domingo, 11 de março de 2018

MUNGU ALIUPENDA ULIMWENGU HATA AKAMTOA MWANAWE WA PEKEE



Kutafakari kuhusu Yoh 3, 14-22


            Baada ya tukio ambalo Yesu aliwafukuza watu nje ya hekalu, mkuu mmoja wa Mafarisayo aliyeitwa Nikodemo alimtafuta Yesu wakati wa usiku ili kukutana nawe. kukutana na Yesu ni hamu ya moyo wa binadamu. Lakini ni lazima kutambua ikiwa yeyote anamtafuta Yesu ni kwa sababu Yesu alimtafuta kwanza. Kukutana na Yesu ni kukutana na Mungu, kwa sababu Yesu mwenyewe alisema, “yeyote anayeniona mimi anamwona Baba,” na “mtu anayenikaribisha mimi anamkaribisha Yule aliyenituma.” Nikodemo alishangaa kwa sababu ya tabia ya Yesu ya kinabii, lakini alipendelea kubaki amefichwa kwa sababu ya hofu ya wenzake Mafarisayo.

Tunakuta vifungu vingine viwili ambavyo Nikodemo alionyesha upatikanaji fulani kwa ajili ya Yesu. kifungu kimoja ndicho wakati alipowakumbusha wenzake wa Baraza kuu wa Wayahudi kwamba Sheria hairuhusu kumlaani mtu bila kumhukumu. Katika kifungu kingine alionekana pamoja na Yosefu wa Arimathaya ambaye alimwendea Pilato na kumwomba apewe mwili wa Yesu. Kulingana na toleo la Mathayo Yosefu alikuwa mwanafunzi wa Yesu. Ingawa Nikodemo alikuwa kiongozi wa Mafarisayo na Yusefu wa Arimathaya alikuwa mmoja wa Baraza kuu wa Wayahudi, wote wawili ni mfano ya kumtafuta Yesu.

Ishara ya Yesu hekaluni iligusa ndani ya Nikodemo. Ile ilikuwa nafasi kwa kuitafuta nuru kwa sababu labda aliona kwamba maisha yake alikuwa kama usiku na giza. Katika sehemu ya mwisho ya kifungu hiki cha injili jambo hili la usiku/giza linatumika kama ishara ya upinzani dhidi ya pendekezo la Yesu aliye nuru ya dunia na kumwita kila mtu aje kwenye nuru ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu. Ni tabia ya mwinjilisti Yohane mwenyewe kusisitiza kuhusu tofauti kati ya baadhi ya maneno kama haya, mfano, giza na mwanga ama usiku na asubuhi/mapambazuko ama mbingu na dunia, akionyesha haja hali ya Mungu katika hali yetu.

Yesu alijali tukio la nyoka ambaye Musa alimwinua jangwani kama mfano ya kuinua kwake kwa njia ya msalaba ili kila mtu awe na uzima wa milele. Kazi ya wokovu wa ulimwengu ni kazi ya upendo mno wa Mungu ambaye “aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee”. Hii ni sehemu ya msingi wa andiko hili. Ndio upendo maana ya ishara ya Baba akimtoa Mwana wake kwa ajili ya wokovu wetu. Basi, hatuwezi kutafakari jambo la msalaba peke yake bali kama maonyesho na matokeo ya maisha mazima yalitolewa kwa upendo. Tena kwa sababu ya upendo baada ya msalaba tuko na ushindi wa uzima juu ya mauti. Imani katika Yesu inatufanya kuonja uzima wa milele kwa kutarajia wakati tuko bado duniani. Kwa hivyo misalaba sio aibu kama Wayahudi walivyofikiri wala wazimu kama walivyofikiri Wapagani bali ni kutukuzwa kwa Kristo na wokovu wetu.

Mwendo wa kutukuzwa kwa Kristo unaifuata njia ya kuwa tupu na kujinyenyekeza. Tunaweza kukuta maoni hayo katika waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Wafilipi (Fil 2, 5-9a): “Yeye ingawa alikuwa sawa na Mungu, hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya si kitu, akajifanya sawa na mtumwa, akazaliwa katika umbo la mwanadamu. Naye akiwa na umbo la mwanadamu,  alijinyenyekeza hata mauti, naam, mauti ya msalaba! Kwa hiyo, Mungu alimtukuza sana”. Kwa hivyo tuko na tumaini. Mateso na mauti hayana neno la mwisho wala hayawezi kuyatawala maisha yetu. Hivyo, hatuwezi kutafakari msalaba bila ufufuko. Ndio upendo ambao unaimarisha Yesu kwa kujisalimisha kwake. Ni kwa sababu ya upendo wanafunzi wake wataendelea kazi yake na kujitolea kama vile yeye. Ni kwa sababu ya upendo sisi sote kama Wakristo tunaweza kuishi maisha mapya na kutangaza kwa furaha ukaribu wa Mungu na mambo makuu ambayo yeye anaendelea kutenda kwa ajili ya wokovu wetu. Tuwe macho kwa ishara ya upendo wa Mungu katika hali yetu na kupatikana kama Nikodemo kwa kukutana nawe na kubadilisha mawazo yetu na njia yetu ya kuishi.

Fr Ndega

Nenhum comentário: