sábado, 5 de maio de 2018

TUPENDANE ILI FURAHA YETU IWE KAMILI



Mdo. 10: 25-26, 34-35, 44-48; 1Yoh. 4: 7-10; Yoh 15: 9-17

      Mungu hawabagui watu kwa sababu anawapenda na katika upendo hakuna ubaguzi. Hivyo kuabudu kwa kweli kuandamana na kuishi kwa haki na undugu. Haiwezekani kumwabudu Mungu kwa kinywa peke yake na kuwa na moyo mbali sana naye. Ndiye Roho Mtakatifu ambaye anamwezesha yeyote kuwa na uhusiano wa kweli na Mungu. Ulikuwa hivyo uzoefu wa Petro nyumbani mwa Kornelio. Wakati Roho Mtakatifu alipowashukia wale waliolisikiliza Neno la Mungu kupitia kinywa chake Petro, alidhibitisha kwamba Mungu ndiye Baba aliye na macho kwa tamani ya moyo wa watoto wake wanaomwomba kwa imani sio muhimu taifa lake la asili. Mbele ya Mungu hakuna mtu aliye na heshima kuliko mwingine hata ikiwa mtu fulani ana upendeleo mbele ya wengine. Mungu anatarajia tu tuweze kujifunza kutoka kwake njia kamili ya kufikiri na kutenda.       
       Mtakatifu Yohana katika waraka wake anawaalika watu kupendana kwa sababu upendo unatoka kwa Mungu na wale wanaopenda wana asili yao katika Mungu na kumjua Mungu. Basi, kupenda ni kujua. Mungu anajua kwa sababu anapenda. Kumjua Mungu ni kumpenda, yaani, kuishi naye uhusiano wa ndani. Mungu ni upendo na kuwapenda watu mno hata alimtoa Mwana wa pekee kama maonyesho makuu ya upendo huu ili awafundishe watu jinsi ya kupenda kwa kweli. Kutokana na uzoefu huu tulipata uhai wa Mungu. Yeye anajua kwamba hatuwezi kumpenda hivyo lakini anatarajia angalau tupende wengine kama ndugu.
      “Mwana alitupenda kama Baba anavyompenda”. Andiko hili la injili ni sehemu ya ujumbe wa Yesu wakati wa Karamu ya Mwisho. Yaliyomo ya ujumbe huu ni urithi wake kwa wale ambao wanapaswa kwendelea kazi yake. Umuhimu wa mafundisho ya Yesu ni kupenda. Upendo una chanzo chake katika Mungu kwa sababu Mungu ndiye upendo na kumpenda Mwana. Uwepo wa Mwana miongoni mwa wanadamu uliufanya upendo huu ujulikane. Upendo ni hali ya ndani ya Mungu; huu ni maana ya ushirikiano wake. Wanadamu ni matokeo ya ushirikiano huu na kualikwa washiriki katika ushirikiano huu sawa, kwa kupitia upendo wa Kristo. Kipimo ili tukae katika upendo wake ni kuishi mafundisho yake, yaani, kupendana kama alivyotupenda na kujitoa kwetu. Yesu halazimishwi kutupenda. Upendo wake ni maonyesho ya furaha yake, yaani: furaha ya ushirikiano wake na Baba, furaha ya kuishi miongoni mwa wanadamu, furaha ya kuwachagua wanadamu kama washirika katika kazi yake, furaha ya kujitolea kwa ajili yetu. Tukibaki katika upendo wake, Yesu anahakikishia furaha kubwa kwetu kwa sababu kwake hali ya upendo unaihusu furaha. Hivyo, mtu tu anayependa kwa kweli ni mwenye furaha ya kweli.  
     Upendo ni maana ya wokovu wa ulimwengu, kwa sababu ilikuwa kwa upendo kwamba Mwana wa Mungu aliyatoa maisha yake. Kulingana na Yesu, kipimo cha urafiki wa kweli ni kuyasalimisha maisha kwa upendo. Yesu ni rafiki yetu kwa sababu alifanya hivyo vizuri sana. Alituchagua na kututuma tuyazae matunda, na matunda yanayodumu. Tutakuwa marafiki zake ikiwa tuwe na ujasiri wa kupenda kama yeye alivyopenda. Anajitambulisha na wale wanaotumwa kwa jina lake. Utambulisho huu ni matokeo ya upendo wake ndani yetu kwa sababu tabia ya upendo ni kuuzaa utambulisho na kusababisha hisia ya kujiungana na mtu fulani. Ikiwa tunakaa katika upendo yake tutakuwa watu wa ushirikiano na kuweza kutoa ushirikiano katika jumuiya zetu. Huu ni ushuhuda wetu  wa kwanza: “Mwone kama wanavyopendana”! Ilikuwa maoni kuhusu Wakristu wa Kwanza. Upendo wao ulionyeshwa kupitia ridhaa wao kwa wao, kushiriki pamoja, uvumilivu katika maombi pamoja na unyenyekevu wa moyo. Je, maisha yetu ni maonyesho ya yale ambayo sisi huamini? Itawezekanaje jumuiya zetu kuishi hali hiyo ya Jumuiya za Kwanza?
Pamoja na kuuzaa ushirikiano katika jumuiya, upendo unatufungua kwa watu wengine nje, wanaohitaji kukaribishwa pia. Ndio kuhusu upendo huu ambao Yesu anatuambia siku ya leo, yaani, upendo tofauti ya mawazo ya jamii, upendo ulio na tabia ya kujitolea na kujisalimisha bila kuwabagua watu. Tunaalikwa kujifunza kutoka kwa Mungu anayewapenda wote lakini ana upendo maalum kwa maskini na wale ambao hawana nguvu. Vivyo hivyo, kama anavyotenda akinamama ambao wanawapenda watoto wake wote, lakini wana utunzaji maalum kwa mtoto mgonjwa. Kwa maneno mengine, tunaalikwa kupenda hasa wale ambao sio muhimu wala wanaweza kutupenda kwa kipimo sawa. Ahadi yetu ya Kikristo ndiyo kukaa katika upendo wa Kristo ili tukute msaada na msukumo kwa kupendana na kuwa macho kwa hali ya wale wanaohitaji zaidi katika jumuiya zetu.    

Fr Ndega

Nenhum comentário: