Kutafakari kuhusu Lk 21, 25-28, 34-36
Tumeanza
wakati mpya katika liturujia ya kanisa uitwao Majilio. Wakati huu unayaimarisha
matumaini yetu katika matarajio ya
Kuja kwake Bwana mara ya pili katika mwisho
wa nyakati na kukumbuka pia Kuja kwake kwa kwanza kwa kutuandaa ili tusherehekee
sikukuu ya kuzaliwa kwake katika Krismasi. Basi, Liturujia ya msimu huu ni mwaliko kwa kukesha ili tutambue na
kuzikaribisha ishara za uwepo wa
Bwana katika hali yetu ya kila siku. Ni mwaliko pia kwa shukrani kwa sababu
Bwana anakuja daima kukutana na sisi, kutupa wokovu wake. Matukio yote makuu yanahitaji maandalizi mazuri ili yaweze kusherehekewa
vizuri. Hivyo ndiyo Majilio kulihusu tukio
kubwa la Krismasi.
Mwanzoni mwa sura
ya kumi na tatu ya injili ya Luka Yesu anaongea kuhusu uharibifu wa Yerusalemu.
Ufunuo huu uliwaimarisha baadhi ya wanafunzi wake wamwulize swali kuhusu ishara
gani, siku na saa gani ya uharibifu huu. Yesu anatumia nafasi hii kutabiri
kuhusu mambo mengi akiiandaa mioyo ya wafuasi wake kwa wakati ujao. Aliwaambia
kuhusu ishara nyingi mbinguni, taabu, mateso, dhiki kuu na kuja kwake,
kulingana na unabii wa Danieli, yaani, juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na
utukufu mwingi. Kanisa katoliki hutafsiri tukio hili kama kuja kwake Yesu mara
ya Pili ili kuwahukumu wazima na wafu. Hiyo ndiyo imani yetu ambayo sisi
hutangaza kila jumapili. Kuhusu siku na saa hii hakuna mtu ajuaye. Hii ni sehemu ya mpango wa hekima na wema wa Baba. Kwa hivyo huu ni pia
mwaliko kwa kukesha.
Yesu anatabiri kuhusu
hali ngumu na matokeo ya hiyo katika maisha ya wafuasi wake. Wanafunzi wa Yesu
wataishi kipindi cha machafuko na watajaribiwa kuiacha imani katika Kristo na
kukata tamaa kuhusu utambulisho wao wa wanafunzi kwa sababu ya matusi,
majaribio, matatizo na mateso mengi. Ilionekana kwamba walikuwa peke yao mbele
ya machafuko hayo yote. Lakini Yesu mwenyewe alikuwa amewaahidi uwepo wake daima
kupitia maneno haya, “mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamiliifu wa
dahari.” Maneno haya ni mwaliko kwa ushuhuda kama njia ya kukesha. Hao wana
jukumu la kuendelea utume wa Mwalimu, wakiwa makini kwa ishara za kuja kwake ili
akutane nao na kuwatuza kwa maana ya uaminifu wao.
Andiko hili linatuambia kwamba Kristo ni mshindi na ujio wake unaanzisha wakati
mpya anaoshiriki na wanafunzi wote wanaobaki wamesimama na kuinua vichwa vyao
kupitia imani na ushuhuda kwa uaminifu. Tunapaswa kuishi imani yetu ya kikristo
kwa uhusiano na kila kitu ambacho kinatokea kandokando yetu. Jamii inatarajia
imani yenye maana na kuhitaji jibu kwa hali ngumu binadamu anayoiishi. Je, Wakristo
wanapaswa kuwa na tabia gani wakati wa mazingira magumu? Kama alivyowaambia
wafuasi wake wa zamani, Yesu anatuhakikishia kuwa mazingira magumu ni sehemu ya
safari ya wale ambao wanamfuata katika nyakati zote, lakini Yeye anatukumbusha
pia kwamba ni katika machafuko haya ya dunia hii tunapojiandaa kukutana naye
mwishoni mwa maisha yetu binafsi hapa duniani. Kwa hivyo kila hatua ya safari
yetu ni maandalizi kwa mkutano wa mwisho na Bwana wetu.
Liturjia linataka
kuimarisha imani yetu na kufufua tumaini letu kwa tendo la wokovu wa Mungu
ndiye mkuu katika nyakati zote, zilizopita na zijazo. Hali hii inatualika
kuishi wito wetu wa wafuasi kwa uaminifu katika nyakati zote pia, hata wakati
wa dhiki. Baada ya machafuko yote tutakuwa washindi pamoja na Bwana wetu
mshindi. Kulingana na mithali fulani, “hakuna usiku hata wa muda mrefu pasipo
mapambazuko”. Basi, kwa wale wanaomfuata Kristo, mazingira magumu si ishara za
mwisho wa nyakati bali ni wakati mpya, wakati wa kuishi wito wetu kwa shauku
zaidi, furaha na tumaini, kuushuhudia kwa uaminifu uwepo wa Bwana miongoni
mwetu. Anakuja kwa upendo na kutuokoa. Tukaribishe ishara za nyakati kama
msaada tutambue uwepo wa Bwana na kuishi mafundisho yake kwa njia mpya.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário