terça-feira, 23 de agosto de 2022

WOKOVU NDIO ZAWADI YA MUNGU NA SIO ASTAHILI YETU

 

Kutafakari kuhusu Lk 13, 22-30




 

    Wakati wa safari ya kwenda Yerusalemu, Yesu alitumia nafasi ya kuwafundisha wanafunzi wake hasa kuhusu masharti ya kuingia katika ufalme wa mbinguni. Kwanza kabisa haitoshi kuwa wanafunzi wake ili kupata wokovu. Hivyo, aliwapendekezea mlango mwembamba kama changamoto. Ikiwa Yesu anajulisha mlango mwembamba ni kwa sababu pia kuna mlango mpana.

     Wakati Mt. Yohane Paulo wa II alipoongea na vijana katika mwaka wa 1993, alitofautisha vizuri njia hizi mbili, akisema: “kataeni barabara rahisi: barabara ya anasa, uhalifu, kudharau mazuri, na kukwepa wajibu. Ulevi na matumizi ya madawa ya kulevya na uasherati visiwe na nafasi katika maisha yenu. Pitieni mlango mwembamba. Chagua barabara ielekeayo kwenye uzima wa milele na furaha pamoja na Mungu.”

    Katika kifungu kingine Yesu alisema kwamba mlango mwembamba ni njia ambayo inaongoza kwenye uzima na wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo. “Huu ni mlango wa uvumilivu, busara, kujitoa, ukarimu, wema, shukrani na kazi”. Kuhusu mlango mpana, hii ni njia rahisi inayoongoza kwenye maangamizi na waendao njia hiyo ni wengi. Basi, ili wanafunzi wa Yesu waweze kupata mafanikio katika safari yao wapaswa kupitia mlango mwembamba.   

    Katika mazingira yetu mlango mwembamba ni ishara ya juhudi yetu ya kushinda mwelekeo mbaya wa maisha yetu na kuwatendea watu mema. Katika mwendo huu ndio sisi wa kwanza wa kupata mafanikio ama bahati mbaya, kwa sababu lile tunalofanya kwa ajili ya wengine linasababisha hali nzuri ama mbaya kwetu pia. Hadithi fulani inatusaidia kuelewa vizuri hali hii.

    “Siku moja mwandishi wa habari alimhoji mwenye shamba ambaye ameshinda mara ya tano mashindano kuhusu mahindi mazuri zaidi katika eneo hilo. Mwandishi alimwuliza swali akisema, “unapataje kuzaa mahindi bora kuliko wengine?” Mwenye shamba alijibu, mwendo huu ni rahisi sana; nina mazoea ya kushiriki mbegu zangu nzuri na majirani wangu.” Mwandishi aliendelea kwa swali akisema, “Kwa nini unashiriki mbegu zako nzuri na majirani wako ikiwa hao wanashindana pia katika mashindano haya pamoja?” “kwa sababu ni upepo ambao unasambaza poleni ya mahindi na tena ni upepo ambao unaweka poleni mashambani na unafanya mbegu zikue. Ikiwa majirani wangu watakuwa na mahindi mabaya, upepo utasambaza poleni mbaya shambani kwangu nayo mahindi yangu yatakua mbaya. Basi ili mahindi yangu yawe mazuri ninapaswa kuwasaidia majirani wangu wote ili wawe na mbegu nzuri.”

    Basi, lile zuri ambalo tunatarajia kwa maisha yetu tunapaswa kusaidia kwa ajili ya wengine. Katika mwendo huu hatuwezi kuitafuta furaha kwa njia ya ubinafsi. Ikiwa tunataka kuwa wenye furaha, tunapaswa kuisaidia hali hii nzuri kwa wale wanaoishi karibu nasi nao wako na shida sawasawa nasi. Tunapaswa kushinda mwelekeo wa jamii wa kufikiria wengine kama washindani nasi. Wengine sio washindani, bali ni ndugu.

    Kujaribu kupata upendeleo tukiwavuruga wengine ni udhalimu na kutuacha mbali sana na pendekezo la Yesu. Ikiwa tuko mbali na pendekezo la Yesu, matokeo yatakuwa mbali sana na yale tuliyotarajia kwa maisha yetu. Tunaweza kuongea vizuri sana kuhusu Yesu ili kuonyesha kwamba tunamjua Yeye na Biblia pia. Tunaweza hata kufikiri kwamba kuongea bora kuliko wengine kunatuhakikishia faida ili tupokee baadhi ya tuzo kutoka kwa Mungu. Lakini, kulingana na andiko hili, maneno hayatoshi kuingia katika ufalme wa Mungu. Wokovu si astahili yetu, lakini hii ni zawadi ya ukarimu wa Mungu.

    Inawezekanaje tuseme kwamba tunamjua Yesu naye aseme kwamba hatujui sisi?” Hii ni kwa sababu katika biblia kitenzi kujua kinamaanisha uhusiano wa ndani, uzoefu wa kina ambao ni muhimu sana katika safari yetu ya wanafunzi wa Yesu. Ikiwa yeye anasema kwamba hatujui sisi ni kwa sababu sisi hatumjui yeye. Katika mwendo huu hakuna makubaliano kati yetu na pendekezo lake, hakuna utambulisho. Hatuwezi kuwa wanafunzi wa Yeu kupitia maneno peke yake. Ushuhuda wa maisha unathamini zaidi kuliko maneno.

    Tukijifikiria bora kuliko wengine hatuuhakikishii wokovu. Kila kitu tunachofanya kinasababisha matokeo makubwa kwetu na katika hali iliyo kandokando yetu. Kwa maneno mengine, kufikia mafanikio ama bahati mbaya kwa maisha yetu kunatutegemea sisi wenyewe; huu ni uamuzi wetu. Kwa upande wa Mungu tunaumbwa ili kushiriki katika maisha yake, yaani ili kuokolewa. Neema ya Mungu ituongoze ili tuweze kufanya mapenzi yake na kupata uhai.


Fr Ndega

Nenhum comentário: