Tafakari kutoka Mwanzo 18: 1-10a; Kol 1: 24-28; Lk 10: 38-42
Muhimu ya liturujia hii ni ukarimu
kama uwezo wa kuwakaribisha watu vizuri. Ukarimu unawafanya watu kuwa wanadamu wa
kweli na, kwa hivyo, waliofaa kwa kushirikiana katika kazi ambayo Bwana anataka
kutimiza ulimwenguni.
Somo la kwanza linasimulia kuhusu
ziara ya Mungu aliyeonekan kupitia wageni wa tatu kwa Ibrahimu na Sara ambao,
kwa njia yao ya kuwakaribisha, walitafuta kufanya kila liwezekanalo ili wageni
hawa watukufu wajihisi wako nyumbani. Kwa shukrani kwa kujitolea huko, Mungu aliwapa
wazee hawa wasio na watoto zawadi inayongojewa sana maishani mwao: kuzaliwa kwa
mwana, mtoto Isako. Mungu anapenda kukaribishwa na kuleta maisha mapya katika
maisha yetu. Na sisi pia tuwe tayari kwa ziara zake, kwa mipango yake.
Katika somo la pili, mateso ambayo
Paulo anayapata katika kutangaza injili kwa mataifa yanamletea furaha kubwa pia
kwa sababu anajiona kuunganishwa na Kristo ambaye aliteseka na kujitoa mwenyewe
ili wokovu wa Mungu uwafikie watu wote, hakuna aliyetengwa. Paulo anajiona kuwa
mtumishi wa mpango huu, na kwa hili anatumia nguvu zake zote, akiteseka kwa
ajili ya Kanisa. Mateso kwa ajili ya Kanisa ni
mateso kwa ajili ya Kristo. Yeyote aliyemchagua Kristo hajifikirii nafsi yake mwenyewe
kwa maana kwake yule aliye hai ni Kristo.
Katika
kifungu cha Injili, Yesu aliyechoka kwa maana ya safari, alikubali kwa hiari
kukaribishwa nyumbani kwa marafiki zake kwa wakati wa kupumzika. Wakati huo
ndani ya nyumba kuna dada wawili tu. Ndugu Lazaro hakika yuko kazini nje. Dada
hao wawili walijaribu kutoa ukarimu unaostahili kwa mgeni huyo mtukufu, lakini
kila mmoja kwa njia yake mwenyewe. Marta alishughulikia mazingira, Maria alitunza
nafsi ya mwalimu; Martha kwa huduma, Mariamu kwa kusikiliza. Yanaonekana kuwa mambo tofauti na yanayopingana,
lakini Yesu anatufundisha kutafsiri kwa njia tofauti:
Tangu
alipofika, Yesu aliona kwamba Martha alifadhaika alipokuwa akitumikia, akienda
kutoka upande mmoja hadi mwingine bila lengo, bila rejeo, bila kuacha. Kweli
kulikuwa na haja ya kumhudumia mgeni tu, na si kuwa na wasiwasi kwa ajili ya
uwepo wake. Mariamu alifanya uamuzi tofauti, yaani alijiweka kama mfuasi
miguuni pa bwana-mkubwa, kama yule asiye na la kufanya, akifikiria umuhimu
zaidi yale ambayo Yeye alitaka kumfanyia kuliko yale ambayo angeweza kumfanyia
Yesu. Tofauti ni kubwa sana lakini hili si tatizo: Yesu haoni huduma kama
kinyume na kusikiliza.
Hata
ikiwa Yesu aliiona tabia ya Martha, labda hangalisema lolote ikiwa hangaliulizwa.
“Ghafla Martha, akiwa amekasirishwa kwa sababu Mariamu hakumsaidia kufanya kazi
za nyumbani, alimwuliza Yesu, kwa njia fulani ya mwenye kujisifu”, akimpa amri
ya kumsahihisha dada yake; hapo tunaona hali yake kubwa ya kuchanganyikiwa. Ikiwa
dada yake angalimsaidia katika njia yake ya kufanya, labda isingekuwa yeye tu
katika fadhaa bali wote wawili. Kwa kifupi,
ni jambo moja kuwa mwenyeji na jambo lingine kuwakaribisha. Martha alikuwa
mwenyeji kwa Yesu lakini Mariamu ndiye aliyemkaribisha.
Yesu
alimkemea Martha kwa upole sana kwa sababu alitambua pia ukarimu na kujitolea kwake,
lakini alimwambia kwa wazi kwamba hahitaji fadhaa yake. Kwa hili, ni lazima
tukatae tafsiri inayosema kwamba Yesu hakuona huduma madhubuti kuwa ni muhimu.
Kwa kukemea kwake, alitoa ushauri kwa Martha na kwa sisi sote kuhusu “umuhimu
wa kimsingi wa kulisikiliza neno lake”. Mambo mengine ni muhimu lakini yanaweza
kusubiri. Ni neno ambalo lazima liongoze
nafsi yetu na matendo yetu. Kwa hivyo, kusikiliza kwake kwa kipaumbele hakupaswi
kupuuzwa. Kwa maana hii, Mariamu wa Bethania ndiye mfano wetu.
Kweli Yesu anatafuta marafiki na si watumishi: “Siwaiti ninyi watumishi... Nimewaita rafiki kwa sababu nimewajulisha yote ambayo Baba aliniambia”. Sisi si watumishi bali ni marafiki wa bwana arusi, tulioitwa kutumikia. Utumishi wetu utakuwa maonyesho ya mapenzi yake ikiwa sisi ni marafiki zake. Sio wingi wa mambo tunayofanya ambayo ni muhimu, lakini ubora wa mahusiano yetu. Tunafikiri ya kufanya mengi kwa ajili ya Bwana, lakini anataka tu bora tuwezavyo. Ikiwa uchaguzi wetu haupatani na matarajio yake, tunachofanya kwa jina lake huwa bure.
Ili kuepuka kutumia
maisha yetu kwa ajili ya Kristo bila kufanya utume wetu kuwa bure, ni lazima
tujifunze "kujiweka kwa tabia ya unyenyekevu na tulivu kwa ajili ya kusikiliza
maneno yake ili kujaribu kujua na kutimiza mapenzi yake". Utumishi na hali
ya kiroho ni mambo mawili ya kweli ambayo yanapaswa kupata ushirikiano wao na
kila moja kukuta nafasi sahihi katika maisha yetu ili Bwana, akitugeukia,
atambue kile alichotambua katika Mariamu, yaani, sehemu bora, chaguo bora
zaidi, kwa sababu ilifanywa kwa hekima n asio kwa fadhaa.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário