Kutafakari kuhusu Lk 16, 1-13
Mungu anatarajia kwa watu wake maisha marefu
na kwa heshima. Mambo yote ambayo hayaisaidii hali hii yanakataliwa na Mungu.
Hivyo, kupitia nabii Amos, katika somo la kwanza, yeye (Mungu) anashutumu aina
yote ya ukandamizaji ambao uliwazuia watu waishi kama watu wa Mungu hasa hali
ya udhalimu dhidi ya maskini na wenye njaa. Mateso yao
yadhihirisha kwamba tuko na jamii ya kijeuri ambapo wako baadhi ya watu wenye
nguvu kwa sababu wanamiliki mali na pesa nyingi wakati wengine wengi hawana kilicho
cha kutosha kwa kuishi. Sisi pia kama si makini tunaweza kusaidia ili hali ya
udhalimu wa kijamii uongezeke kwa sababu dhambi ya kijamii ni matokeo ya kiasi
cha dhambi za kibinafsi. Kuhusu hayo Baba Mtakatifu Francisco
asema: “Ulaji umetuongoza kutumia vitu bure pamoja na ubadhirifu wa chakula cha
kila siku... Tunapaswa kukumbuka kwamba chakula ambacho sisi hutupa takatakani
ni kama ikiwa tulikuwa tumeiba kutoka meza ya walio maskini na wenye njaa.”
Hali ya watu hawa ilikuwa kipaumbele katika kazi ya Yesu ambaye alichukua ahadi
ya kuwa maskini ili kuwatajirisha wote kwa umaskini wake.
Katika somo la pili, Mt. Paulo anatushauri
kuwaombea watu wote hasa wale ambao wako na mamlaka ya kuongoza na kutawala,
yaani Viongozi wa Kanisa, Serikali na kadhalika. Hao wanapaswa kufanya kazi yao
vizuri ili tuweze kuishi maisha ya utulivu na amani. Sisi ni wa Mungu na kwa
hivyo, kazi ya viongozi wote kwa ajili ya maisha yetu ni ushiriki katika
utawala wa Mungu mwenyewe ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua
yaliyo kweli. Ni jukumu letu ili watawale vizuri nayo inampendeza Mungu. Tukiendelea
kutafakari kwetu, tuko na mfano ambao Yesu alisimulia kuongea kuhusu mahitaji
ya kuwa mwaminifu katika jukumu ambalo tumepokea kutoka kwa Mungu. Kile kilicho
nacho kinatoka kwa Mungu kwa sababu vyote vyatoka kwake. Anatukabidhi utunzaji
wa vyote na kutarajia tupate kusimamia zawadi zake kulingana na mapenzi yake. Sisi
sio walio na mali bali wasimamizi wa zawadi za Mungu. Hivyo, tunapaswa kuitumia
pesa sio kama lengo la maisha, bali kama chombo cha kuizaa hali nzuri kwa wote.
Tunaishi katika jamii ambapo pesa ni kipimo cha
kila kitu na pia inaonekana kwamba pesa inatutawala. Kila kitu ambacho
tunahitaji hakiwezekani kupata bila pesa. Hii ni nguvu na maana ya kuishi kwa
watu wengi. Je, Wakristo wanapaswa kuwa na tabia gani mbele ya utajiri? Wale
wanaofuata Kristo wanapaswa kuwa waaminifu katika mambo yote na kutumia tabia
kamili kuhusu pesa. Kutokuwa na tabia kamili kuhusu jambo hili kunatuongoza
kusahau uangalifu kwa ajili ya familia, utunzaji kwa afya yenyewe, uhusiano wa
kweli na Mungu na kadhalika. Mara nyingi uhusiano wetu na Mungu unasumbuliwa
kwa sababu ya hamu ya kuwa na pesa na mali nyingi. Yesu hasemi kwamba pesa si
muhimu, lakini asema kwamba haiwezi kutushika na kutumiliki. Yesu anataka tufahamu
kwamba pesa haijengi thamani za kweli ambazo zinazaa uzima na furaha. Tunaweza
kuitumia pesa ili kumtumikia Mungu, bali hatuwezi kumtumia Mungu ili tupate
pesa. Tunapaswa kuwa macho kwa sababu hali hii inaweza kutokea na mara nyingi bila
tuweze kuitambua hiyo. Pesa ni kitu ambacho kinaweza kututumia na kutubadilisha
kuwa wasio na hisia kwa ajili ya Mungu na kwa mahitaji ya wengine.
Pesa inatusaidia
kuishi lakini imewaweka watu mbali sana wao kwa wao. Pesa inaijenga nyumba
lakini inaweza kuharibu familia. Kupitia pesa tunaweza kuinunua nguo, chakula
na kadhalika, lakini pia inaweza kuzaa upendeleo, ubaguzi na utoaji rushwa.
Hatuwezi kuruhusu kwamba pesa iwe chombo cha tofauti kati yetu, kutuongoza kuwabagua
wengine. Kati yetu tunajua jinsi vile pesa imekuwa muhimu, hasa kuhusu sadaka
ya ukarimu kwa ajili ya kulijenga kanisa-hekalu na kwa ajili ya mahitaji mengi
katika kazi zetu za uinjilishaji. Tunamshukuru Mungu kwa matumizi ya pesa kama
maonyesho ya ukarimu kwa manufaa ya jumuiya zetu kwa kulijenga Kanisa la Bwana.
Tena tumwombe neema ya kuwa na tabia kamili mbele ya pesa kutumia ishara hii si
kama chombo cha ubaguzi, bali kama chombo cha undugu.
Padre Josuel Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário