Kutafakari kutoka Hek 1,13-15;2,23-24; Mk 5, 21-43
Mauti yako duniani
lakini hayatoki kwa Mungu kwa sababu yeye ndiye uzima na kutuumba kwa uzima. Mungu
hataki mauti ya watoto wake lakini hazuii watende dhidi ya mapenzi yake kwa
sababu anaheshimu uhuru wao wa uamuzi. Huu ndio ujumbe wa kifungu cha Kitabu cha
Hekima. Andiko hili linachukua tena tukio la uumbaji na kuonyesha nia ya Mungu
alipoumba viumbe vyote. Ingawa ndiye binadamu anayefanyika kwa mfano na kwa
sura ya Mungu, viumbe vingine pia vinaonyesha uzuri wa nafsi ya Mungu na kuongelea
yeye. Hivyo, binadamu anaitwa kuishi kwa maelewano na viumbe vyote kwa sababu yeye
na vingine vina asili sawa. Mambo yote binadamu anayepanga kufanya kwa ajili ya
viumbe vingine yanaleta matokeo kwa maisha yake mwenyewe.
Baada ya
kufukuza pepo wachafu kutoka mtu fulani, Yesu aliendelea anahubiri habari njema
na kutenda mambo mema mengi. Watu wakastaajabu. Kweli Yesu alikuwa mtu maarufu
na mahali popote ambapo alifika mara makutano makuu yalikusanika yakimsongasonga
ili kusikiliza neno la Mungu. Kulingana na andiko la leo Yesu alivuka ziwa la
Galilaya na kubaki kando ya bahari. Tena umati wa watu ulikusanika kumsikiliza.
Kwa upande wa Yesu, yeye alipatikana kwa ajili ya kujifunza watu na kuwasaidia
katika mahitaji yao. Kwa upande wa watu, imani ndiyo kipengele msingi.
Alipozungumza,
mtu mmoja aliye mkuu wa sinagoga aliyeitwa Yairo alimwendea kumwomba aponye
binti yake aliyekuwa mgonjwa na mara Yesu alienda pamoja naye na wanafunzi
watatu. Lakini wakati wa safari mtoto alikufa. Yesu alimwambia Yairo: “uwe na
imani tu!” kweli, kwa sababu ya imani ya Yairo na mke wake mtoto alifufuliwa. Kabla
ya Yesu kwenda kwenye nyumba ya Yairo, mkutano mkuu waliomfuata wakisongasonga.
Miongoni mwao alikuwako mwanamke fulani aliyekuwa mgonjwa wa kutoka damu. Yeye
alimgusa Yesu kwa imani kubwa na mara akapata kuponywa. Yesu alimwambia:
“binti, imani yako imekuokoa”.
Katika
matukio hayo mawili ndiyo imani kipengele cha msingi ili Yesu atende muujiza. “Imani
ndiyo msingi, kama Marko asemavyo kwamba, Yesu hakuweza kufanya miujiza
Nazareti kwa sababu watu walikosa imani (Mk 6, 1-6).” Miujiza siyo uchawi ili
mtu aseme: “utuonyeshe kitu nasi tutasadiki!”, bali ni mwaliko wa kutusaidia
kuzikuza imani yetu. Katika miujiza mingi ya Yesu, imani ndicho kipengele cha
msingi. “Hata iwapo siyo imani kutoka kwa mgonjwa mwenyewe moja kwa moja, kwa
mfano binti Yairo, imani ya jumuiya ni muhimu (Mk 2,5).” Tukumbuke tena wakati
Yesu alipokuwa ndani ya nyumba fulani iliyojaa watu. Kikundi kimoja cha watu
ambacho kilimbeba mtu mgonjwa, kilifanya shimo katika dari ya nyumba na kupata
kumuweka mtu mgonjwa mbele ya Yesu. Kwa sababu ya imani yao, Yesu alimponya mtu
mgonjwa.
Ndilo jambo
la ajabu inayoonekana katika matukio mawili, yaani mwanamke fulani alikuwa
mgonjwa kwa miaka kumi na miwili na mtoto alikuwa na umri wa miaka kumi na
miwili. Nambari hii yaani kumi na miwili ndiyo ishara muhimu katika biblia na
kumaanisha Watu wa Israeli na ubinadamu mzima. Wote yaani mwanamke na mtoto
wanahitaji uzima kwa sababu ya ugonjwa. Ndiye Yesu peke yake anayeweza
kuwapatia uzima kwa kuwa yeye mwenyewe ndiye uzima wa milele. “Mwanamke mgonjwa
wa kutokwa damu, alikuwa na imani iliyosukuma amguse Yesu na hivyo akaweza
kuponywa.” Kulingana na Agano la Kale,
kugusa mavazi ni kugusa mtu mwenyewe. Tukumbuke kwamba ilitosha kupata mavazi
ya Elijah ili Elisha apokee roho yake. “Tendo la kugusa ni ishara ya upendo,
kama vile mtu anapomgusa mgonjwa, ni ishara kwamba anampenda na kumjali katika
hali yake yote.” Ingawa hali ya mwanamke ilikuwa uchafu na yeyote aliyekutana
naye alikuwa mchafu, Yesu aliruhusu kuguswa naye na kubadilisha hali
iliyotarajiwa na wote, yaani badala ya kuwa mchafu yeye alisababisha usafi
mwilini mwa mwanamke.
“Usiogope; amini tu...” yalikuwa maneno ya
Yesu kwa Yairo alimpoteza mtoto wake. Maneno ya Yesu ni maonyesho ya upendo na
huruma yake kwa ajili ya walioteseka. Tumejifunza na kuhisi kwamba “moyo wa
Yesu ni chemchemi ya huruma” na Maandiko yenyewe yashuhudia kwamba “Kwa upande
wake tumepokea neema juu ya neema”. Habari hii inaiimarisha imani yetu na
kulifufua tumaini letu. Nasi kama Yairo na watu wengine twapewa changamoto ya
kuamini kuwa Yesu anaweza kurudisha
uzima. Kilichotokea katika maisha ya Yesu kilikuwa kimelenga katika
kuwaelimisha wale wenye imani kuwa wao pia watapata uzima kwa sababu, kulingana na mapenzi ya Mungu maisha yetu yanafaa kupata
ukamilifu kwa kufufuka kama Mwanawe. Uzima kwa mwenye imani wawezekana
kutokana na ufufuko wa Kristo. Tujaribu kumwamini Kristo na matendo yetu yawe
tangazo la uzima uliomo ndani yetu ambao yeye mwenyewe anatuhakikishia.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário