili la leo pamoja na lile la Luka linalosema
kwamba kuwa maskini yatosha kuumiliki ufalme. Yesu alifanyika mwili kuonyesha
ukaribu wa Mungu. Wale waliomkaribia Yesu mlimani walikuwa na moyo uliofunguliwa
kwa ukaribu huu wa Mungu kwa maana walikuwa na tabia zinazompendeza. Watu Hawa
walionyeshwa na nyuso nyingi, yaani, walio maskini wa roho ndio wasio na tamaa
ya makuu bali wanaweza kuyasalimisha maisha yao mikononi mwa Mungu; wenye
huzuni ndio wanaoguswa na uchungu wa wenzao; wenye upole ndio wanaoishi kwa
ushirika na moyo wa Mungu; wenye njaa na kiu ya haki ndio wanaojitolea kwa
kujenga jamii nzuri; wenye rehema ndio wanaoguswa na huruma ya Mungu ili wawe
chombo cha huruma hii; wenye moyo safi ndio wanaoweza kumjua Mungu; wapatanishi
ndio wanaosaidia uzoefu wa kindugu katika jumuiya zetu; wanaoteswa kwa ajili ya
haki na kwa jina la Yesu ndio walio mashahidi wa wema wa Mungu kati yetu. Ufalme
wa mbinguni ni tuzo yao.
Sisi, tulio wafuasi wa
Yesu, tunaalikwa kuchukua ujumbe wa “Heri nane” kama mpango wa maisha.
Hatuhitaji njia nyingine ya kuishi kwa ajili ya kupata furaha ya kweli. Mambo
yote Yesu aliyotaka kusema kwa wanaotaka kumfuata yapo hapa. Mungu anataka tuwe
wenye furaha, lakini njia zake zina masharti yaliyo Heri nane yanayotualika
tuweze kubadilisha njia ya kuona na ya kuishi. Hii ni njia ngumu, lakini hatuko
pekee yetu. Maisha yetu yana thamani kubwa kwa Mungu. Yeye yu pamoja nasi kwa
sababu hawaachi wale wanaomtumainia yeye. Jibu letu kwake ni tuweze kuishi kwa
uaminifu yale aliyoishi na kufundisha Yesu. Huu ni utabiri wa wakati mpya. Ingawa
ufalme upo katika Yesu, yeye mwenyewe anatambua thamani za ufalme huu duniani
na katika hali ya jumuiya zetu. Neema yake ituimarishe tuwe vyombo vya thamani
za ufalme huu.
Fr Ndega
marekebisho: Carlistus Mulama