Kutafakari kutoka Kum
8,2-3.14b-16a; 1Wak 10,16-17; Yoh 6, 51-58
Tunasherehekea
sikukuu ya chakula kinachodumu milele, yaani Ekaristi takatifu. Hii ni
sakramenti ya uwepo hai wa Yesu kati yetu. Asili ya sherehe hii ni Karamu ya
mwisho katika Alhamisi Takatifu lakini hali ya ukimya na tafakari kwa sababu ya
Ijumaa Kuu inatuzuia kusherehekea kwa
furaha kubwa. Kwa hivyo Baba Mtakatifu Urbano wa IV katika karne ya 13
alianzisha sherehe hii ya Mwili na Damu ya Kristo. Katika sikukuu hii tunaweza
kutangaza hadharani imani na upendo wetu kwa Ekaristi Takatifu na kujiona
kuungana na Kristo anayefanya upya ishara yake ya upendo kwa ajili ya wokovu
wetu na kutualika kwenye karamu ili tuweze kushiriki furaha yake kubwa na uzima
wa milele.
Masomo haya ni
uthibitisho kwamba ndiye Mungu mwenyewe anayewalisha watu wake. Muda ambao Watu
wa Israeli waliishi jangwani ulikuwa nafasi ya kumjua Mungu kama Mtoaji ambaye
aliwapatia chakula tofauti na kile cha Misri. Walipokea Mana kutokana na
ukarimu wa Mungu kwa ajili ya kufanya upya nguvu zao za kimwili na kuwaimarisha
kumshukuru Mungu aliyekuwepo miongoni mwao daima. Kulingana na Mtakatifu Paulo,
chakula ambacho Mungu anawapatia watu wake wapya ndiye Mwanawe. Yeye anawaalika
wote wale mwili na damu yake ili tuwe wamoja naye. Ingawa sisi ni wengi
tumefanyika mwili mmoja kwa sababu ya Mkate mmoja tunaoumega ulio Kristo
mwenyewe.
Katika injili
Kristo aliwaalika wasikilizaji wake kuukaribisha ufunuo juu ya utambulisho wake
kama chakula kilichoshuka kutoka mbinguni si kwa binadamu tu bali kwa ajili ya
uhai wa ulimwengu wote. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata
alimtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa
milele (Jo 3, 16)”. Mwana anajitoa kama chakula kinachodumu hadi uzima wa
milele kwa sababu ya mapenzi ya Baba aliye chemchemi ya uzima. Yeye ndiye
anayesababisha uzima ndani ya kila mtu anayempokea Mwanawe. Tunaongea hapa
kuhusu kiini cha mafundisho ya Yesu kama mwokozi na mkombozi wa ulimwengu,
lakini wasikilizaji wa Yesu hawakuweza kuelewa kwa sababu walijua hali ya Yesu
ya kibinadamu. Waliwajua wazazi wake, yaani Yusufu na Maria na kushiriki pamoja
naye katika shule moja. Hakika hawakuweza kukubali kwamba mwenzao huyu alishuka
mbinguni. Lakini ugumu wao haukumzuia Yesu kufunua njia iliyojaa maana kwa
maisha yao.
Yesu anaongea
kuhusu uzima bila mwisho unaopatikana kwa wote. Inawezekana kuupokea uzima huu
kwa kuula mwili wake na kuinywa damu yake, kwa sababu yeye ndiye uhai na huishi
ndani ya wale wanaompokea. Yesu anatenda ishara hii ya upendo kwa uhuru kabisa
na kulenga kukaa miongoni mwa wanadamu na ndani ya kila mtu. Hiki ndicho kipimo
cha kupata uzima. Hilo ndilo fumbo la Ekaristi takatifu. Ndiyo zawadi kutoka
kwa Mungu ambaye hataki kuishi mbali na binadamu. Ekaristi ni hazina ya kanisa
na kiini cha uzoefu wake. Ekaristi inalifanya Kanisa na Kanisa linaishi kwa
Ekaristi. Kulingana na Mtaguso Mkuu wa Vatikano wa pili, “matendo yote ya
Kanisa yatoka kwa Ekaristi na kulenga Ekaristi”. Ndivyo hivyo kwa sote
tunaoumega mkate mmoja na kunywa kikombe kimoja. Uzoefu huu ni ukamilifu wa
ushirika wetu na Mungu na msukumo kwa ahadi yetu ya kindugu.
“Tunapokula
chakula cha kawaida mwili wetu unaingiza chakula hiki ili uwe na afya nzuri.
Hivyo, chakula kinaingizwa na mwili wetu. Kuhusu Ekaristi, chakula cha uzima,
matokeo ni tofauti: wakati tunampokea Yesu, ni sisi tunaoingizwa naye”. Kwa
maneno mengine, Yesu anatuingiza, anatuchukua kwake ili tuishi naye na kwa
sababu yake. Yeye anakaa ndani yetu nasi ndani yake. Yeye anatuunganisha naye,
kutuhusisha katika ushirika sawa anaoishi na Baba. Katika uzoefu huu
tunabadilika kuwa yule tunayempokea kwa ajili ya ukuaji wa mwili mmoja. Hivyo,
wakati tunaposherehekea Ekaristi kwa kina mahusiano kati yetu yabadilika na
sisi tunakuwa vyombo vya umoja, upatanisho na amani kulingana na hisia za
Kristo.
Fr Ndega
Mapitio ya Kiswahili: Christine Githui
Nenhum comentário:
Postar um comentário