Kutafakari kuhusu Yoh 20,19-31
Jumapili hii inaitwa “Jumapili ya huruma”.
Tuko na mengi ya kujifunza kuhusu jambo hili lililo tabia ya msingi ya
kitambulisho yetu ya Kikristo. Yesu mwenyewe anatuhakikishia: “Heri walio na
huruma, maana watahurumiwa” (Mt 5:7). Kulingana na Baba Mtakatifu Francisco,
“Yesu Kristo ni uso wa huruma ya Baba. Fumbo la imani ya Kikristo linaonekana
kukuta awali yake katika neno hili (...) Tunahitaji kutafakari fumbo la huruma.
Hiyo ndiyo chemchemi ya furaha, utulivu na amani.”
Somo la kwanza linaongea
kuhusu njia ya Wakristo wa kwanza ya kuishi kilicho kipimo cha utambulisho wa
jumuiya za Kikristo za nyakati zote. Wakristo wa zamani walipata mafanikio
katika safari yao kwa sababu ya vipimo vinne, yaani “mafundisho ya mitume,
kuishi pamoja kindugu, kumega mkate na kusali.” Njia ya kuishi kama wamoja iliwavutia
wengine wengi ambao walitambua katika matendo yao ya ajabu tendo la Bwana aliye
Mfufuka. Hivyo, kwa ushuhuda wao watu
wengi walikutana na huruma ya Mungu.
Akiongea na watu wa
Jumuiya za Kikristo ambazo zilikabiliana na migogoro mingi, Petro aliwahamasisha
kwa maneno ya kutia moyo akiwaalika kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake
kubwa. Kwa ufufuko wa Kristo yeye Mungu alitufanyisha kuzaliwa tena kwa tumaini
hai ambayo haikatishi tamaa. Ingawa tukabiliane changamoto na mateso mengi
tunaalikwa kuishi imani yetu kwa furaha na kwa ahadi mpaka tupate lengo la
imani hii, yaani wokovu.
Baada ya kuona ukatili
kwa Bwana wao, wanafunzi wa Yesu waliishi katika mazingira ya hofu. Hawakutaka
kuwa na mwisho sawasawa wa mwalimu wao, lakini waliendelea wanakutana hata kwa
siri. Mambo mengi ambayo walijifunza kutoka kwa Yesu yalikuwa maana ya utambulisho
wao. Basi, ingawa walikuwa na hofu hawakuwa wasio na tumaini kwa sababu yule
aliyewaita kumfuata hangewaacha peke yao. Kweli aliwataka kama mashahidi wake.
Akijua kwamba
walihitaji msaada, Yesu aliwajia akiingia bila kufungua milango na kusimama
katikati yao kwa sababu alitaka kuwa rejeo maishani mwao. Bwana Mfufuka ndiye
mwenye uhuru na kupanga kufanyisha wenye uhuru wale ambao wanamfuata. Wanafunzi
hawa walikuwa watumwa bado, yaani watumwa wa hofu zao, wa mashaka yao, wa
mawazo yao ya Masihi yaliyokatisha tamaa na moyo wao wa kijiwe. Yeye alikuja
kuwasaidia kushinda yote hayo katika safari yao ambayo yaliwazuia kumshuhudia kwa
kweli.
Matokeo ya kwanza ya
uwepo wa Bwana Mfufuka kwa wanafunzi ni furaha, yakithibitisha kwamba kuwa mwanafunzi
wa Yesu ni kuwa mwenye furaha. Furaha inaifungua milango ya moyo kwa kuzipokea
zawadi zingine. Bwana Yesu anawapa amani kama utambulisho naye aliye “Nabii
asiye na ukatili”. Hivyo walikuwa vyombo vya amani. Pumzi ya Roho Mtakatifu ni ishara
ya maisha mapya kwa ubinadamu uliofanyika upya kabisa kwa msalaba na ufufuko wa
Kristo. Watu wapya hawa wakiishi kwa ushirika na Yesu na kwa msaada wa Roho
Mtakatifu walitumwa kwa wajumbe wa huruma ya Mungu kwa kupitia msamaha na
upatanisho.
Kwa upande
mwingine, tunaweza kusema kwamba mfano wa Thomas unafanya jumuiya kushuhudia
imani yake kwa kweli na kuaminika. Haitoshi
kusema “tumemwona Bwana!”. Bali ni lazima kumtambua na kumtangaza bila hofu
kama “Bwana wangu na Mungu wangu!”. Kwa sababu ya Thomas, Yesu anatangaza
maneno haya ya ajabu, yaani “Heri walioamini bila kuona.”
Kupitia mitume yake
kama msingi Yesu ametupa zawadi ya imani na kutuomba tuishi imani hii pamoja na
wengine, kwa kupendana na kusaidiana kama matokeo ya maisha mapya kutokana na
ufufuko wa Bwana wetu. Mtu ana ugumu wa kuamini ikiwa anaamini peke yake. Imani
yetu ni matokeo ya uzoefu wa kikanisa, kwa sababu imani ya Kanisa inaitangulia,
inaizaa na kuiimarisha imani yetu. Bila ushiriki kwa hamu katika Jumuiya ya kikanisa,
tuko na ugumu wa kutambua ishara za uwepo wa Bwana Mfufuka miongoni mwetu na
imani yetu inakuwa haba na tena ndiyo hatari kwa imani ya wengine.
Andiko hili linatusaidia
kutambua umuhimu wa kushiriki pamoja katika jumuiya. Bwana Mfufuka alitaka
kujifunua kwetu kupitia msaada wa wengine. Tunapaswa kuwa macho kwa mwelekeo wa
ubinafsi katika jamii ambao umeshawishi mahusiano yetu ya wanafunzi wa Kristo na
kuuvuruga undugu wetu. Kwa njia ya ubinafsi maovu mengi yanatujia. Ni lazima
kumchukua Yesu kama kipimo cha uzoefu wetu wa jumuiya nayo jumuiya inapaswa
kuwa na nafasi muhimu katika maisha yetu ili tuweze kushinda hofu na kutokuwa
na imani ili ushuhuda wetu uwe ufanisi katika hali iliyo kandokando yetu.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário