sábado, 25 de fevereiro de 2023

MAFUNDISHO YATOKAYO JANGWANI

 

Kutafakari kuhusu Mwanzo 2, 7-9; 3,1-7; Waroma 5, 12-19; Mathayo 4, 1-11



 

 

Binadamu alifanyika kwa mavumbi ya ardhi ili kupokea uhai wa Mungu ndani yake. Pamoja na mahali pazuri pa kuishi, binadamu alipewa pia zawadi zote alizohitaji aishe kwa ushirika na Mungu na kwa maelewano na ardhi iliyo sehemu ya maisha yake. Lakini majaribio ya kutumia zawadi zake kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe yalimwongoza binadamu kuacha ushirika na Mungu na kupanga maisha yake tofauti kabisa na mpango wa Mungu kwake.

Binadamu wa kwanza alipendelea kumtii “nyoka”, aliye mfano wa “yule mwovu,” kuliko kumtii Mungu. Hali hii ilisababisha mauti kwa watu wote. Ndiye Yesu “Adamu mpya na wa kweli” aliyegundua tena mpango Mungu na kushinda uovu akimtii Baba yake. Chaguo lake lilifanya tofauti, yaani, lilikuwa muhimu mno kwa sababu ikawaletea wote uzima.  

Mambo yote ambayo Yesu aliweza kufanya alipata mafanikio kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Ndiye huyo Roho ambaye alimwongoza nyikani na huko pia alijaribiwa na shetani. Kweli Yesu alionyesha ahadi na hali yetu ya kibinadamu. Mfano, yeye alienda jangwani baada ya ubatizo. Ingawa hakuhitaji kubatizwa alikubali uzoefu huu kwa ajili ya mshikamano nasi tulio wenye dhambi na ya kuiheshimu kazi ya Yohane. Vivyo hivyo, alikubali kushawishiwa jangwani.

Kupitia uzoefu huu, Yesu anatuonyesha kwamba “baada ya ubatizo majaribio mengi yanatujia.” Kwa upande wake, ingawa alijaribiwa jangwani, “alichagua kubaki mwaminifu kwa Mungu.” Kila mtu anakabiliana na njia mbili ya kufuata na kupaswa kuchagua moja tu ili kufanya mapenzi ya Mungu. Ndiye Yesu mfano wa chaguo kamili. Yeye alijua wazi sana kwamba ndiye Mwana wa Mungu aliyekuja duniani si kwa ajili ya kufanya mapenzi yake mwenywe bali ya Baba.

Katika uzoefu wake wa jangwa, Yesu alifunga kwa siku arobaini na akaona njaa. Arobaini ni namba ya mfano iliyomaanisha “muda mrefu.” Kabla ya Yesu tuko na baadhi ya mifano ya Viongozi wa kibiblia ambao, kabla ya kuchukua kazi ya kuwaongoza watu ama kabla ya tukio muhimu, waliruhusu kuongozwa jangwani na kubaki bila kula chakula wakati wa muda mrefu ili waweze kujiandaa wenywe vizuri kwa ajili ya kazi aliyowakabidhi Mungu.

Tukumbuke ile muda ya siku arobaini ambayo Musa alibaki mlimani Sinai ili azipokee Amri Kumi; na pia siku arobaini wa Eliya akitembea mpaka mlima Horeb ili akutane na Mungu na kupokea kutoka kwake maelekezo ya kazi yake kama nabii. Namba arobaini inatumika pia kwa ajili ya kuongea kuhusu kiasi ya miaka ambayo Waisraeli walibaki jangwani kabla ya kuingia katika nchi ya ahadi. Kwa watu hawa wakati huu ulikuwa wa utakaso na kukomaa kulingana na ufundishaji wa Mungu. Lakini hawakuwa na uaminifu kama Yesu alivyo.

Uzoefu jangwani ni maalum kwa ajili ya upweke, utakaso na kukomaa. Lakini jangwa ni pia maisha yetu ya kawaida ambapo tumeongozwa na Roho Mtakatifu, lakini pia tunajaribiwa kukata tamaa kwa sababu ya majaribio ya yule mwovu, kama ilivyotokea na Yesu. Mshawishi alianza kutoka mambo madogo akichukua nafasi ya kosa la nguvu mwilini mwa Yesu kwa sababu ya kufunga. Matarajio yote yalikuwa dhidi ya namna ya utume wa masihi ambao Yesu alichagua.

 Yesu alishawishiwa kutumia uwezo wake kwa manufaa ya kibinafsi badala ya kwa ajili ya upendo, ya huruma na ya kuwahudumia wengine. Tena Yesu alishawishiwa kujisifa mwenyewe badala ya kumtangaza Mungu na Ufalme wake. Majaribu matatu ya Yesu yamaanisha majaribio yote ambayo yalikuwapo maishani mwake nyakati zote za kazi yake. Hata hivyo, alipata kushinda yote kwa sababu akaongozwa na Roho Mtakatifu na kuwa mtiifu kwa Baba yake.

Majaribu ya mali, nguvu na utukufu Yesu aliyokabiliana nayo hayakumzuia kufanya mapenzi ya Mungu. Kama ilivyotokea na Yesu, na Adam na Waisraeli, sisi pia tunashawishiwa kuishi bila kumwamini Mungu. Mitego ya mshawishi inatuongoza kupendelea kutumia mamlaka kuliko utumishi, kuamuru kuliko kutii, kudanganya kuliko kusaidia, kulazimisha kuliko kupendekeza, kutafuta upendeleo kuliko kupenda, kuwa wanafiki kuliko kuwa binadamu wa kweli.

Kama Yesu amekwisha kumshinda adui ya Mungu, ndilo chaguo lake msukumo ili chaguzi zetu ziweze kufanya tofauti, yaani kuwa muhimu sana. Kulingana na Mt. Agustino “Ikiwa katika Kristo tumeshawishiwa, katika yeye tutamshinda shetani. Kristo angeweza kumtupa mshawishi mbali sana naye; lakini ikiwa yeye hangalikuwa ameshawishiwa hangetufundisha jinsi ya kushinda juu ya majaribu.” Kweli yeyote ambaye anaufuata mfano wake wa kumtii Baba na kufunguliwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu anapata kufanya mapenzi ya Mungu na kushinda majaribio yote.


Fr Ndega

segunda-feira, 20 de fevereiro de 2023

WAKATI MWAFAKA UMEANZA

 

Kutafakari kutoka  Yoe 2, 12-18; 2Kor 5, 20-6:2 Mt 6, 1-6; 16-18




 

    Kupitia sherehe hii ya Majivu tumeanza wakati wa kwaresima. Kwaresima ni siku arobaini za maandalizi kwa adhimisho la fumbo la Pasaka ya Kristo. Wakati huu unatukumbusha siku arobaini ambazo Musa alibaki milimani Sinai; pia miaka arobaini ya Wana wa Israeli jangwani; tena siku arobaini za Eliya akitembea mpaka milima Horebi na siku arobaini za Yesu jangwani aliyeongozwa na Roho Mtakatifu.

    Wakati wa kwaresima unalenga kuwa uzoefu wa jangwa. Kwa upande wa viongozi wengi katika biblia jangwa palikuwa mahali pa mkutano na Mungu kwa hamu na uzoefu wa utakaso. Walitafuta mahali huko kabla ya matukio muhimu maishani mwao ili waweze kuchukua ahadi kwa nguvu na uaminifu. Vivyo hivyo, ni Kwaresma kama maandalizi kwa tukio muhimu sana la imani yetu, yaani Ufufuko wa Yesu.   

    Huu ni wakati kwa kutafakari kwa njia ya ndani kuhusu huruma ya Mungu na hali yetu ya wenye dhambi. Dhamiri kuhusu matokeo ya dhambi katika maisha yetu inatuongoza kumwomba Mungu kulingana na somo la kwanza, yaani “Wahurumie watu wako ee Bwana!” nasi tunajua kwamba Mungu anawahurumia watu wake sio kwa sababu tunastahili, lakini kwa sababu hii ni tabia yake ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa rehema.

    Kulingana na Baba Mtakatifu Francisco, “Mbele ya hali kubwa ya dhambi, Mungu anajibu kwa msamaha kamili. Huruma itakuwa daima kubwa kuliko dhambi yoyote, na hakuna awezaye kuuwekea mipaka upendo wa Mungu anayesamehe daima.” Kwa hivyo tunaalikwa kumrudia yeye kwa imani kubwa na kuutumainia wokovu wake.

    Somo la pili linaongea kuhusu mahitaji ya upatanisho na Mungu kwa sababu yeye mwenyewe anatupa nafasi ya kufanya hivyo kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo. Huu ni wakati wa neema, nasi hatuwezi kuipokea neema ya Mungu bure. Hebo tuonyeshe tabia ya toba kutoka ndani! Tubuni na kuiamini injili”, asema Yesu. Wakati wa mabadiliko na wa wokovu ndio sasa.

    Katika dini ya kiyahudi, kuna hatua tatu muhimu sana ambazo zinadhihirisha utambulisho wa myahudi wa kweli, yaani sala, sadaka (itolewayo kwa maskini) na kufunga. Hasa wakati huu wa kwaresima tunaalikwa kuchukua hali hizi kama ishara ya toba yetu. Yesu alipopendekeza hatua hizi tatu, yeye aliwakumbusha wafuasi wake kuhusu tabia ya roho ambayo inapaswa kutoa maana kwa hatua hizi. Wakati wa Yesu, kufunga kulikuwa shughuli ya kawaida, naye pia alifunga kwa wakati wa siku arobaini jangwani kabla ya kuanza ujumbe wake kwa umma.

    Yesu alitaka kwamba wanafunzi watende kwa tabia ya kweli sio kama ile ya baadhi ya watu (wanafiki) ambao walipofunga wakaonyesha huzuni ili wapate kuonekana kwa watu kuwa wanafunga. Yesu alitokubali tabia hii na kusema kwamba wamekwisha pata tuzo lao. Kufunga kwetu tulio Wakristo ni tabia ya toba na ya ushirikiano na Kristo ambaye alifunga kwa siku arobaini na baadaye aliteseka kwa ajili yetu. Mtakatifu Agostino alisema kwamba “kufunga kwetu ni halali ikiwa kunachoma ndani yetu tamaa ya kumwona Kristo”. Kufunga kunalenga kutusaidia kujinyima wenyewe ili tuwe watu bora. Tunaweza kueneza ujumbe huu hasa kwa ajili ya kufunga baadhi ya maneno, ya matendo na ya mawazo ambayo si mazuri katika uhusiano wetu na wengine.  

    Kuhusu sala, ni vizuri pia kuufuata mfano wa Bwana wetu. Yeye alikuwa mtu wa sala na aliijulisha sala kama njia kamili ya kuwa mwaminifu kwa mpango wa Mungu. Sala yake ilikuwa maonyesho ya uhusiano wa ndani na Baba na mwaliko ili wanafunzi wake wafanye vivyo hivyo kama utambulisho naye. Kwaresima ni wakati wa sala kwa hamu zaidi, kwa kufungua akili zetu na mioyo yetu kwa tendo la wokovu wa Mungu. Huu ni wakati pia wa kutenda matendo ya huruma kwa wenzetu, kwa kuonyesha juhudi yetu ya kubadilisha hali yetu na kandokando yetu. Majivu usoni ni ishara ya udhaifu yetu na kukubalika kwetu kuhusu mwaliko wa Kanisa wa toba kwa sababu wakati wa kuukaribisha wokovu wa Mungu na kuiamini injili ndio sasa.   


Fr Nega

sábado, 18 de fevereiro de 2023

UPENDO BILA MIPAKA

 

Kutafakari kuhusu Law 19,1-2.17-18; 1Kor 3,16-23; Mt 5,38-48




 

    Uumbaji wa mwanadamu ulikuwa ni tendo la upendo. Wakati Mungu alimwumba alisema: “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu.” Kwa hiyo, tangu asili binadamu ameitwa kutenda kama Mungu alivyo. Kutenda kama Mungu ni kupenda. Ahadi yote ambayo mtu anachukua katika safari yake duniani inapaswa kumwongoza kwenye mwelekeo huo.

    Hivyo, tunaweza kuelewa sababu ya agizo la sheria katika Agano la Kale linalosema, “Muwe watakatifu kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.” Sheria hii ni njia ya utakatifu kwa Wayahudi. Kwa sababu ya utakatifu wa Mungu, watu ambao wamechaguliwa naye wameitwa kuwa watakatifu, na njia ya kufikia lengo hili ni “kumpenda jirani yao kama nafsi yao wenyewe.” Matarajio ya Mungu ni kwamba waweze kutenda kama yeye alivyo.

    Andiko la pili linatuambia kwamba Yesu ametupa Roho wake naye huyo Roho anaishi ndani yetu. Hivyo maisha yetu yamekuwa hekalu la Mungu. Hii inathibitisha wito wetu wa kuwa watakatifu, kulingana na mpango wa Mungu tangu mwanzo. Uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu ni msaada ili matendo yetu yawe matakatifu.

    Mafundisho ya Yesu yanalenga kuzaa uhusiano mpya kati ya watu na Mungu na kati ya watu wenyewe. Yeye anaonyesha kuwa ukamilifu wa Baba ni msukumo wa ukamilifu wa wana wake. Hili si jambo lisilowezekana, bali Yesu mwenyewe anajulisha, hatua kwa hatua, jinsi ya kumkaribia Mungu hata jinsi ya kuishi kama yeye aliyejaa upendo na ukarimu.

    Maneno haya “jicho kwa jicho na jino kwa jino” ambayo Yesu aliyataja, inaitwa “Sheria ya Talioni”. Sheria hii haikulenga kuwa msukumo kwa ajili ya ukatili ama wa kisasi, bali “ilikusudiwa kuzuia kulipiza kisasi, na hivyo kumlinda mtu aliyefanya kosa asipewe adhabu kubwa kuliko uzito wa kosa lenyewe.” Kweli sheria hii ilizaliwa kwa sababu “mara nyingi adhabu ilikuwa kubwa kuliko kosa.” Hata hivyo, njia hii iliyofundisha na Sheria hii haikuonyesha mapenzi ya Mungu, ambaye aliagiza “wampende jirani kama nafsi yao.”

    Kama nia ya Yesu ni kugundua tena mpango wa Mungu wa kiasili, anataka kuwafundisha watu kwa njia tofauti. Yeye hawalazimishi wasikilizaji wake kuchukua ahadi hii, bali ili waweze kumfuata kwa kweli kuna masharti. Wakati watu wengine wanapenda tu wale wanaowapenda wao, kwa upande wa wanafunzi wa Yesu ni masharti kuwapenda hata maadui zao na kuwatendea mema wale wanaowachukia. Huu ni upendo bila mipaka ulio tabia ya upendo wa Kikristo. Lengo la jambo hili ni tuwe watoto wa Mungu ambaye anazitoa zawadi zake kwa wale walio wema na kwa wabaya. Anafanya hivyo kwa sababu ni tabia yake na kwa sababu anataka tujifunze kutoka kwake. Ingawa hatustahili zawadi zake, hatuwezi kuweka mipaka katika ukarimu wake.

    Mwanafunzi wa kweli wa Yesu “hashindani na mtu mwovu”, bali anatoa “shavu tofauti la maisha” na njia tofauti ya kutenda. Hii inamaanisha kumpa mwingine nafasi ya kufikiri vizuri na kubadilisha matendo yake. Mafundisho ya Yesu yanatuimarisha kutumia wema wa moyo na matendo mema kwa kumwombea mtu mwovu. Kwa msaada wa Mungu tunaweza kuibadilisha hali ya uovu kwa sababu yeye mwenyewe ana mazoea ya kubadilisha hali mbaya kuwa hali nzuri na hali ya mauti kuwa hali ya uzima. Kifo cha Mwanae kilikuwa tendo baya la wanadamu, lakini yeye alibadilisha hali hii mbaya kuwa ni manufaa ya wokovu wetu. ushuhuda wazi sana ya hili ni wakati Yesu alipokuwa msalabani akiteswa na maadui wake, akawaombea msamaha kwa Mungu Baba. Pia aliwatetea kuwa hawakujua walilolifanya.

    Kutokana na mfano wa Kristo, anayeitwa pia “nabii asiye na ukatili”, njia ya kipekee ya kuushinda ukatili ni kujibu kwa ishara za amani. Yesu anataka kwamba tabia zetu zishinde mwelekeo wa kijamii kwenye kisasi, ukatili na ukabila. Ukabila unauharibu undugu na kuukanusha utambulisho wetu wa Kikristo. Kulingana na Baba Mtakatifu Francisco, “kipimo cha utambulisho wetu kama watoto wa Mungu ni tabia ya huruma.” Kama wafuasi wa Yesu sisi sio bora kuliko wengine, lakini tunapaswa kutenda tofauti, yaani kulionyesha “shavu lingine.” “tunapowachukia maadui wetu tunawapa uwezo juu yetu: uwezo juu ya usingizi wetu, hamu yetu ya chakula, shinikizo letu la damu, afya yetu na furaha yetu” (Dale Carnegie). Kwa kifupi, Hatuwezi kuruhusu kuwa waovu waamue jinsi tunavyopaswa kutenda.

    Kuna hadithi fulani inayoongea zaidi kuhusu hayo. “Mwandishi fulani anayeitwa Sydney Harris, anatuambia hadithi ambayo ilitokea alipoandamana na rafiki yake kwa duka la magazeti. Rafiki yake alimsalimia mwanagazeti kwa heshima sana, lakini kama jibu, mtu huyo alimtendea vibaya. Rafiki wa Harris akikubali gazeti lililotupwa kwa njia mbaya kwenye mwelekeo wake, alitabasamu kwa heshima na kutakia wikiendi njema kwa mwanagazeti. Baadaye,  walipotembea njiani, mwandishi alimwuliza rafiki yake, akisema, “Mtu huyo ana tabia mbaya kwako daima?” “Ndiyo, kwa bahati mbaya, yeye alivyo.” Na wewe una tabia ya heshima na ya kirafiki kwake daima?” “Ndiyo, mimi ndivyo.” “Kwa nini wewe ni mtu mwema mno kwake ikiwa yeye ana tabia mbaya kwako?” “Kwa sababu sitaki kwamba aamue jinsi ninavyopaswa kutenda.”

    Ndiye Yesu mwenyewe ambaye anatualika kutenda vivyo hivyo. Kulingana naye, uovu hauwezi kuondoa uovu, bali ni wema tu unaoweza kufanya hivyo. Tupendane kama Yesu alivyo na, kwa njia ya upendo huu, tuweze kuijenga jamii inayotarajiwa na Mungu kwa watoto wake.

 

 Fr Ndega