Tafakari kuhusu Is 66: 10-14; Gal 6: 14-18; Lk 10: 1-12
Akitumia
lugha ya mama, Isaya anatoa mwaliko wa furaha kwa sababu ya kile ambacho Bwana
anakaribia kutimiza katika maisha ya watu wake. Uwepo wa kudumu wa Mungu
katikati ya watu wake hushinda nyakati za usumbufu na kukatishwa tamaa kwa
kufungua nafasi za matumaini na furaha hata kama kila kitu kinaonekana kupotea.
Kama watu hawa, sisi pia tunaombwa kuwa na imani isiyochoka katika utendaji wa
Bwana kwa sababu Yule anayeahidi ni mwaminifu daima.
Somo la
pili linatoa mabishano makubwa: baadhi ya Wakristo wa Kiyahudi, ambao bado
waliendelea kushikamana na mila zao za Kiyahudi, walitaka kuwalazimisha
wapagani kutahiriwa kama wao. Kwa sababu hii Paulo anasema kwamba tukihukumu
hivyo tunaufanya msalaba wa Kristo kuwa bure. Kwa njia ya msalaba Kristo
alishinda kifo nao ulimwengu wa kale pia ulisulubiwa! Sisi ni viumbe wapya. Ni
jukumu letu kuishi kama wamefufuka, tukiacha tabia za zamani, mawazo ya zamani,
kila kitu ambacho kinapingana na hali yetu mpya.
Kifungu
cha Injili kinatujulisha kwamba Yesu pamoja na mitume kumi na miwili tena aliita
na kuwatuma watu wengine 72 ili kuinjilisha. Nambari hii, katika Agano la Kale
ilikuwa ishara ya jumla ya mataifa na kumaanisha utume wa ulimwenguni kote,
yaani, kuinjilisha sio tu kazi ya mapadre na watawa bali inahusisha kila mtu
anayebatizwa. Yesu anawatuma wawili-wawili, akiweka uzoefu na uhusiano wa
jumuiya kama rejeo la shughuli zao. Utume ni ahadi ambayo mtu achukua sio peke
yake. Tunahitaji msaada wa jumuyia kwa mafanikio ya kazi yetu ya kuinjilisha.
Wanafunzi
wanapaswa wawe watu wa sala kama tukio la msingi, yaani, kama msingi
unaodumisha jengo la kuwepo kwao. Ni lazima wafahamu kwamba mavuno yana bwana
wake, yaani Baba mwema na mkarimu, ambaye anajua mahitaji ya watoto wake kabla
ya amwombe chochote. Akitumia neno mavuno, Yesu anataja umuhimu wa kuthamini
kila mahali tunapofika kwa sababu Roho Mtakatifu ametutangulia kwa mbegu za
Neno la milele. Kwa hiyo, mtu hatoki nje ya bustani yake kuelekea jangwani mwa
wengine, bali aenda kutoka bustani moja hadi nyingine.
Mungu
hahitaji maombi yetu; ni sisi tunaohitaji kuomba kwa sababu tunapoomba tunakua
katika ufahamu wa kuwa watoto na wanafunzi wanaopendwa sana; tunakuwa vile
tulivyo kwa wito. Wanafunzi ni kama wana-kondoo katikati ya mbwa-mwitu, kwa
sababu wameitwa kumwilisha utambulisho wa Mwana-Kondoo wa kweli, Yeye anayeondoa
dhambi za ulimwengu kwa sababu anaweza kutoa maisha yake kwa ajili ya rafiki
zake. Ni katika utambulisho huu - wa upendo, wa kujitolea - kwamba maisha yao
yanapata maana yake ya kweli. Kuinjilisha ni kujitolea.
Miongoni
mwa mahangaiko ya Yesu pia kuna tatizo la miliki ambayo tunaitegemea sana kwa
ajili ya kufanya baadhi ya shughuli. Yesu anatuomba busara, unyenyekevu,
kujitenga na usalama hio wa uwongo ambao mara nyingi zinaelekea kuchukua nafasi
ya Mungu maishani mwetu. Amini kwa Riziki takatifu ya Mungu ni tabia ya msingi
ya mmisionari wa kweli na inakuwa tangazo la kinabii la upendo na utunzaji wa
Mungu kwa watoto wake. Kuishi katika wingi wa mali kunahatarisha uaminifu wa
ujumbe tunaotangaza kwa kuwa kikwazo kwa imani ya wengine.
Wanafunzi wanarudi wakiwa wamejawa na furaha
kwa sababu walipata mafanikio katika utume, hasa kuelekea pepo waliojisalimisha
kwao kwa sababu ya jina la Yesu. Lakini bwana aliwaomba wawe macho kwa aina hii
ya furaha inayoweza kutudanganya. Furaha ya kweli haitokani na mafanikio kwa
kazi iliyofanywa au kuwa maarufu katika ulimwengu huu. Utukufu wa dunia hii hudumu
sana. Furaha ya kweli ni kukaribishwa na Baba kama watoto wapendwa na kushiriki
katika utume wa Mwana, kwa kupokea uhai wake mwenyewe. Tuweze kupata kufanana
na maisha ya Yule ambaye tumeitwa kumtangaza kwa maisha kabla kwa maneno.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário