Mtdo 1, 1-11; Waef 1, 17-23; Mt 28, 16-20
Maandiko haya
yanaongea kuhusu fumbo la uwepo wa Yesu. Yesu hakumwacha Baba alipokuja kwetu
na hakutuacha alipomrudia Baba. Kupaa kwake Yesu kunaongea kuhusu njia mpya ya
uwepo wake miongoni mwetu kwa kutangaza hatua mpya ya kazi yake. Huu ni wakati
wa Kanisa, jumuiya ya wanafunzi wa Yesu. Ujumbe muhimu kuhusu hayo ni wazi sana
katika maandiko mawili ya Luka, yaani, Injili na Matendo ya Mitume. Katika
Injili yeye anajulisha vitendo vya Yesu, na andiko la Matendo ya Mitume anajulisha
vitendo vya wanafunzi wake waliosaidiwa na Roho wake, aliye nguvu ya juu
atauhakikisha uwepo wa Yesu miongoni mwao.
Mizimu ya Yesu
kwa baadhi ya muda iliwaimarisha wanafunzi wake kugundua tena maana na furaha ya
kuwa wanafunzi. Uzoefu huo wa kuona Yesu Mfufuka ulikuwa mpya sana kwao naye
Yesu alifahamu kwamba alipaswa kuwa na uvumilivu kwa sababu ya imani yao haba. Kulingana
na andiko la injili, baadhi yao waliona shaka bado. Hakika shaka hili halikuwa
kuhusu hali ya ufufuko wa Yesu bali ni kuhusu uwezo wao wenyewe wa kuutangaza
ukweli huu. Walikuwa kumi na mmoja kwa sababu Yuda hakuwa tena kikundini, lakini
namba hii inaweza kuwa pia ya mfano, yaani kama kumi na wawili ni makabila ya
Israeli, kumi na mmoja ni namba ya wanafunzi Yesu aliwatumia kwa watu wote.
Walitumwa kueneza injili kwa ulimwengu kote.
Kulingana na somo
la kwanza, katika maneno ya mwisho kwao, Yesu aliwasaidia kufahamu uhusiano
kati ya kila kitu alichotenda na kufundisha na hali ya Ufalme wa Mungu. Hali ya
Ufalme huu ilidhihirishwa kwa ishara za Yesu na kuendeleza kwa matendo ya Kanisa
mpaka miisho ya ardhi. Kabla ya kuanza kazi hii kwa dunia nzima, wanafunzi waliipokea
nguvu kutoka juu. Kwa nguvu hii waliweka tayari kuwa vyombo vya wokovu wa Mungu
wakifanya wanafunzi wapya kwa ajili ya Kristo. Roho mmoja aliyekuwepo mwanzoni mwa
uumbaji na mwanzoni mwa kazi ya Yesu ataiongoza kazi ya jumuiya ya wanafunzi
wake.
Wanafunzi
waliitwa na Yesu kuenda pamoja kwenye mahali fulani huko Galilaya. Kutoka
mahali huko walitumwa pamoja tena
kuinjilisha kwa sababu ushahidi wa kwanza wa jumuiya ya wanafunzi wa Yesu ni
umoja utakaohakikishwa na Roho yake. Kila mtu anaitwa kuweka juhudi kwa ajili
ya kuusaidia umoja huu kama maana ya utambulisho. Tumezipokea zawadi kutoka kwa
Mungu ili tuwe zawadi sisi kwa sisi na kuendeleza kuujenga mwili mmoja, ambao
ni takatifu na hai kwa sababu ni Roho mmoja anayetenda ndani yake. Hivyo, uwepo
wa Yesu ni muhimu sana kwa ajili ya nguvu na ufanisi wa wanafunzi wake, kwa maana
mwili bila kichwa unakufa. Siku moja alisema, “Bila mimi hamuwezi kufanya
chochote”.
Ndiye Yesu peke
yake na mamlaka aliyopokea kutoka kwa Baba ya kudhihirisha mpango wake wa
wokovu. Alishiriki mamlaka haya na wanafunzi wake kwa ajili ya kufanya
wanafunzi wapya miongoni mwa watu. Wanafunzi walitumwa kama wajumbe wa habari njema kwa
wanadamu wote kwa sababu injili haina mipaka. Yesu aliwaahidi kuandamana nao
mpaka upeo. Ingawa uwepo wake wa mwili hauonekani tena, Roho wake anahakikisha
ukaribu wake katika safari yao kwa sababu kama Yesu alitenda pamoja na Baba na
Roho Mtakatifu, vivyo hivyo Roho huyo anatenda pamoja na Yesu na Baba. Ikiwa
wanafunzi wanaruhusu kuongozwa na Roho huyo wanaweza kuwashirikisha wengi
katika mpango wa Yesu ulio mpango wa Utatu Mtakatifu. Kuwa mwanafunzi wa Yesu
ni kuwa makao ya Utatu Mtakatifu.
Malaika wawili waliwaambia
wanafunzi wa kwanza na wanatuambia siku ya leo: “mbona mmesimama mkitazama
mbinguni?” Hakika kama Wakristo tunahitaji kuelekeza mtazamo wetu kwa Yesu,
mfano wetu na kichwa chetu ili tuendeleze kazi yake kwa uaminifu, lakini hatuwezi
Kukaa kusimamishwa kutazama mbinguni. Kama wanafunzi wake tunaitwa kuendeleza
kazi yake kwa kuandaa kurudi kwake katika mwisho wa nyakati. Bwana anatutaka
wenye uangalifu na fanifu kwa sababu “Wabarikiwa watumishi wale ambao watakuwa
wakitumikia Bwana wao atakaporudi”. Ahadi ya Kikristo kuhusu maisha ya
kibinadamu kwa kusaidia amani na upatanisho kati ya watu ni ishara ya
maandalizi yetu kwa kurudi huku.
Basi, “Maisha ya
Kikristo ni njia; siyo njia ya huzuni bali ni njia ya furaha” kwa sababu pamoja
na Kristo, sisi tuko katika mwendo wa kupaa mbinguni, bali kwa miguu imara
katika nchi hii ya utume. Maisha ya Kikristu ni tafakari na kitendo, imani na
matendo. Ishara za uwepo wa Yesu ulimwenguni zinatambuliwa kwa mapendo ya wale
wanaomwamini na wanayofuata nyayo yake. Kwa ajili ya hayo tuko na msaada wa
Roho Mtakatifu ambaye sio anakaa ndani yetu tu, bali anatenda pia ili atufanye kuwa
kulingana na jina letu, yaani Wakristo, “Kristo mwingine”. Kwa hivyo tuseme,
Uje Roho Mtakatifu!