Kutafakari kuhusu Is 56,
1.6-7; Rom 11,13-15.29-32; Mt 15, 21-28
Mungu anataka
kuongoza njia ya mataifa kwa “nyumba” yake, yaani kwake mwenyewe. Yeye
anawapenda wote na kutaka kuokoa wote. Yeye sio Mungu wa Israeli peke yake na
hata Watu hawa walichaguliwa sio kwao wenyewe bali ili wawe chombo cha wokovu
Mungu aliopanga kwa wote. Wokovu ni zawadi ya Mungu na hakuna mtu hata mmoja
anayestahili zawadi hii. Mungu mwenyewe anawavutia watu kwake kwa sababu ya
wema wake, lakini kipimo cha jibu kamili kwa mwaliko wake ni upendo na haki.
Ndiye Mungu huyo ambaye Mt. Paulo anatangaza kama Mungu wa huruma kwa wote. Kupitia
kazi hasa ya mtume huyo wale waliofikiriwa wa nge wa huruma hii wana nafasi ya
kuionja vizuri. Ndio watu hawa ambao watawasaidia wale waliochaguliwa kwanza.
Mathayo anasema
kwamba Yesu alienda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni. Zote hizi mbili ni
wilaya ya Ugiriki, yaani ndiyo maeneo ya wasio Wayahudi. Yesu aliruhusu
kuongozwa ili kukutana na watu wa nge wa Israeli. Mama mmoja alimjia Yeye na kupaza
sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo.”
Mama huyo anaongea na Yesu kuhusu jambo la thamani kubwa mno maishani mwake,
yaani, binti yake. Lakini mama huyo hapashi habari tu kuhusu binti yake, bali
alimtambua Yesu kama Mwana wa Daudi na Bwana. Huyo mama Asiye Myahudi, hata
anaweza kufundisha ‘watu’ wa Yesu mwenyewe jinsi ya kumkaribisha vizuri na
kumwamini yeye. Basi, Yesu alifanya muujiza sio kwa sababu ya mahitaji ya mama
huyo tu, bali hasa kwa sababu ya imani yake kubwa. Kama hitimisho tuko na
ushindi wa imani.
Majibu ya Yesu
yalikuwa maneno magumu na mazito, yaani, “sikutumwa ila kwa watu wa Israeli
waliopotea kama kondoo”; na jimbo lingine, yaani “si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Kweli
ni ngumu kukubali na kufahamu kwamba maneno haya yatoke midomoni mwa Yesu kwa
sababu tunajua kuhusu hisia zake mbele ya hali ya walio na mahitaji. Tunapaswa
kufahamu kwamba andiko hili linatafsiri mtazamo wa Wayahudi kuhusu wokovu kama
upendeleo wa baadhi ya watu. Hasa kati ya Wayahudi sio wote waliostahili
kuokolewa. Yesu ndiye Myahudi lakini alitenda tofauti akikubali mwendo wa
‘kujifunza’ kuhusu lengo la kazi yake. Yeye aliruhusu kuongozwa na Roho kwenye
Tiro na Sidoni na kila mkutano na watu ilikuwa nafasi ya kujifunza.
Hasa kuhusu
wanawake, Injili zote zinaongea juu ya uhusiano wa Yesu nao kama urafiki
maalum. Hao waliandamana naye kutoka mwanzo mpaka mwisho wa maisha yake katika
hali ya kibinadamu. Tukumbuke kwamba ndiye mwanamke mmoja (mamaye) aliyemwimarisha
kuanza ufunuo wa Saa yake. Katika kifungu cha leo ndiye mwanamke mmoja (mgeni)
aliyemwimarisha kuanza ufunuo wa utambulisho wake zaidi ya mipaka ya Israeli.
Ndiye mwanamke mmoja (Magdalena) aliyekuwa wa kwanza wa kupokea habari ya
maisha mapya ya ufufuko wake na jukumu la kuitangaza kwa wengine. Mtazamo wake
na ishara zake za upendo kwenye wanawake zinawaimarisha kushinda hali ya dharau
na ubaguzi katika jamii. Uhusiano wake nao unawahakikishia maisha mapya.
Hali hii
inadhihirisha kwamba Yesu sio mali ya Wayahudi. Kazi yake ni kwa wote kwa
sababu alikuja kutimiza mapenzi ya Mungu anayetaka kuwaokoa watoto wake wote. Ingawa
tunafikiria kwamba “tumeokolewa” na kufikiri kwamba maisha yetu yanampendeza
Mungu, tunapaswa kuwa macho kwa sababu labda Mungu hana nafasi bado katika
maamuzi yetu ya kila siku. Yesu anatufundisha njia ya kukutana na wengine na hata
kushangazwa kuona imani yao kubwa. Kila wakati tunaalikwa kutambua kwamba imani
haina mipaka na tena wakati tunakutana na wale wanao imani tofauti na yetu sisi
tuko na nafasi ya kujifunza zaidi na kuimarishwa katika imani yetu. Mwendo huu
unawezekana kwa sababu ni sehemu ya utambulisho wetu kama Wakristo kujifunza na
kukua pamoja na wengine. Hatuwezi kusahau kwamba hata mwanamke wa injili ya leo
anatufundisha sana hasa jinsi ya kuongea na Mungu. Kulingana na mfano wa mama
huyo, ukubwa wa imani ya mtu unaonyeshwa na tabia ya uvumilivu na unyenyekevu
kwa kuwaombea wengine kuliko yeye mwenyewe na kuwa na uhakika kuhusu msaada wa
Mungu. Tunataka kumwomba imani hii.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário