domingo, 28 de agosto de 2016

UNYENYEKEVU NA UKARIMU KAMA VIPIMO VYA UHUSIANO WETU


Kutafakari kutoka Luka 14,1.7-14

        Yesu alialikwa kula chakula nyumbani mwa Mfarisayo mmoja na, kwanza kabisa, yeye alisababisha usumbufu kwa sababu alimponya mtu mmoja siku ya Sabato. Sheria ya Wayahudi inakataza hali hii, lakini Yesu anapendelea kuwajali watu kuliko kuifuata sheria ambayo haikufuata tena nia ya Mungu ya asili. Akitarajia waweze kufikiri kama yeye aliwauliza swali: “Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya Sabato?” Lakini wao wakakaa kimya. Tukumbuke kwamba Mafarisayo na Waandishi waliondoa maana ya kinabii ya sheria, wakitafsiri kulingana na mawazo yao ya upungufu. Hao wanapenda sana kujiinua na kupendezwa. Mara nyingi Yesu alipokutana nao hakufikia mafanikio kuhusu mapendekezo yake ya maisha mapya kwa sababu wao ni wanafiki na wanapendelea kumjaribu Yesu kuliko kubadilisha mawazo yao kulingana na matarajio ya Yesu. Kwa hivyo mkutano wa Yesu nao ni maana ya mapambano/mfarakano daima.

     Yesu yupo mloni, karamuni. Injili ya Luka inaonyesha kwamba kushiriki katika milo mbalimbali kulikuwa muhimu sana kwa Yesu aliyetumia vipindi hivi kama nafasi ya kuwafundisha watu. Karamu miongoni mwa Wayahudi inathamini sana. Pamoja na maana ya uzoefu wa familia, kielelezo cha urafiki, mshikamano na hamu ya kukuwa pamoja, karamu pia ni mfano wa uhusiano wa upendo kati ya Mungu na watu wake (Hos 2:1-23, Isa 54:4-8, Eze 16:7-8). Katika mafundisho ya Agano la Kale, kushiriki katika Ufalme wa Mungu, mara nyingi hulinganishwa na kushiriki katika karamu (Isa 34:5-7, Zek 9:15,1 Nya 12:38, Zek 14:15-24). “Karamu za namna hiyo mara nyingi zilikuwa na ujumbe wa kimasiha. Zilisherehekea ushindi wa Mungu dhidi ya nguvu za uovu (Isa 25: 6-8), zikaimarisha uhusiano kati ya Mungu na watu wake, na kuwaunganisha watu kati yao.” Huu ni kweli, mfano kwenye karamu ya arusi. “Upendo wa Mungu ni kama ule wa Bwana arusi, jinsi alivyolipenda na kulichagua Taifa la Israeli kama mali yake mwenyewe. Wakristo wa kwanza, walifikiria pia juu ya uhusiano wao na Kristo kama mfano (Yoh 3:39, 2Kor 11:2, Efe 5:23-32).”

         Basi, katika injili ya leo, Yesu alishangaa kwa sababu ya mashindano ya watu kwa ajili ya mahali pa kwanza katika karamu naye aliwapendekezea tabia tofauti. Kulingana na Yesu tabia ya ukarimu wao kwa ajili ya maskini na wasiojiweza ni njia ya kuonyesha kuwa upendo wa Mungu unatolewa kwa hiari kwa ajili ya watu wote. Kwa maneno mengine, karamu zinapaswa kutafakari upendo wa Mungu kwa wote. Katika karamu ya arusi mbinguni, yeye atawakaribisha wale wanaomwelekea. Katika jamii, kwa kawaida, kutafuta mahali pa kwanza, msimamo, upendeleo, umaarufu, na kadhalika huongezeka sana. Hali hii husababisha mapambano/mfarakano, chuki na ukatili. Hata katika Kanisa na jumuiya zetu tunaweza kukuta hali kama hii. Yesu alikwisha ameonya kuhusu hatari za hali hii na kufundisha unyenyekevu kama njia kamili. Unyenyekevu ni fadhila ambayo inampendeza Mungu na watu. Kuwa mnyenyekevu ni kuchukua hali ya udhaifu ya kibinafsi kushinda mwelekeo wa kuwa bora kuliko wengine. Inamaanisha kuweka vipaji vya kibinafsi kuwatumikia wengine kwa ukarimu na upendo.


        Lengo la Yesu ni kuzaa ubinadamu mpya na aina mpya ya uhusiano miongoni mwa watu. Msingi wa ubinadamu mpya ni unyenyekevu na upendo. Thamani hizi zinapaswa kusaidiwa zaidi miongoni mwetu. Kupitia utumishi wa kindugu na wa kinyenyekevu tunaweza kufikia lengo la Yesu ambaye ana mawazo tofauti na yale ya jamii. Kwake Yesu, mtu ni mkuu ikiwa yeye ni mdogo; tena mtu ni wa kwanza ikiwa yeye ni wa mwisho; pia mtu anakwezwa ikiwa yeye anajishusha. Katika jumuiya zetu za wafuasi wa Yesu muhimu sio uhusiano wa biashara bali upendo wa hiari na ukarimu, kutumikia wenzetu kama Mwalimu Yesu ambaye alikuja kutumikia na sio kutumikiwa. Maisha yake ya utumishi ni kipimo chetu. Hatuhitaji mahali pa kwanza, bali kutumikia kwanza kwa njia ya unyenyekevu na ukarimu. Tujifunze kutoka kwa Kristo aliyefahamika kama Mtumishi wa Bwana kwa namna ya kipekee, ili utumishi wetu uweze kumpendeza Mungu.   

Fr Ndega

domingo, 21 de agosto de 2016

KUFANYA MAPENZI YA MUNGU NA KUPATA UZIMA


Kutafakari kuhusu Lk 13, 22-30

    Wakati wa safari ya kwenda Yerusalemu, Yesu alitumia nafasi ya kuwafundisha wanafunzi wake hasa kuhusu masharti ya kuingia katika ufalme wa mbinguni. Kwanza kabisa haitoshi kuwa wanafunzi wake ili kupata wokovu. Hivyo, aliwapendekezea mlango mwembamba kama changamoto. Ikiwa Yesu anajulisha mlango mwembamba ni kwa sababu pia kuna mlango mpana. Wakati Mt. Yohane Paulo wa II alipoongea na vijana katika mwaka wa 1993, alitofautisha vizuri njia hizi mbili, akisema: “kataeni barabara rahisi: barabara ya anasa, uhalifu, kudharau mazuri, na kukwepa wajibu. Ulevi na matumizi ya madawa ya kulevya na uasherati visiwe na nafasi katika maisha yenu. Pitieni mlango mwembamba. Chagua barabara ielekeayo kwenye uzima wa milele na furaha pamoja na Mungu.” Katika kifungu kingine Yesu alisema kwamba mlango mwembamba ni njia ambayo inaongoza kwenye uzima na wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo. “Huu ni mlango wa uvumilivu, busara, kujitoa, ukarimu, wema, shukrani na kazi”. Kuhusu mlango mpana, hii ni njia rahisi inayoongoza kwenye maangamizi na waendao njia hiyo ni wengi. Basi, ili wanafunzi wa Yesu waweze kupata mafanikio katika safari yao wapaswa kupitia mlango mwembamba.   

    Katika mazingira yetu mlango mwembamba ni ishara ya juhudi yetu ya kushinda mwelekeo mbaya wa maisha yetu na kuwatendea watu mema. Katika mwendo huu ndio sisi wa kwanza wa kupata mafanikio ama bahati mbaya, kwa sababu lile tunalofanya kwa ajili ya wengine linasababisha hali nzuri ama mbaya kwetu pia. Hadithi fulani inatusaidia kuelewa vizuri hali hii. “Siku moja mwandishi wa habari alimhoji mwenye shamba ambaye ameshinda mara ya tano mashindano kuhusu mahindi mazuri zaidi katika eneo hilo. Mwandishi alimwuliza swali akisema, “unapataje kuzaa mahindi bora kuliko wengine?” Mwenye shamba alijibu, mwendo huu ni rahisi sana; nina mazoea ya kushiriki mbegu zangu nzuri na majirani wangu.” Mwandishi aliendelea kwa swali akisema, “Kwa nini unashiriki mbegu zako nzuri na majirani wako ikiwa hao wanashindana pia katika mashindano haya pamoja?” “kwa sababu ni upepo ambao unasambaza poleni ya mahindi na tena ni upepo ambao unaweka poleni mashambani na unafanya mbegu zikue. Ikiwa majirani wangu watakuwa na mahindi mabaya, upepo utasambaza poleni mbaya shambani kwangu nayo mahindi yangu yatakua mbaya. Basi ili mahindi yangu yawe mazuri ninapaswa kuwasaidia majirani wangu wote ili wawe na mbegu nzuri.”

      Basi, lile zuri ambalo tunatarajia kwa maisha yetu tunapaswa kusaidia kwa ajili ya wengine. Katika mwendo huu hatuwezi kuitafuta furaha kwa njia ya ubinafsi. Ikiwa tunataka kuwa wenye furaha, tunapaswa kuisaidia hali hii nzuri kwa wale wanaoishi karibu nasi nao wako na shida sawa nasi. Tunapaswa kushinda mwelekeo wa jamii wa kufikiria wengine kama washindani nasi. Wengine sio washindani, bali ndugu. Kujaribu kupata upendeleo tukiwavuruga wengine ni udhalimu na kutuacha mbali sana na matarajio ya Yesu. Ikiwa tuko mbali na matarajio ya Yesu, matokeo yatakuwa mbali sana na yale tuliyotarajia kwa maisha yetu. Tunaweza kuongea vizuri sana kuhusu Yesu ili kuonyesha kwamba tunamjua Yeye na Biblia pia. Tunaweza hata kufikiri kwamba kuongea bora kuliko wengine kunawezekana kuwa faida ili tupokee baadhi ya tuzo kutoka kwa Mungu. Lakini, kulingana na andiko hili, maneno hayatoshi kuingia katika ufalme wa Mungu. Wokovu si astahili yetu, lakini hii ni zawadi ya ukarimu wa Mungu.


         Je, inawezekanaje tuseme kwamba tunamjua Yesu naye aseme kwamba hatujui sisi?” Hii ni kwa sababu katika biblia kitenzi kujua kinamaanisha uhusiano wa ndani, uzoefu wa kina ambao ni muhimu sana katika safari yetu ya wanafunzi wa Yesu. Ikiwa anasema kwamba hatujui sisi ni kwa sababu sisi hatumjui yeye. Katika mwendo huu hakuna ahadi/makubaliano kuhusu pendekezo lake, hakuna utambulisho. Hatuwezi kuwa wanafunzi wa Yeu kupitia maneno peke yake. Ushuhuda wa maisha unathamini zaidi kuliko maneno. Tukijifikiria bora kuliko wengine haituhakikishia wokovu. Kila kitu tunachofanya kinasababisha matokeo makubwa kwetu na katika hali iliyo kandokando yetu. Kwa maneno mengine, kufikia mafanikio ama bahati mbaya kwa maisha yetu kunatutegemea sisi wenyewe; huu ni uamuzi wetu. Neema ya Mungu ituongoze ili tuweze kufanya mapenzi yake na kupata uhai. 

Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Serah

quinta-feira, 18 de agosto de 2016

MOYO WETU UKO WAPI?


Kutafakari kuhusu Hek 18, 6-9; Wab 11, 1-2. 8-19; Lk 12, 32-48

Liturgia ya siku ya leo ni mwaliko wa kumwamini Mungu kwa kweli. Kwa kufanya hivyo, tuna Ibrahimu kama mfano na mwaliko wa Yesu ili wanafunzi wake wakeshe na kujiweka tayari kwa ujio wake. Somo la kwanza linaongea kuhusu usiku ule maarufu ambao Waisraeli waliutazamia wokovu wa wenye haki na uharibifu wa adui. Uhakika kuhusu uwepo na tendo la ajabu la Mungu katika safari yao uliwaimarisha watu kukesha na kungoja ukombozi wao kutoka utumwani Misri. Huu ni mwaliko wa tuwe tayari kumtambua Bwana Yesu miongoni mwetu na kumkaribisha katika nyakati zote.  Kulingana na somo la pili, katika imani sisi tu warithi wa ahadi za Mungu kwa Ibrahimu; nasi, pamoja naye, tu wasafiri na wageni juu ya nchi. Kupitia imani tunatamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Ndiye Mungu mwenyewe aliyetutengenezea mji kwa sababu hana haya ya kuitwa Mungu wetu. Pamoja na Ibrahimu na wenye haki wengine tunaalikwa kuziamini ahadi za Mungu kwa sababu ni mwaminifu yule aliyeahidi.
Katika njili Yesu aliwaita wanafunzi wake kama kundi dogo ambalo lilikuwa limepewa ufalme kutokana na ukarimu wa Mungu Baba. Katika mazingira yale, watu walioacha kila kitu na kumfuata Yesu, walikuwa wachache na hawakuwa matajiri au watu wenye uwezo. Hata hivyo, Yesu aliwaalika kuuza mali yao na kutoa sadaka kwa ajili ya walio na mahitaji zaidi. Katika njia hii wanaweza kujitajirisha wenyewe kwa Mungu kupitia uhuru wa moyo kama vile mwalimu wao alivyo. Mali yao haina maana tena kwa sababu Kristo ndiye hazina yao. Kristo mwenyewe anataka kuwatumikia kwa kushiriki nao furaha sawa anayoona katika ushirika wake na Baba. Yeye anaweka wazi kwamba kumtumainia Mungu na wala siyo mali, ni wajibu wa kila mfuasi wake wa kundi dogo, ambalo mwishowe wanaunda Kanisa lake. Mwinjili Luka alipoiandika Injili yake, Kanisa lilikuwa bado dogo, la wanyonge wasiokuwa na uwezo na hawakujulikana.
Mwaliko wa Yesu kwa kundi lake, lililo sisi sote, ni kufanya tofauti na tabia ya kutafuta usalama katika mali nyingi ama ulinzi katika wenye nguvu. “Ni hatari kwa Kanisa na viongozi wake kutafuta umaarufu na nguvu, kama vile kuwa na uwezo wa kisiasa na kuweka vitega uchumi. Wakati wote katika historia, ambapo Wakristo walitegemea serikali, wanasiasa, na faida kubwa katika biashara, Kanisa lilikuwa dhaifu na kuporomoka.” Basi, Yesu anatuangalisha tena kuhusu hatari ya mali na anatushauri tuwafadhili fukara. Tumepewa ufalme na Baba kwa sababu sisi tu kweli wake, katika Yesu. Kutokana na hii zawadi ya Mungu, tunakuta hazina yetu ya kweli na kwa hivyo ni halali kumtegemea Mungu katika mambo yote; hayo ni matarajio yake. Wakati Mungu anakuwa hazina ya kweli katika maisha yetu, na mioyo yetu ikamtukuza yeye, uhusiano mpya utaanza na kukua. Moyo wetu uko wapi? Mungu alitukabidhi ufalme wake nasi tunaalikwa kujikabidhi mikononi mwake. Huu ni ukabidhi wa makubaliano. Hii ni hali inayotupasa kuwa na imani, yaani, ile imani ya Ibrahimu na wenye haki wengine wa Biblia.

kulingana na uzoefu wa Ibrahimu, haitoshi kuamini; ni lazima kutii, kumwachia Mungu na kuruhusu kuongozwa naye hadi palipompendeza. Kuhusu uzoefu huu wa Ibrahimu, waraka wa Waebrania unatuletea ushuhuda mzuri sana, yaani, “Kwa njia ya imani Ibrahimu alitii alipoitwa ahamie nchi ambayo angepewa kuwa mali yake. Alihama bila kujua anakokwenda” (Waebrania 11:8). Kumwachia Mungu ni kuwa na imani ya Ibrahimu. Ni imani ya kumwacha Mungu aitwe  Mungu aliye Baba na Mtoaji. “Matatizo yote yapaswa kufikiriwa na kusomeka kwa maelewano na ubaba wake” (Mt. Yohane Calabria). Haya ni matarajio ya Yesu kwa maisha ya sisi sote tulio wanafunzi wake wapya na warithi wa utume wake. Yeye anakuja daima kukutana nasi na kutarajia kukaribishwa vizuri kupitia uaminifu na utayari wetu. Kama anavyoona furaha kwa kushiriki nasi ufalme wa Baba yake vile vile ataona furaha kubwa zaidi atakapokutana na wale ambao watakuwa tayari kwa ujio wake. Tukumbuke kwamba “furaha ya Bwana ni nguvu yetu.”

Fr Ndega 
Mapitio na marekebisho: Serah

domingo, 14 de agosto de 2016

HATARI YA KUMILIKI MALI NI KUMILIKIWA NA MALI


Kutafakari kuhusu Mhu 1,2;2,21-23; Kol 3,1-5.9-11; Lk 12,13-21

Masomo ya siku ya leo ni mwaliko wa kwelekea kwa uangalifu katika mambo ya mbinguni kwa sababu tumefufuliwa pamoja na Kristo na tumerithi zawadi za kimungu kupitia yeye. Maisha yetu yanaonja hali mpya ambayo yanafikiria mambo yaliyo juu kuwa muhimu zaidi kuliko mambo ya dunia. Ili tuweze kuendelea na safari yetu kwa maana, tunapaswa kumtegemea Mungu katika mambo yote.
Kuhusu injili tunataka kutafakari kuhusu mambo muhimu mawili, yaani maana ya maisha yetu na maana kamili ya mali katika maisha yetu. Kuhusu maana la maisha yetu, Yesu alisema kwamba “Uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu alivyo navyo.” Yesu anafikiria kwamba Maisha yanathamini zaidi kuliko mali. Tukumbuke yale aliyomwambia kijana tajiri, yaani “Nenda na kuuza ulicho nacho, ukawapa maskini na kunifuata”. Mali ilipotumika kwa ajili ya upatanisho na ndugu ni chombo cha wokovu; tukumbuke mkutano wa Yesu na Zakayo: “Leo wokovu umeingia katika nyumba hii, alisema Yesu.”
Wakati wa Yesu kilianza kipindi kipya ambapo wasiwasi na mahangaiko ya kawaida katika maisha yalikuwa  hayana maana tena. Yesu aliweka wazi kuwa mshikamano na familia haipaswi kumzuia mtu kumfuata. Mfano, mtu fulani alisema: “Nipe ruhusu ili niende kumzika baba yangu.” Yesu alimwambia, uache wafu wazike wafu wao...” Wakati ambapo wafuasi walikuwa bado hawajagundua upya wa ufalme wa Mungu, mali ilionekana kuwa usalama wa maisha ya baadaye. Sasa Yesu analeta mtazamo mpya. Lengo la uwepo wake miongoni mwa wanadamu ni kuwasaidia kugundua tena nafasi maalum ya Mungu katika maisha na ahadi kwa ajili ya jirani. Mali haiwezi kuchukua nafasi ya Mungu katika maisha yetu wala kutuzuia kuwasaidia wengine. Kwa hivyo Yeye (Yesu) anatuuliza swali, yaani, “Vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?” kutokuwa na jibu kuhusu swali hili kunaonyesha kwamba tuko mbali sana na matarajio ya Yesu ambaye aliweka lililo njema kwa ajili ya wengine kama kipimo cha kuishi vizuri, yaani, kwa maana.
Zawadi tumepokea kutokana na ukarimu wa Mungu, hatuwezi kutumia kwa njia ya kibinafsi peke yake. Njia ya mafanikio ya maisha yetu sio kuwa na kitu bali kushiriki kitu. Anaposhiriki zawadi zake nasi Mungu anatufanya vyombo vya ukarimu wake kwa sababu anatarajia kwamba tuweze kutenda kama yeye alivyo. Tunatambua kwamba umo ndani yetu mwelekeo wa kumiliki na kuongeza mali, na kama matokeo, kadiri tunavyokuwa na mali, tena kadiri tunavyokosa kwa unyeti mbele ya hali ya walio na mahitaji mengi. Basi, ingawa mali inaweza kuwa msaada kwetu, injili hii inatukumbusha kuhusu hatari ya kuwa na wingi wa vitu ambavyo ninatufanya kuwa kama vipofu mbele ya hali ya wengine. Wakati tunaposhiriki kile tulicho nacho kwa ajili ya wengine “tutajitajirisha kwa Mungu.”  
Yesu anatuonya kwamba kutafuta usalama na furaha katika mali ni ndoto ya uongo kwa sababu mbili: ya kwanza, kadiri tunavyokuwa na mali, ni kadiri hiyo hiyo tunavyozidi kuwa na tamaa ya kupata zaidi; ya pili, tunapotafuta mali, hatutosheki wala kutulia. Basi, hatari ya kumiliki mali ni kumilikiwa na mali na kusahau hali ya kimungu na ahadi kwa ajili ya ndugu. Hatuwezi kusahau kwamba Mungu alituumba kwa ajili yake hatutulii mpaka tutakapotulia katika yeye (Agostino wa Hippo Afrika Kaskazini). Katika mali hatutulii, tutatulia katika Mungu.

Katika Matendo ya Mitume Luka anatoa picha ya jumuiya ambapo watu wanawashirikisha maskini mali zao, kiasi ambacho “hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu” (Mtd 4, 34).  patakuwa tena na yeyote atakayekosa mahitaji. Sisi ni wasafiri hapa duniani, na tutakapokufa hatutachukua chochote pamoja nasi (Sir 11:19). Mungu tu ndiye utajiri na tumaini letu la kudumu, na kitu kingine chochote ambacho hakituleti karibu na Mungu na wenzetu ni mbatili mtupu. Tukifikiria ufupi wa maisha tungempa Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yetu. Tunaalikwa kutumia mali yetu kama kuendeleza kazi ya Mungu, kusaidia maskini, wateteaji amani. Hivyo tutatumia mali yetu kwa njia ya imani. Tunaweza kusema kwa kutumia maneno ya Zab 90:12, yaani, “Ee Mungu utufundishe ufupi wa maisha yetu ili tuweze kuwa na hekima.”

Fr Ndega 
Mapitio na marekebisho: Serah

BABA YETU ANATUPA ROHO MTAKATIFU


Kutafakari kutoka Lk 11, 1-13

       Siku hii ya leo tunataka kutafakari kuhusu thamani kubwa ya sala ya Bwana, yaani, “Baba Yetu” na ahadi ambayo tunaalikwa kuchukua kutokana na sala hii. Ingawa tunatumia maneno haya, yaani, “Sala ya Bwana”, tusisahau kwamba hii ni sehemu muhimu ya utambulisho wa wakristo nasi tunaposali, tunataka kumaanisha kwamba sisi ni wamoja na wana wa familia moja kwa sababu Mungu ni wa wote. Kwanza kabisa Yesu akisali aliwapa wanafunzi wake mfano muhimu wa kuishi kwa sababu kwake, kusali kulikuwa tabia yake ya kawaida. Katika mazungumzo hayo ya moyoni, Yesu alimwita Mungu kama Baba na kuishi kwa uhusiano wa kina/ndani naye. Basi, tuko mbele ya uhusiano wa Mwana na Baba. Hakika wanafunzi wake walimwona akisali mara nyingi nao walitaka kujitambulisha na mwalimu wao hata katika shughuli hii. Hivyo mmojawapo alimwambia, “tufundishe!”
       Wakati Yesu alipowafundisha wanafunzi wake kusali, hakika aliwakabidhi maneno ambayo aliyatumia katika uhusiano wake na Baba na kuwakumbusha kuhusu mahitaji ya kuwa na tabia kamili, yaani tabia ya mwana anayemwomba Baba kwa imani. Hii ni tabia ya kujisalimisha mikononi mwa Huyo anayejua mahitaji ya wana kabla ya wamwombe kitu. Yesu hakuhitaji kusali kwa sababu ni Mungu aliye mmoja na Baba; hata hivyo, alisali sana. Kwa upande wake mtu anapaswa kusali sio tu anapohitaji bali kwa sababu hii ni sehemu muhimu ya safari yake ya kuishi, kama vile kula chakula, kunywa maji ama kupumua. Sehemu ya kwanza ya sala hii ni utambulisho wa ubaba wa Mungu, ambao unaonyeshwa kupitia utunzaji na wema wake. Huu ni mwaliko wa kulitukuza jina la Mungu, yaani, “Baba yetu… jina lako litukuzwe!” na mambo yote ambayo yanakuja baada ya maneno “Baba yetu…” yanayategemea maneno haya. Kulitukuza jina la Mungu ni kumpa Mungu utukufu wake kufanya Mapenzi yake kama Yesu alivyo, hasa aliposema “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Baba yangu.” Ni lazima kufanya mapenzi ya Mungu ili Ufalme wake utokee duniani kama mbinguni.
        Tunapaswa kumwelekea Baba huyo kwa imani, sisi tulio na uhakika kwamba tumepokea sana. Tunaomba kwa ajili ya mkate, ya msamaha na ya upatanisho. Kulingana na Maandiko matakatifu, “kutokana na wema wake tumepokea neema juu ya neema”. Ushuhuda huu ni uthibitisho wa utunzaji wa upendo wa Mungu anayeshiriki zawadi zake na wana wake, kutarajia kwamba tufanye vivyo hivyo kwa ajili ya wengine ili undugu kati yetu uwe maonyesho ya ubaba wake na chombo cha huruma yake. Sala Baba Yetu yadhihirisha kwamba sisi tuna mahangaiko kuhusu hali ya wengine na sio kuhusu mahitaji yetu ya kibinafsi tu. Sala hii inatufundisha kuomba kwa ajili ya lililo muhimu sana, yaani, “mkate wa kila siku”. Kwa sababu gani? Kwa sababu tunapaswa kupigana dhidi ya aina yote ya ukusanyaji na ubadhirifu wa chakula ambao unauharibu undugu, kuwafanya maskini na wenye njaa wateseke. Kuhusu mambo haya Baba Mtakatifu Francisco asema: “Ulaji umetuongoza kutumia chepesi pamoja na ubadhirifu wa chakula cha kila siku... Tunapaswa kukumbuka kwamba chakula ambacho sisi hutupa takatakani ni kama ikiwa tulikuwa tumeiba kutoka meza ya walio maskini na wenye njaa.”

Kwa Mt. Yohana Calabria, sala “Baba Yetu ni Injili kwa ufupi. Matatizo yote yapaswa kufikiriwa na kusomeka kwa maelewano na ubaba wa Mungu.” Ikiwa tunasema “Baba Yetu” ni kwa sababu tunasadiki kwamba sisi ni ndugu wa wengine wengi. Mungu hawabagui watu na hamsahau yeyote wa wana wake. “Kikundi chochote cha kidini kinapoanza kufikiri na kutenda kama kwamba Mungu yuko nao tu na sio watu wengine huko ni kumbinafsisha Mungu.” Yeye hapendezwi na sala ambayo inawaacha ndugu wengine. Mungu hatupatii daima yale tunayomwomba, bali anatupatia daima tunayohitaji. Ikiwa hatupokei yale tunayomwomba yeye ni kwa sababu hatuombi ipasavyo. Pamoja na kutufundisha kusali Yesu anatufundisha kuishi. Tunaalikwa kuishi kwa undugu kutokana na uzoefu wa ubaba wa Mungu na kuwa na tabia kamili katika ushusiano wetu naye, yaani kuwa na tabia ya wana, kwa sababu mtu ambaye haishi kama mwana hapati kutenda kama ndugu. Roho Mtakatifu aliye zawadi kubwa ambaye Baba alitupa kwa sababu ya wema wake, atusaidia kusali kama Yesu alivyofundisha, yaani, kwa njia kamili. 

Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Serah