Kutafakari kuhusu Yoh 13, 31-35
Umuhimu wa andiko hili ni amri ya upendo kama
Yesu alivyofundisha. Kila kitu ambacho tunatenda kinapaswa kuwa alama ya
upendo. Tendo bila upendo halina maana. Mtume Paulo aliliweka wazi jambo hilo:
“Pia nikiwa na unabii, na kujua mafumbo yote na maarifa yote, na kuwa na imani
yote hata kuhamisha milima, nikikosa upendo, sina maana” (1 Wakorintho 13:2).
Mazingira ya andiko la siku ya leo ni ya
karamu ya mwisho ambayo Yesu alianzisha Ekaristi iliyo sakramenti ya upendo na
ya utumishi. Yesu alijua wazi kwamba Saa yake ilikuwa imefika. Katika injili ya
Yohane, kila ishara ambayo Yesu anatenda ni tangazo la Saa hii ambayo inajumuisha
mateso, kifo na kufufuka kwake. Kupitia Saa hii atamtukuza Baba na kutimiza
utume wake. Kwa upande wa wanafunzi wa Yesu, Saa hii ni kipindi cha uamuzi,
yaani, wanapaswa kuamua ikiwa wanataka kuendelea kazi ya mwalimu au la. Mwinjilisti
Yohane alitaja wakati kamili ambao Yuda alitoka mahali pa mkutano na tena wakati
wa kumtukuzwa kwa Yesu na Baba yake: “Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye
Mungu ametukuzwa ndani yake”.
Mazungumzo ya Yesu na Yuda na kuondoka kwake
kulikwa maandalizi kwa kipindi kifuatacho cha zawadi kubwa ya amri mpya kama
urithi wa Yesu kwa watoto wadogo wake. Yesu alikuwa akizungumza nao kama vile
mama na baba wanavyofanya na watoto wao. Yeye alishiriki nao hisia zake na kitu
muhimu sana, yaani, amri mpya ya upendo. Kwa upande wa wanafunzi amri hii siyo
amri mpya kwa sababu imekwepo tangu Agano la Kale. Lakini wanaalikwa kuiishi
kwa njia mpya, kulingana na njia aliyowafundisha Yesu. Basi, pamoja na zawadi
ya amri hiyo Yesu aliwaonyesha jinsi ya kuishi zawadi hii. Kipimo cha upendo
wao kinapaswa kufuata upendo wa Bwana wao, yaani njia yao ya kupendana inapaswa
kufuata njia aliyochagua Yesu.
Yesu anawapenda wanafunzi wake mpaka upeo, kwa
sababu hajui kupenda kwa njia nyingine. Ilikuwa kwa upendo kwamba Mungu alimtoa
Mwanawe pekee kwa wokovu wa ulimwengu. Upendo tu uliimarisha kazi yake katika
nyakati zote. Ilikuwa kwa upendo kwamba Mwana wa Mungu aliutoa uhai wake.
Umuhimu wa mafundisho yake ni upendo kama amri mpya na kama maana ya
utambulisho wa wanafunzi wake. kupitia kupendana wao kwa wao kama Yesu
alivyowapenda watu wote watawatambua kama wafuasi wa Yesu. Upendo wa Yesu ndio
msingi wa furaha yake, yaani, furaha ya ushirika wake na Baba, furaha ya kuishi
miongoni mwa binadamu, furaha ya kuwachagua baadhi ya wanadamu kama washirika kwa
ajili ya kazi yake na furaha ya kuutoa uhai kwa ajili yao. Akiushiriki upendo
na wafuasi wake, Yesu aliyajaa maisha yao kwa furaha kubwa, kwa maana kuna
uhusiano wa ndani kati ya upendo na furaha. Mtu anayependa kwa kweli yu mwenye
furaha ya kweli.
Kwa kupitia mfano wa unyenyekevu na utumishi Yesu
aliwapa wafuasi wake amri yake mpya. Basi, mfano huu unakuwa ushuhuda wetu wa
kwanza kwa ajili ya kutangaza Yesu na mafundisho yake. Uzoefu wetu wa undugu
unapaswa kuwa maonyesho ya imani yetu, kama ilivyotokea na uzoefu wa Wakristo
wa kwanza ambao watu walisema, “Mwone kama wanavyopendana!” Upendo wao
ulionyeshwa kupitia makaribisho wao kwa wao, kushiriki pamoja, ishara za mshikamano,
uvumilivu katika maombi pamoja na unyenyekevu wa moyo. Tunaalikwa kuchukua hayo
kama mpango wa maisha. Upendo unapaswa kuwa umuhimu kati yetu na maana ya kazi
zetu. Kupitia kupendana tu tunaweza kujitolea kama vile Kristo na kuwafanya
wanafunzi wapya kwake. Kupitia kupendana tu tunakuwa wajumbe wa habari njema
kwa wote. Kupitia upendo tu twatambua kwamba sio sisi ambao tunaofanya kazi
wala hatutendi peke yetu bali ndiye Mungu ambaye kupitia sisi anafanya yote na
kwa upendo.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário