sábado, 17 de fevereiro de 2018

UAMINIFU KWA MPANGO WA MUNGU


Kutafakari kutoka Mw 9: 8-15; 1Pt 3: 18-22; Mk 1: 12-15

Sisi Wakristo tumeanza safari yetu ya toba inayoitwa Kwaresima. Kwaresima ni siku arobaini za maandalizi kwa adhimisho la fumbo la Pasaka ya Kristo. Wakati wa kwaresima unalenga kuwa uzoefu wa jangwa. Kwa upande wa viongozi wengi katika biblia jangwa palikuwa mahali maalum pa mkutano na Mungu na uzoefu wa utakaso na uamuzi. Walitafuta mahali huko kabla ya matukio muhimu maishani mwao ili waweze kuchukua kazi yao kwa nguvu na uaminifu. Ndivyo hivyo Kwaresima kama maandalizi ya tukio muhimu sana la imani yetu, yaani Ufufuko wa Yesu.
Wakati huu unatukumbusha pia siku arobaini ambazo Musa alibaki milimani Sinai ili azipokee Amri Kumi; na tena miaka arobaini ya utakaso wa Wana wa Israeli jangwani; tena siku arobaini za Eliya akitembea mpaka milima Horebi ili akutane na Mungu na kuyapokea maelekezo ya kazi yake kama nabii. Lakini tunataka kuwaelekea uzoefu wa siku arobaini ambao Yesu aliishi huko jangwani kabla ya kwanza kazi yake. Yeye ni mfano wetu wa uaminifu kwa mpango wa Mungu.
Maandiko haya yatualika kutafakari kuhusu uaminifu wa Mungu ulioonyeshwa kupitia maneno yake juu ya Agano. Kupitia Nuhu na familia yake Mungu alifanya agano la kwanza na ubinadamu na uumbaji mzima. Kupitia Agano Mungu anadhihirisha kwamba hataki kuharibu kazi ya mikono yake. Ndiyo tamani yake tuweze kuishi kwa njia mpya uhusiano nawe ili tuishi vizuri uhusiano wetu na viumbe vingine vyote vilivyo hai kwa sababu maisha yetu na uzuri wa uumbaji ni maonyesho ya wema na ukarimu wake. Kwa hivyo anataka tuchukue kwa hamu nafasi ambazo anatupa kwa ajili ya utakaso na toba. Tena hiki ndiko moja kati ya maandiko ya msingi wa ubatizo wetu kwa sababu ndio mfano wa uumbaji mpya ambao Kristo anatufanya kuishi. Katika somo la pili, Mtakatifu Petro anaongea kuhusu athari ya gharika kwa uumbaji kama mfano wa maisha mapya ambayo tunapokea kutoka Kristo kwa kupitia ubatizo.
Katika injili, Yesu aliongozwa na nguvu ya Roho Mtakatifu jangwani. Kama jangwa ni mahali pazuri pa uzoefu wa Mungu, Yesu alienda huko kwa sababu alitaka kutambua kwa ndani mpango wa Mungu. Uzoefu huu ulimwimarisha sana ili aanze kazi yake aliyomkabidhi Baba yake. Uwepo wa wanyama wa mwitu na malaika ambao walimtumikia wanaongea kuhusu utambulisho wa Yesu; ndiyo katika yeye uumbaji wote unapata maelewano na kuwa mpya.
Jangwa ni pia mahali pa kujaribiwa kwa sababu lengo la mshawishi ndilo kumjaribu Yesu apendelee njia nyingine tofauti na ile ya Mungu akikanusha utambulisho wake kama Masihi mtumishi. Mwinjilisti Marko haelezi aina ya majaribio kwa sababu nia yake ndiyo kuongea kwamba Yesu alijaribiwa wakati wa maisha yake yote ya kibinadamu. Ingawa mwinjilisti huyo haongei kuhusu majaribu gani, tunataka kuweka hapa tafakari kidogo kutoka kwa wainjilisti wengine, yaani Mathayo na Luka.
Shetani alimshawishi Yesu atumie uwezo wake kwa manufaa yake binafsi; tena atumie mamlaka badala ya upendo, huruma na utumishi. Tena Yesu alishawishiwa kutafuta kusifiwa badala ya kumtangaza Mungu na Ufalme wake. Majaribu matatu ya Yesu yanamaanisha majaribio yote ambayo yalikuwapo maishani mwake wakati wa kazi yake. Hata hivyo, alipata kushinda majaribu yote kwa sababu akaongozwa na Roho Mtakatifu. Msaada huu na hakika ya utambulisho wake wa kimungu ni maana ya uaminifu wake. Kwa hivyo hakuna kitu ambacho  kiweze kumvuruga kutokana na lengo la maisha yake.
Majaribu ya mali, nguvu na utukufu aliyokabili Yesu hayakumzuia kufanya mapenzi ya Mungu. Kama ilivyotokea naye, mitego ya mshawishi yanatushawishi pia kuacha ahadi yetu katika kanisa/jumuiya ama kutumia nguvu kuliko utumishi ama kuongea kuliko kusikiliza ama kuamuru kuliko kutii ama kudanganya kuliko kusaidia, tena kulazimisha kuliko kupendekeza au kutafuta upendeleo zaidi kuliko kupenda. Kama Yesu hakuwako peke yake, hata sisi hatupambani na mshawishi peke yetu.
Tunaalikwa kujikabidhi zaidi mikononi mwa Yesu na kukubali pendekezo la neno lake linalotualika kwa toba. Majaribu yatakuwako daima lakini, kulingana na Mt. Agustino “Ikiwa katika Kristo tumeshawishiwa, katika yeye tunashinda shetani. Kristo angeweza kumtupa mshawishi mbali sana nawe; lakini ikiwa yeye hakuwa ameshawishiwa hangetufundisha jinsi ya kushinda juu ya majaribu.” Mfano wa Yesu wa uaminifu kwa Mungu ndio mwaliko wa uaminifu wetu. yeyote ambaye anazifuata nyayo zake na kufunguliwa kwa msaada wa Roho wake anapata kufanya mapenzi ya Mungu kama yeye alivyo. Ushindi wake unafufua tumaini letu la kupata mafanikio katika mapigano yetu dhidi ya kila kitu kinachotuondoa kutokana na mapendekezo ya Mungu na utambulisho wetu kama Wakristo.


Fr Ndega

Nenhum comentário: