Kutafakari kutoka Yer
20,10-13; War 5, 12-15; Mt 10: 24-33
Mazingira magumu
ni sehemu ya maisha yetu ya binadamu. Katika safari tunakabiliana na changamoto
nyingi. Mara nyingi tunaogopa kwa sababu tunafikiri kwamba tunaweza kushinda
magumu kwa nguvu zetu peke yake nasi tunashindwa. Hapa ni muhimu kugundua tena
kiini cha ujumbe wa Kikristo, yaani ubaba na utunzaji wa Mungu kwa watoto wake.
Ujumbe huu ni habari njema inayotupa maana ya kuishi kwa tumaini na kusadiki
kwamba mambo yote ulimwenguni ni sehemu ya mpango wa hekima ya wema wa Mungu
ambaye anatenda makuu hata mbele ya udhaifu na maovu ya kibinadamu. Mazingira
ni magumu lakini tuko na Mungu aliye Baba.
Nabii Yeremia ni
mfano wa hali hii. Yeye alikabiliana na mazingira magumu na kuteseka kwa sababu
ya uaminifu wake kwa Mungu aliyemwita kuwa nabii tangu tumbo la mama yake.
Uhakika kuhusu ulinzi na utunzaji wa Mungu ulimwimarisha wakati wote wa safari
yake. Katika maneno ya Yeremia tunaweza kutambua kwamba alikuwa na uhusiano wa
ndani na Mungu. Uhusiano huu ndio maana ya uvumilivu wake na kuwaaibisha maadui
yake. Yule anayemtumainia Mungu hakati tamaa kwa sababu Mungu hawaachi
waliomtumainia yeye. Kulingana na somo la pili, tuko na maana za kuamini kuliko
kukata tamaa kwa sababu, ingawa wanadamu wote waliguswa na dhambi ya Adamu nao
walitenda dhambi, neema ya msamaha ambayo ilikuja kwetu kwa Yesu ilishinda mno
hali ya dhambi. “Mbele ya ukubwa wa dhambi, Mungu anajibu kwa msamaha
kamili. Huruma itakuwa daima kubwa kuliko dhambi yoyote, na hakuna awezaye
kuuwekea mipaka upendo wa Mungu anayesamehe daima” (Papa Francisco).
Katika injili,
Yesu aliwaambia wanafunzi wake “Msiogope." Je, kwa nini alisema hivyo kwa
mara tatu? Alisisitiza kwa neno “Msiogope" kwa sababu alitaka wawe mashahidi
jasiri wa uzoefu ambao ulibadilisha ulimwengu ukishinda giza na kuzifukuza hofu
zote. Yesu alijua kwamba wataonja mateso kama yeye na kwamba imani yao ni haba
kwa kubaki imara. Kwa hivyo, aliwahakikishia uwepo wake maishani mwao na
kuongea kuhusu utunzaji wa Mungu kwao. Kwa Mungu maisha yao yanathamani sana.
Mungu anaweza kubadilisha hali mbaya kuwa hali nzuri. Anafanya hivyo kwa sababu
anawapenda na kuwatunza wale ambao aliwachagua. Maneno haya ya Yesu
yaliwaimarisha ili waiendeleze kazi ambayo yeye aliwakabidhi.
Wakati Yesu
alishiriki mamlaka yake na wanafunzi wake alilenga waweze kutangaza kwa wote.
Hii ni maana ya habari inayopaswa kutangazika hadharani. Kiini cha ujumbe wao
ni utunzaji wa Mungu anayeshughulika hata kwa mambo madogo ya maisha. Kwa
kutangaza ujumbe huu wanafunzi wanapaswa kushinda hofu kwa sababu hali ya hofu
inaonekana kukana ukweli wa ujumbe huu. Tunajua kwamba ukatili dhidi ya wajumbe
wa Mungu ulikuwepo zamani na unaendelea siku hizi. Lakini wameutendea mbaya
mwili tu. Shida inaanza wakati wanaochaguliwa sio waaminifu na kusababisha
kashfa, wakivuruga wale wanaotaka kusadiki. Hali hii ni kifo cha mwili na roho pamoja.
Tunataka
kukumbuka Waathirika wa ukatili kwa sababu ya Imani katika nyakati zote. Kama
mwalimu wao, walibaki imara katika ahadi yake. Njia yao ya kuishi mbele ya
ukatili imewaaibisha maadui zao na kuwasaidia kutafakari. Siku moja Yesu
aliwaambia wanafunzi wake, “Mtu akikupigia kofi shavu la kulia, mgeuzie pia la
pili”, yaani njia tofauti iliyo njia kamili ya kutenda. Ukatili hauwezi
kushinda ukatili bali ndio wema wa moyo unaoweza kufanya hivyo.
Hata sisi
tunapoona hali mbaya tunajaribiwa kuwa na hofu, kukata tamaa, kufa moyo na
kuacha ahadi yetu. Lakini uhakika wa uwepo wa Yesu na utunzaji wa Mungu
unatuimarisha kuendelea na safari. Kwa hivyo maneno haya ya Yesu ni faraja pia
kwetu: “Msiogope”! Mwe na imani tu! Mungu anajua jinsi ya kubadilisha hali
mbaya kuwa hali nzuri. Yeye anajua analofanya. Matarajio yake, kulingana na
mafundisho ya Yesu, ni kwamba tujione watoto wake na kwa hivyo, tumruhusu
kutenda maishani mwetu kulingana na mapenzi yake. Tusiogope kwa maana tuna
thamani kuliko shomoro wengi na Mungu hawaachi wanaomwamini na kumtumainia yeye.
Fr Ndega
Mapitio ya Kiswahili: Christine Ghitui