Kutafakari kuhusu Ezekieli 17: 22-24; 2Wakorinto 5: 6-10; Marko
4: 26-34
Kiini ya liturjia
hii ni uwepo wa kimya na ufanisi wa ufalme wa Mungu miongoni mwetu. Mungu
anafanya mambo yote kwa wema wetu na kutarajia tumwamini yeye kuliko nguvu zetu.
Somo la kwanza
linaongea kuhusu hali ya utumwa wa Babeli katika mwaka wa 597 K.K. na kumjulisha
Ezekieli kama mmoja wa manabii aliyeandamana na watu wa Israeli katika kipindi
hiki kigumu. Watu waliishi hali ya kuchanganyikiwa katika maisha yao bila
matarajio ya mabadiliko. Lakini pamoja mwao alikuwako Ezekieli aliyewaimarisha
kama mjumbe wa Mungu. Kulingana na nabii huyo, Mungu hakuwasahau; yeye yupo
miongoni mwao na kuwaokoa, akiwaletea maisha mapya na kuwafanya kuwa rejeo kwa
ajili ya kutangaza wema wake kwa mataifa yote. Katika mwendo huu wa ukombozi
watu walinganishwa kama mmea mdogo utakaokuwa mti mkubwa. Basi, Mungu atachukua
watu wake waliodhulumiwa na kuaibishwa, atawainua kama chombo cha wokovu wake.
Njia hii ya Mungu ya kutenda inakumbukika katika wimbo wa Bikira Maria: “Bwana
amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi, na akawakweza wanyenyekevu”.
Kulingana na Mtakatifu
Paulo, sisi ni kama wageni, watu waliohamishwa ulimwenguni huu, mbali sana
kutoka makao yetu. Sisi ni wa Mungu nasi hatuwezi kuridhishwa kwa ulimwengu
huu, kwa sababu zawadi kuu ya imani ambayo tumepokea kutoka kwake inautoa
mwelekeo kamili kwa maisha yetu ili tufikie marudio salama katika Mungu
mwenyewe. Zawadi ya imani inatuimarisha kuchukua utambulisho wetu wa Kikristo
kwa kutenda pamoja na Kristo ambaye anatungojea ili kututuza kulingana na
chaguzi ambazo tumefanya katika dunia hii. Sisi sote tunaalikwa kwa maisha
mapya ambayo Mungu anatupatia kwa neema yake, lakini bila kutenda kulingana na
mapenzi yake, maisha mapya hayawezekani.
Katika injili
Yesu anaongea kwa watu kwa kutumia mifano ili kutueleza kuhusu nguvu ya Ufalme
wa Mungu. Mfano wa kwanza ni kuhusu mbegu ambao unaota na kukua kwa nguvu yake mwenyewe;
ushiriki wa binadamu ni kuupanda tu na kusubiri wakati wa mavuno ili kukusanya
matunda. Wa pili ni kuhusu udogo wa kipimo cha mbegu ya haradali na ukuu wa
matokeo yake. Kwa nini Yesu aliongelea watu akiitumia mifano? Chaguo la Yesu
kwa njia hii ya kuongea ni kwa sababu yeye alijitambulisha na hali ya watu wanyenyekevu
na tena akitumia vipengele vya hali hii ilikuwa ni halisi ili watu wafahamu
ujumbe wake. Hivyo, kwa njia ya Yesu ya kuongea, mafumbo makubwa ya Ufalme wa
Mungu yalipatikana kwa watu walio wadogo na wanyenyekevu.
Katika ujumbe
wake, Yesu hakujitangaza mwenyewe; yeye aliutangaza Ufalme wa Mungu. Ufalme ni kiini
ya ujumbe wake. Kulingana na Yesu, hali na nguvu ya Ufalme wa Mungu haitegemei juhudi
za binadamu, bali hiki ni tendo la neema ya Mungu inayotolewa kwa hiari. Kila
mtu anaalikwa kutoa uwezo wake ili kusaidia kuujenga kwa Ufalme wa Mungu duniani,
lakini ufalme huu ni kwanza tendo la Mungu nao unamtegemea yeye sio binadamu. Kwa
upande wetu ni vizuri kutenda kama Mt. Yohana Calabria aliyechukua kama ahadi kutafuta
kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake kupitia imani na kujisalimisha kabisa kwa
riziki ya Mungu Baba. Mfano wake unatusaidia kufahamu kwamba hakuna kipaumbele
kingine katika maisha yetu ili tuweze kupata furaha kamili.
Watu wengi
miongoni mwetu ni wakulima na mifano hii pamoja na kuwa mafundisho kuhusu hali
ya Ufalme wa Mungu, tena ndiyo msaada ili waendelee kwa shughuli zao za kila
siku kwa uvumilivu na imani katika tendo la Mungu. Mifano hii inatualika
kuangalia mwendo wa ongezeko la mashamba katika uwanja, hasa kuhusu mahindi na
maharagwe. Sisi sote tunajua kwamba baada ya kazi ya kwanza ya kupanda tunaitegemea
mvua na nguvu ndani ya mbegu. Hiki ni kitendo cha Mungu anayethamini juhudi ya
binadamu kama ushiriki katika uumbaji na kutubariki kwa mavuno mengi.
Tumshukuru Mungu kwa nguvu ambayo anatupa ili kufanya kazi kwa uaminifu naye
aendelee kutupatia Baraka zake kwa manufaa ya familia zetu.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário