Kutafakari kuhusu Lk 10, 25-37
Katika injili ya siku ya leo mwanasheria alimwendea Yesu na alimwuliza
maswali mawili, yaani la kwanza “nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”;
na la pili, “Jirani yangu ni nani?” kuhusu swali la kwanza Yesu alimsaidia
kugundua tena umuhimu wa sheria, yaani “kumpenda Mungu na kumpenda jirani”.
Amri ya Kumpenda Mungu tunapata katika kitabu cha Kumbukumbu la Sheria (6:5) na
ya Kumpenda jirani inapatikana katika kitabu cha Walawi (19:18). Ikiwa Yesu
alimwambia mwanasheria kwamba yatosha kutenda hivyo ili apate uzima wa milele
ni kwa sababu “Torati yaonyesha njia ya uzima wa milele ikiwa mtu anampenda
Mungu na jirani yake.”
Katika Agano la Kale Mungu alianzisha Agano na Watu wa Israeli akiwafanya
wana wake. Kama ishara halisi ya Agano hili tuko na Amri kumi ambazo zinalenga
ushusiano mwema na Mungu na jirani. Lakini, kulingana na mawazo yao ya
kiyahudi, jirani siyo yule ambaye anaishi karibu nao bali ndiye yule aliye na
uhusiano wa damu nao. Basi, wageni hawawezi kuwa jirani kwao. Hivi mawazo haya yawazuia
kuwa na uhusiano mwema hasa na Wasamaria waliofahamiwa kama maadui wao kwa
sababu waliichangamana damu yao na ya wageni.
Kupitia swali la pili, yaani “Jirani yangu ni nani?” mwanasheria alitarajia
Yesu akubaliane na mawazo haya ya kivuo. Lakini Yesu alisimulia mfano wa
Msamaria Mwema. Kulingana na mfano huu mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu
kwenda Yeriko na kushambuliwa na wanyang’anyi ambao walimwacha karibu na kufa. Wote
wawili, yaani kuhani na Mlawi walipomwona mtu walipita kando lakini Msamaria
alipomwona mtu alimwonea huruma na kumsaidia. Wawili wa kwanza ni ishara ya wale ambao wanapaswa kuitii
sheria, na kulingana na sheria hii, hawawezi kugusa ama kuguswa na “kitu
kichafu”. Walitumia njia nyingine kwa sababu kuwa karibu na mtu yule aliye na
haja ya msaada kungewazuia kumsifu na kumtumikia Mungu kamili. Walisahau kwamba
“ni jambo baya kutofanya mazuri kwa kutumia jina la Mungu au la dini”.
Kwa sababu ya sheria ya utakaso wawili wa kwanza walidharau yule aliye
mwenzao kushindwa kuonyesha ujirani. Kupitia tabia yake ya huruma, “Msamaria
alionyesha ujirani mwema” kwa sababu hakuhitaji kuitii sheria ya utakaso.
“Msamaria mwema hakujifikiria mwenyewe, alimfikiria mwingine.” Kupitia mfano
huu Yesu anaonyesha kuwa swali la msingi sio “ni nani jirani yangu?,” bali
ninawezaje kuwa jirani kwa mwenzangu?” Yesu anasahihisha mtazamo kuhusu jirani
na kuonyesha kuwa upendo wa kweli kwa Mungu unatokea pamoja na kushiriki katika
maisha ya wale anaowapenda hasa walio na shida.
Kwa Yesu, upendo wa kweli unaonyeshwa kupitia ishara za upole na huruma. Yesu mwenyewe ni Msamaria
Mwema kwa namna ya kipekee ambaye alichukua hali yetu na kuponya majeraha yetu
ya dhambi. Tena anajitambulisha na
wale ambao “wameanguka kando ya njia za maisha”. Je, tunaweza
kutambua uwepo wake Kristo katika watu ambao kwa kawaida tunakutana na hao ambao wanauomba msaada wetu? Kumwabudu Mungu kwa kweli
kunatokea kupitia uhusiano mwema na ufanisi na wengine. Kusherehekea Ekaristi
ni alama ya undugu ikiwa undugu uko miongoni mwetu, vinginevyo, sio Mwili na Damu
ya Kristo tunayosherehekea. Haiwezekani kufanya uhusiano wa kweli na Mungu
wakati tunapowasahau wenzetu katika mahitaji yao.
Hatuwezi
kuishi kwa kutojali kuhusu hali ya wengine kama ilivyotokea kwa Kaini, yaani “Je mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mw 4:9). Hali hii ni kutojali iliyo njia ya kukanusha utambulisho wetu wa Wakristo.
Sihitaji kujua ni nani jirani yangu ili nimpende na kumsaidia. Nimekuwa
mwanafunzi wa Kristo ili kuwa jirani wa wote ka ma Kristo alivyo. Kumpenda
jirani ni kumsaidia kushinda hali mbaya ya maisha yake. Kwa upande wetu tulio Wakristo,
jirani ni yule tunayomgundua kama aliye na haja nasi twamua kuwa jirani kwake
kwa kuandamana naye kumhakikishia maisha ya heshima hata ikiwa mwendo huu unapodai
tutumie muda wetu na rasilimali zetu. Neema ya Bwana itusaidie kutenda kama “msamaria
mwema”.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário