Tafakari ya Mt 17, 1-9
Siku sita baada ya kuwasilisha masharti ya
kumfuata, Yesu aliwaalika wanafunzi wake kupanda mlimani. Jambo la Mlima ni
muhimu sana katika Injili ya Mathayo. Mwinjilisti huyo anaandika kwa Wayahudi
na kwa hivyo, nia yake ni daima kumjulisha Yesu kama Musa mpya. Mlima katika
Biblia ni mahali pazuri kwa ajili ya uzoefu wa Mungu. Hasa katika injili hii
mlima unatajwa sana kwa sababu ni rejeo katika matukio makubwa ya maisha na utume
wa Yesu. Tangu mwanzo wa maisha ya umma mpaka kupaa kwake, Mathayo anaongea
kuhusu milima 7. Namba 7 inatusaidia kuelewa umuhimu wa mahali huko katika
uzoefu wa ufunuo wa Yesu kama Mwana mpendwa wa Mungu.
Tunataka kwa kifupi kukumbuka kidogo matukio
ya milima hii 7 kwa kusisitiza yale ambayo tumesema, yaani Mlima wa majaribu - wakati wa majaribu, Yesu aliletwa kwenye mlima
juu sana ambapo yeye alithibitisha uaminifu wake kwa mpango wa Baba (Mt 4,8s). Mlima wa Heri nane – Yesu alienda
mlimani wakati alipotangaza kwa mara ya kwanza Ufalme wa Mungu (Mt 5). Mlima ya maombi - baada ya kuzidisha mikate
na samaki kwa mara ya kwanza, yeye alipanda mlimani peke yake ili kusali
(14:23). Mlima vya kuzidisha mikate –
hali hii inatukumbusha tukio la Heri, yaani, Yesu alipanda mlimani na huko
aliketi; umati mkubwa ukakusanyika karibu naye (15,29s). Mlima wa Golgotha (27), Mlima
wa kupaa mbinguni (28) na katika sura ya 17 tuko na Mlima wa Kugeuka sura.
Kisha, Yesu aliamua kuchukua baadhi ya
wanafunzi na kwenda pamoja kwenye mlima mrefu. Kulingana na desturi ya
Kikristo, mlima huu unaitwa Tabor. Huko mlimani Yesu aligeuka sura mbele yao.
Hakika Yeye alikuwa kama kawaida lakini uzoefu huu ulibadilisha mtazamo wao
kuhusu mwalimu. Yesu aliwaonyesha kidogo utukufu wake na hali ijayo ya maisha
ya wale wanaomfuata kwa uaminifu. Yesu aliwaalika kwa uzoefu wa juu ili waone
kwa mtazamo wa juu na kuweza kuona vizuri hali ya kujisalimisha kwake na hali
wanayoalikwa kuichukua kama ahadi na Mwalimu wao.
Uwepo wa Musa na Elia unaeleza kuhusu rejeo la
ufunuo katika Agano la Kale. Wote wawili waliongea na Yesu wakionyesha kwamba
hakuna kupasuka kati ya mafundisho yao na yale ya Yesu, bali uhusiano na
mwendelezo. Lakini kulingana na sauti iliyosikika kutoka kwenye wingu ndiye
yeye kwa uwezo wa kufundisha na kutafsiri kamili yale yaliyosemwa na mababu wa
zamani. Baba alishuhudia kuhusu Mwana wake, akimweka kama rejeo la maisha yetu,
yaani, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni”. Wote wanaalikwa kumsikiliza.
Kusikiliza katika Biblia ni kitenzi chenye nguvu sana. Hii ni tabia kamili ya
Myahudi mbele ya Neno la Mungu, akifanya mazoezi kuhusu yale aliyosikia. Basi,
kusikiliza kuna uhusiano wa ndani na kushika/kutenda.
Yesu ni ufunuo wa kipekee wa Mungu. Hakuna
mwingine ambaye aweze kumdhihirisha Mungu kama Yesu alivyo. Kweli Mungu
aliongea wakati wa zamani kwa mababu zetu. Lakini “siku hizi” mambo yote Mungu
anayoendelea kudhihirisha kwa watu anafanya kwa Mwanawe Yesu. Hata wale ambao
hawamjui Yesu wanapokea ufunuo wa Mungu kwa njia yake. Katika kila ndugu ambaye
wanamsaidia wanaweza kukutana na Kristo ambaye alijitambulisha na walio na
mahitaji mengi (cf. Mt 25,31-46). Kipimo ni upendo/huruma. Matendo yao ya
huruma yanaongelea Kristo.
Wanafunzi “wanatamani kubaki mlimani, lakini
sauti inatoka mbinguni ikiwaalika kumsikiliza na kumtii Yesu.” Mara nyingi
Mungu anatualika kufanya uzoefu wa uwepo wake kama ilivyotokea kwa wale kwenye
mlima, mfano, wakati tunaposhiriki katika sherehe fulani ama siku za maombi na
kadhalika. Uzoefu kama huu unaiimarisha imani yetu na hamu yetu kwa ajili ya
kazi ya Mungu. Kwa kawaida tunataka uzoefu huu uwe wa muda mrefu. Lakini safari
yetu yapaswa kutendeka kati ya “kupanda mlimani” (mfano wa uzoefu wa Mungu wa
kibinafsi) na “kushuka milimani” (mfano wa changamoto za undugu na kazi). Kila
siku tunaalikwa kufanya uzoefu wa “kugeuka sura” kwa kusikiliza Neno la Yesu na
kufanya mazoezi kuhusu Neno hili. Uzoefu huu unatusaidia kutambua nyuso za
baadhi ya ndugu wengi kandokando yetu na kuona hisia na tabia za Kristo kwa ajili
yao. “Kusikiliza neno lake kunatupatia nguvu ya kumfuata mpaka mwisho.” Hii ni
njia kamili ili tuwe pia “wana wapendwa” wa Mungu.
Fr Ndega
Mapitio ya kiswahili: Christine Githui
Nenhum comentário:
Postar um comentário