Kutafakari kuhusu Bar 5,
1-9; Wafil 1: 3-6, 8-11; Lk 3, 1-6
Liturujia ya
jumapili hii inaendelea kutumwalika kumkaribisha Bwana anayekuja kutuletea
wokovu. Tunapaswa kujiandaa vizuri ili tuweze kumpokee Masiya wakati wowote. Wakati
wa Majilio unatusaidia kutambua kwamba kwa matayarisho kamili ni lazima mabadiliko
ya moyo, kwa njia mpya kabisa. Maneno ya
nabii Baruku yaliimarisha watu utumwani Babeli yakitangaza ukombozi karibu.
Baada ya mateso hayo yote wataweza kurudi nyumbani Yerusalemu kwa furaha kubwa
kwa sababu Mungu aliwakumbuka na kuwaongoza katika mwangaza na utukufu wake.
Huu ni mfano wa wokovu wetu katika Kristo. Paulo anatambua kwamba imani na
ushirika wa Wafilipi ni uenezi wa injili waliyochukua kwa shauku na utayari.
Kwa njia ya Kristo na injili yake wanaweza kuzaa mazao mazuri kwa utukufu na
sifa ya Mungu.
Injili inaongelea
Yohane Mbatizaji anayefikiwa na Neno la Mungu jangwani. Katika biblia jangwa ni
mahali maalum pa uzoefu wa Neno la Mungu. Katika mahali huko watu wengi walijibadilisha
kuwa viongozi wenye nguvu kwa kuwaongoza Watu wa Mungu kulingana na mwongozo
wake. Yohane Mbatizaji anafikiriwa kuwa nabii wa mwisho na mkuu wa manabii
wote. Toleo la Luka linataja makuhani na viongozi wa kisiasa ili kuonyesha
kwamba kupitia mjumbe wake, Mungu huingia katika maisha halisi ya watu kwa
wakati fulani. Mungu haongei moja kwa moja bali kwa kupitia matukio mazuri au
mabaya ya historia ya watu. Mungu alijifanya
mmoja wetu na bado yuko nasi kwa namna mbali mbali. Kwa kiyo hakuna tukio
lolote la historia lisilokuwa na maana. Kwa kuonyesha wito wa Yohane katika
matukio ya wakati wake, Luka anaonyesha kwamba tukio kubwa liko karibu. Mungu
anaingia katika historia kwa namna ya pekee na kuomba watu watayarishwe
kumkaribisha Masiya aliyetarajiwa kwa muda mrefu.
Kuja kwake Yohane Mbatizaji kuna maana na kuufuata mpango wa Mungu ambaye
ana wakati kamili kwa kila kitu. Neno lake linayabadilisha maisha ya Yohane
katika chombo cha wokovu. Kama Yohane ni kiungo kati ya Agano la kale na Jipya,
kazi yake inatangaza kwamba nyakati za Masiya ziko karibu kuanza. Yeye ni sauti
tu ambayo inatayarisha njia za Bwana. Yohane aliwatayarisha watu kumpokea
Masiya kwa ubatizo. Kupitia ishara hii alitangaza huruma ya Mungu iliyopatikana
kwa kila mtu kwa sababu ni mpango wa Mungu kwamba wokovu wake ufikie wote. Basi
ishara ya Yohane ilikuwa kipimo cha kupita kutoka katika dhambi na mauti kwenda
katika neema na maisha mapya ya Mungu. Kipengele muhimu katika tendo hili la
Yohana ni kwamba aliwabatiza wale waliomhitaji Mungu na kutubu dhambi zao.
Yohane na watu hao waliamini kwamba ndiye Mungu anayesamehe dhambi zao.
Ubatizo wa Yohane ni tofauti na ubatizo wetu, lakini yote mbili ni nafasi ya
kuishi maisha mapya. Kwa upande wetu maisha mapya ni zawadi ya Kristo na
matokeo ya utume wake. Ubatizo wa Kikristo, pamoja na maondoleo ya dhambi,
unadhamini ushiriki katika uzima wa Mungu mwenyewe. Ubatizo ni wa kwanza kati ya
sakramenti tatu za mwanzo ukifuatiwa na Kipaimara na Ekaristi. Ubatizo wetu ni
ishara ya nje ya kufa kwa maisha ya dhambi, na tena ndiyo ishara ya ufufuko wa
maisha mapya katika Kristo aliye mshindi dhidi ya dhambi na mauti. Yeye ni mwanga
wa kweli ambao unamtia nuru kila mtu. Kupitia mwendo huu tumekuwa wana wa nuru
ili tutembee katika nuru ya Mungu kila siku ya maisha yetu.
Kipindi cha Majilio kinatusaidia kujiandaa kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu.
Wakati ulimwengu wa biashara unashauri watu wajiandae kwa Noeli kwa kununua
vitu, kipindi cha Majilio kinatupendekezea matayarisho ya kiroho na hamu ya
kuishi kupatanishwa na Mungu na wenzetu. Kuna vikwazo vya kuondoa katika maisha
yetu kwa msaada wa neema ya msamaha wa Mungu. Kwa hivyo tuchukue wakati mzuri
huu kuadhimisha msamaha wa Mungu kwa sacramenti ya Upatanisho (na kitubio) na
kuishi kwa njia mpya uhusiano wetu na Mungu na wengine.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário