Kutafakari kutoka Isaya 35:4-7; Yak 2:1-5; Mk 7: 31-37
Katika andiko la kwanza, nabii Isaya anatangaza
wakati ujao umejaa tumaini kwa sababu Mungu atatembelea watu wake kama mwokozi
na kuwatendea mambo makuu. Hali yote kandokando yao na miongoni mwao itabadilika
kuwa ni nzuri, hasa hali ya maskini na wengine walio na shida ya afya. Ahadi hii
ya kimasiya, Mungu alitimiza duniani kupitia Mwanawe Yesu Kristo ambaye aliwapa
wote uwezo wa kuishi maisha mapya na mazuri.
Katika andiko la
pili Yakobo anawaalika Wakristo kushinda tabia ya ubaguzi katika jumuiya kwa
kuthamini uwepo wa kila mtu bila kufikiria msimamo wake katika jamii.
Kipaumbele ya jumuiya inapaswa kuwa maskini kwa sababu ndio wenye heri wa Mungu
nao watapokea ufalme. Jumuiya za Kikristo haziko ili kufuata mawazo wa jamii
bali kutenda kwa njia ya kinabii kulingana na injili. Utabiri wao utaonyeshwa
wakati zinapopata kuwakaribisha na kuwanganisha katika uzoefu wake wote hasa wale
ambao wanakataliwa.
Katika injili, matendo
ya Yesu yanatambuliwa na watu ambao walitangaza, “amefanya yote vyema:
amewajalia viziwi kusikia, na bubu kusema”. Uwepo wa Yesu umeleta wakati mpya
ulimwenguni. Katika Yeye ufalme wa Mungu umekuwa hali halisi, ilipatikana kwa
wote. Wakati Yesu aliutangaza ujumbe wake katika sinagogi ya Nazareti, mahali
alipolelewa, alikataliwa. Lakini alikaribishwa sana katika upande wa ziwa
Galilaya, mahali panapoitwa Dekapoli - yaani miji kumi. Kulingana na toleo la
Mathayo, Galilaya lilifikiriwa “nchi ya watu wa mataifa”. Uwepo wa Yesu uliwafanya
watu waliokaa “gizani” waone mwanga mkubwa.
Basi, ingawa watu
hawa walikuwa na lugha na desturi tofauti na Wayahudi wa Yudea, walimtarajia na
kumkaribisha Masiya kwa hamu sana. Injili ya Marko inasisitiza kipengele hiki
kwa sababu iliandikwa kwa Wakristu wa huko Roma na lengo la injili hii ni
kujibu kwa swali “Yesu ni nani?”. Jibu kwa swali hili tunakuta katika wakati wa
mwisho wa maisha ya Yesu msalabani kutoka midomo ya jemadari mmoja wa Roma:
“Kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
Kama Mwana wa
Mungu, lengo la Yesu ni kutangaza wokovu wa Mungu si kwa watu fulani tu, bali kwa
wote. Yesu alikuwa Myahudi, bali hakuwa mali ya Wayahudi. Ishara zilizotumiwa
na Yesu zilidhihirisha kwamba wokovu wa Mungu si mpango kwa wakati ujao tu, bali
umekwisha anza katika historia kwa wote. Wakati tunaongea kuhusu “watu
waliochaguliwa” tunamaanisha mpango wa hekima ya Mungu ambaye anatumia baadhi
ya watu ili kufikia wengine kwa urahisi.
Hivyo, kutoka
Waisraeli Yesu na washirika wake walifikia wasio na Wayahudi pia wakitangaza
habari njema ya injili. Mtu yule aliletwa kwa Yesu alikuwa na matatizo mawili,
yaani, alikuwa bubu na kiziwi. Aliteseka sana na mara nyingi alikuwa mpweke kwa
sababu hakuweza kuwasiliana na wenzake kila alichofikiri au kutamani, na wengine
pia hawakuweza kuzungumza naye. Alitamani kukutana na Yesu na kupata maisha
mapya ili kuishi uhusiano mwema na wengine. Kabla ya kufanya mwujiza Yesu alimwalika
kuenda mahali pa faragha kwa sababu hakutafuta kuwa maarufu wala watafsiri muujiza
wake kwa njia siyo kweli. Muujiza wa kwanza Yesu anaotaka kutenda katika maisha
ya yeyote ndio kuwa na uhusiano wa ndani nawe. Yesu anatazama juu mbinguni kwa
maana ya ushirika wake na Baba aliye wa pekee aliyemwezesha kumponya Bubu
kiziwi. Hivyo, mkutano na Yesu kwa uhusiano wa ndani unaleta maisha mapya.
Kazi ya Yesu
ilikuwa kumwalika binadamu kutoka upweke na kutengwa kwa ushirika, yaani
ushirika na Mungu na wenzake. Kama wafuasi wa Yesu tunaimarishwa na mfano wake
na ishara zake. Ujumbe wetu unapaswa kuwa ni mwendelezo wa ujumbe wake na kama vile
yeye tunaalikwa kufanya mambo yote vyema, yaani matendo yetu na mahusiano yetu
yapaswa kufanya watu waishi maisha mapya. Yesu anatualika kwa uhusiano naye kwa
faragha ili kutuponya kwa maana sisi tu kama mtu bubu na kiziwi, yaani tuna
ugumu wa kusikiliza Neno la Mungu vizuri na kulitangaza kwa uaminifu. Matokeo wa
uhusiano wetu na Bwana yatakuwa ni matunda mazuri kwa ajili ya utukufu wa Mungu
na manufaa ya ndugu zetu. Ndiyo neema ya Mungu inayotenda ndani yetu ili tuweze
kutenda kwa jina lake. Kama injili haina mpaka, tunaalikwa kushinda vikwazo
ambavyo vinatuzuia kuwakaribisha wengine na kuwa na hisia mbele ya mahitaji
yao. Ikiwa ni kweli uhusiano wetu na Bwana, tulime hisia na tabia kama yeye ili
wengine wapate maisha mapya na sisi tuwe na furaha kamili.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário