Kutafakari kuhusu Mdo. 2,1-11; 1Kor. 12,3b-7.12-13;
Yoh 20,19-23
Siku ya leo
tunasherehekea ujio wa Roho Mtakatifu juu ya wanafunzi wa kwanza na mwanzo wa
utume wa Kanisa, lililo Jumuiya ya Agano Jipya. Sherehe hii inatuhakikishia
kwamba Roho Mtakatifu ndiye kuwepo kanisani na ndani ya kila mmoja wetu. Huyo
ndiye Roho wa Yesu na Baba aliye Roho wa faraja kwa wale wanaohisi kutokuwepo
kwa Yesu kwa kimwili. Huyo ndiye Roho wa nguvu kwa wale wanaohitaji ujasiri ili
wawe mashahidi wa makuu ya Mungu kwa wote. Huyo ndiye Roho wa umoja ili
ushahidi wetu kwa Yesu uwe wa kuaminika.
Kulingana na somo la kwanza, wafuasi walikusanyika kusali wakishiriki
pamoja matarajio yao kuhusu ahadi ya Yesu pamoja na mama yake na wanawake wengine,
lakini walikuwa wamejawa na hofu kwa sababu ya upinzani wa jamii ya Wayahudi
dhidi ya mafundisho ya Yesu na wafuasi wake. Yesu aliahidi kuandamana nao siku
zote, lakini walikuwa hawajafahamu bado maana ya uwepo huu. Walihitaji nguvu
kutoka juu kwa uelewa kabisa kuhusu maneno ya Yesu. Hao walisubiri wakimwomba
Mungu kwa uvumilivu na imani ili wapate nguvu hii. Ghafla, Roho aliwashukia
wote kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Ndimi hizi za moto zilizo
mfano wa zawadi za Roho Mtakatifu, zilichoma hofu ambayo iliwazuia kuongea na
kuwafanya kuwa mashahidi jasiri.
Mwinjilisti Luka anasema kwamba Roho Mtakatifu alikuja katika Sikukuu ya
Pentekoste ambayo Wayahudi walisherehekea Sikukuu ya Majuma ama ya mavuno. Tena walikumbuka
utoaji wa Amri kumi Mlimani Sinai. Kwa wanafunzi wa Yesu hii imekuwa Sikukuu ya
uumbaji mpya kwa tendo la Roho wa Yesu. Mungu alifanya Agano jipya na watu
wapya. Kwa hivyo ishara nyingi za ajabu zilionyeshwa kama zilitokea katika
Agano la kwanza, yaani moto, tetemeko la ardhi, upepo wa nguvu na kadhalika.
Hivyo, Kanisa lililo jumuiya ya Agano Jipya, lilianza safari yake kwa nguvu
ambayo ikalifungua kwa dunia nzima. Zawadi
ya lugha mbalimbali inaonyesha kwamba Kanisa linatumwa kwa wote na kuongea nao
kwa lugha rahisi ili iwafanye watu wote wawe familia moja.
Kwa upande wa injili ya Yohane, Roho Mtakatifu ndiye zawadi iliyotolewa
katika siku ile ya Ufufuko kama alama ya maisha mapya ya Yesu Mfufuka kwa wote.
Yeye aliingia katika mahali
ambapo wanafunzi walikusanyika ili kuwasaidia kushinda hofu na kugundua tena
msukumo katika safari yao. Yesu aliwavuvia akiwapa Roho Mtakatifu. Lakini kabla
ya kuwapa zawadi hii kubwa Yesu alisimama katikati yao na kuwahakikishia hali
nzuri kama maandalizi ya kupokea Roho yake Mtakatifu.
Kwanza kabisa, aliwapa
zawadi ya amani nao walifurahia uwepo wa Bwana Mfufuka. Yesu aliwashirikisha
katika kazi yake akiwatuma kama mashahidi wa furaha ili watangaze mambo makuu
ya Mungu. Watapaswa kutangaza huruma ya Mungu na upatanisho kati ya watu. Kazi
hii muhimu haiwezekani kufanya bila msaada wa Roho Mtakatifu. Kwa hivyo, Yesu
aliwapa Roho yake kwa hiari. ‘Roho
waliyempokea kutoka kwa Yesu anawafanya wapya na kuwapa nguvu ya kufanya
maajabu kwa jina la Yesu.’
Hili ndilo tendo
la Roho Mtakatifu maishani mwetu tulio wanafunzi wapya wa Yesu. Ikiwa katika
tukio la pentekoste Roho Mtakatifu aliwakalia kila mmoja wa wanafunzi wa
kwanza, yeye anaendelea kufanya kazi kwa ajili ya wanaomfuata Yesu kwa vizazi
vyote. Sisi tumepokea Roho Mtakatifu huyo tangu ubatizo wetu. Makaribisho ni ya
kibinafsi lakini uzoefu huu tunaishi katika jumuiya na kwa ajili ya jumuiya ya
wanafunzi wa Yesu. Kwa kifupi, “kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho Mtakatifu kwa
kufaidiana.”
Ingawa hatutambui, sisi tumeongozwa na Roho Mtakatifu kila wakati.
Hivyo, hatuwezi kusema Yesu ni Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Tena
hatuwezi kutenda mema ama kumwomba Mungu kama ipasavyo isipokuwa katika Roho
huyo. Ingawa sisi ni wa tamaduni
mbalimbali na kuongea lugha nyingi, tunaweza kupanga pamoja kwa ajili ya wote
kwa sababu ya Roho huyo ambaye anaongea lugha moja peke yake, yaani lugha ya
upendo iliyo lugha ya msamaha na ya amani. Roho Mtakatifu atupatie lugha hii.
Fr Ndega
Kiswahili review: Christine Githui
Nenhum comentário:
Postar um comentário