Kutafakari kutoka Yer 20, 7-9; Mt 16,
21-27
Ujumbe wa
masomo haya unatuimarisha sana kwa sababu ingawa sio rahisi kufanya kazi kwa
ajili ya watu wa Mungu, lakini ndiyo nzuri. Uaminifu wa Mungu ndio maana ya
uvumilivu wetu tulio watumishi wake. Ikiwa tunapata kufanya mapenzi yake tuko
na uhakika kwamba tutakuwa washindi wakati wa mazingira magumu katika safari
yetu. Huu ndio uzoefu wa Yeremia. Yeye ndiye nabii aliyeteseka kwa sababu ya
uaminifu wake kwa Yule aliyemwita awe nabii. Yeye aliishi wakati wa mgogoro
katika kazi yake kwa sababu ya upinzani dhidi ya maneno yake na hatari kwa
maisha yake. Alikuwa karibu ya kukata tamaa kwa sababu ilionekana kwamba
alifanya kazi bure, yaani bila maana, lakini uhusiano alioishi na Mungu ulimwimarisha
kusimama mwaminifu na mshindi. Upendo wa Mungu kwa Yeremia ndio kama moto
inayochoma ndani yake na kuizaa hamu kwa ajili ya Mungu.
Andiko la
injili ni mwendelezo wa lile ambalo Yesu aliwauliza wanafunzi kuhusu
utambulisho wake kulingana na mtazamo wa watu. Majibu yalikuwa ishara ya kwamba
mawazo kuhusu Yesu hayakuwa wazi sana kwa upande wa watu. Lakini Yesu alitaka
kujua jambo hili kwa upande wa wanafunzi wake, kwa sababu kwa Yesu si muhimu
yale ambayo watu wanafikiri, bali muhimu ni kukiri kwa wafuasi wake. Petro alisema
yale ambayo wanafunzi wengine kumi na mmoja walijua pia, yaani Yesu ni Masiya wa
Mungu. Lakini yeye aliwakataza ili watangaze habari hii kwa sababu ya kutokuwa
na maana kamili. Yesu alitambua kwamba wafuasi wake wakahitaji ufunuo zaidi na
kujifunza vizuri maana ya Masihi yake na masharti kwa kumfuata kwa kweli.
Ni jambo
la ajabu kwamba yule Simoni aliyeruhusu kuongozwa na msukumo wa Mungu na kuwa Petro
aliye mfano wa umoja wa Kanisa, tena kwa haraka aliruhusu kuongozwa na shetani.
Hilo linamaanisha kwamba ingawa wanafunzi wa Yesu wanaongozwa na Mungu, kuna
nguvu za ndani ambazo zinawaongoza kumpinga Mungu. Kweli mawazo ya wafuasi wa
Yesu kuhusu Masiya yalifuata matarajio ya Wayahudi wengine, yaani, masiya wa
kisiasa atakayetumia nguvu zake za kimungu ili kuwakomboa Wayahudi toka ukoloni
wa Warumi. Bila shaka Yesu aliyakanusha mawazo hayo akionyesha njia tofauti ya
kutimiza ujumbe wake wa Masiya, yaani kupitia mateso, kifo na kufufuka. Uamuzi
wa Yesu ni kulingana na mpango wa upendo wa Baba yake aliyeupenda ulimwengu mno
hata alimtoa Mwana wa pekee ili kila mtu asipotee bali awe na uzima wa milele.
Basi, kumfuata Yesu kupitia njia aliyochagua ni kutenda kulingana na mapenzi ya
Mungu.
Wanafunzi
wa kwanza walihitaji mwendo mrefu ili kujifunza kumhusu Yesu na kuyafahamu
mapendekezo yake sawasawa. Kidogo kidogo walitambua kwamba kwa kujitoa kama Yesu
alivyo, walipaswa kuzifuata hatua tatu, yaani, kujikana wenyewe, kuichukua misalaba
yao na kumfuata Yesu. Kwa maneno mengine, walipaswa kubadilisha njia yao ya
kuishi na kufikiri. Hivyo, wale ambao hukutana na Yesu hawabaki walivyo wala hawawezi
kumdai Yesu atende kulingana na njia yao ya kufikiri. Mwendo unapaswa kuwa
tofauti. Mawazo ya Yesu ni tofauti na mwelekeo wa ulimwengu, yaani mtu
anayetaka kuwa wa kwanza anapaswa kuwa wa mwisho; tena ikiwa anataka kuwa
mkubwa anapaswa kuwa mtumishi wa wote; tena ikiwa anataka kuiokoa nafsi yake
anapaswa kujitoa kwa ajili ya Kristo na injili. Kwa maneno mengine, kulingana
na Yesu, ni lazima kufa kwa kuishi.
Basi, ili
tuwe wanafunzi wa kweli tunapaswa kupitia kwa mwendo wa kufa kwa nafsi yetu
kila siku. Kwa kumfuata Yesu kwa kweli tunapaswa kupatikana kwa kila kitu katika
jumuiya zetu. Tunapaswa kufanana maisha yetu kulingana na njia ya Yesu ya
kuishi. Hali hii haileti upendeleo au hadhi, bali mateso na kujisalimisha kwa
ajili yake. Yeyote anayetaka kuishi bila ahadi hawezi kumfuata Yesu. Mtu anayetamani
kumfuata Kristo bila msalaba hatamfuata kweli kamwe. Tujiulize kidogo, Je, ni
Kristo gani tumemfuata? Mawazo au kitu gani tunahitaji kujinyima bado ili
tuweze kumfuata Yesu kabisa? Ujumbe huu utuimarishe kumfuata Yesu kwa uaminifu,
yaani kulingana na njia aliyochagua ili mapenzi ya Mungu yafanyike.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário