sábado, 13 de janeiro de 2018

UZOEFU AMBAO UNALETA MAANA YA KWELI KWA MAISHA YETU


Kutafakari kutoka Sam 3: 3-10.19; 1Wak 6: 13-15.17-20; Yoh 1,35-42

Wito wetu ndio historia ya upendo kwa sababu asili yake ndiye Mungu ambaye anajitoa mwenyewe anapomwita yeyote ili awe mtumishe wake. Kwa hivyo kila wito unaleta ukweli mkubwa, yaani: Ikiwa Mungu yuko, yeye anapenda; ikiwa anapenda, yeye anaita. ikiwa uhuru uko, asili yake ni Mungu; ikiwa binadamu yuko ndiye mwenye uhuru maana anatoka kwa Mungu; ikiwa maisha yako, yakatolewe kama Mungu mwenyewe anafanya. Katika kila wito ndiye Mungu anayechukua nafasi ya uhusiano wa upendo na mtu kwa kumwita kwa utumishi wa watu wake.
Wito wa Samueli, unaosimuliwa katika somo la kwanza, ni mfano wa wito wote. Mungu alikutana naye katika nafasi maalum na kumwita kwa jina lake akionyesha kwamba alimjua Samueli. Mtoto huyo alitolewa na mamaye kwa ajili ya Mungu na kukua hekaluni. Mungu alichukua nafasi hii kumwita Samweli ili awe mtumishi wake. Bila shaka Samueli alihitaji mwendo wa utambuzi ili kufahamu nia ya Mungu kwa maisha yake. Kuhani mkuu Eli alikuwa mpatanishi wa Mungu kumsaidia Samueli kuitambua sauti ambayo ilimwita kutoka ndani yake na kujibu kwa utayari. Mungu alimwita Samueli kwa mara tatu. Inamaanisha kwamba mwaliko wa Mungu kwa Samueli ulikuwa daima. Hivyo, Mungu hachoki kuwaita watu kwa sababu hii ni njia yake ya kuonyesha upendo kwao. Ni lazima kuwa macho na kuutafuta msaada ili kutambua sauti ya Mungu kati ya sauti nyingi zilizosikika na kujibu kwa mwaliko wake kwa ukarimu na utayari.
Kulingana na Mtakatifu Paulo, wito wetu ni kuwa sehemu ya mwili wa Kristo kama hekalu hai la Mungu. Kwa njia ya ubatizo Mungu ametufanya makao yake: Ninyi ni hekalu la Mungu na Roho wake anakaa ndani yenu.” Basi, kama sehemu za mwili wa Kristo, utambulisho wetu ni kuwa pamoja na wengine. Hatujaumbwa kwa upweke ama kwa ubinafsi bali kwa ushirikiano. Tunaishi wito wetu pamoja na wengine na kusaidiwa nao. Mungu alitaka kutumia hali yetu ya kimwili ili kuonyesha hali yake ya kimungu. Wakati tunaporuhusu kuongozwa na Roho wake tunaweza kumdhihirisha Mungu anayekaa ndani yetu. Hii ndiyo hali ya kwa mahekalu matakatifu ya Mungu. Hata bila kujua sisi tunasaidiwa ili kutimiza wito wetu kwa sababu sisi ndio wa Mungu.  
Injili inaongea kuhusu safari ya wito wa wafuasi wa kwanza wa Yesu. Mambo yote yaanza kwa uzoefu. Yohana Mbatizaji alikuwa na nafasi ya kukutana na Kristo na kumjua na kwa hivyo alikuwa na uwezo wa kumwonyesha kama “Mwana-kondoo wa Mungu, aondoaye dhambi za dunia”. Ushuhuda wake ulikuwa msaada mkubwa ili wafuasi wake waweze kumfuata Yesu. Wakati Yesu alipowaona aliwauliza swali la msingi wa safari yao, yaani, “mnatafuta nini”? Kweli katika sehemu ya mwisho wa injili ya Yohane swali hili litabadilishwa kuwa “mnatafuta nani”? kwa sababu kutafuta kwa wanafunzi sio kuhusu kitu bali kuhusu Mtu. Wafuasi wawili walijibu kwa kutumia swali lingine: “Mwalimu, unakaa wapi”? Swali hili linaonyesha kwamba walitaka kujua mwalimu kwa kweli na kukaa pamoja naye. Uzoefu huu ulibadilisha maisha yao na kusababisha moyoni mwao hamu ya kumtangaza Yesu ili wengine waweze kuwa na nafasi ya kuonja maisha mapya kama ilivyotokea kwao. Hivyo, Andrea alimjia nduguye Simoni na kusema “Tumemwona Masihi”, yaani tumemwona yule ambaye alileta maana ya kweli kwa maisha yetu.

Uzoefu wa “Njoni nanyi mtaona” uliopendekezwa na Yesu ndio changamoto kwetu. Hatuwezi Kumjua Yesu kwa haraka kwa kuisikiliza habari yake peke yake. Mwendo huu unachukua muda mrefu sana na kuhitaji uzoefu wa uwepo wake daima. Yeye mwenyewe anataka kujifunua kwetu. Lakini ufunuo wake ni pole pole na hatua kwa hatua kama ilivyotokea katika kifungu hiki cha injili ambapo Yesu aliitwa kwanzaMwana-kondoo wa Mungu” na baadaye “Mwalimu” na tena Andrea alisema “Masihi”. Hivyo, pendekezo ni kukubali mwendo wa kubaki pamoja na Yesu katika hali yake na kuruhusu kwamba hali yake pole pole na kidogo kidogo yachukuliwe na maisha yetu. Katika mwendo huu upatanishi ambao Mungu anatutumia ni muhimu sana mfano, Neno lake, hali ya jumuiya zetu, ndugu zetu walio na shida, shauri ya mtu mwenye busara na kadhalika. Bila mwendo wa utambuzi kupitia hali hizi ni ngumu kugundua mwaliko wa Mungu na kutambua sauti yake iliyotuita. Kama Samueli, tunahitaji kuwa macho kwa mwaliko wa Bwana na kujibu kwa mwaliko wake kwa utayari. Kama Eli, tunaalikwa kupatikana ili kuwasaidia wengine kugundua mapenzi ya Mungu kwa maisha wao. Turuhusu kongozwa na Neno la Mungu na kufunguliwa kwa hali kandokando yetu ili tuweze kuishi wito wetu kwa ahadi na uaminifu.

Fr Ndega

Nenhum comentário: