Kutafakari kuhusu Lk 10:
1-12, 17-20
Yesu alikuwa na wanafunzi wengi. Alichagua
kumi na wawili kati yao ili wawe mitume, lakini alipowatuma wamtangulie katika
kila mahali, aliwatuma wote, hata wasio na cheo cha mitume. Jambo hili muhimu
tunakuta katika toleo la Luka peke yake. Injili zingine, yaani, Marko na
Mathayo, zinataja utume wa Thenashara peke yake. Kama namba Sabini na mbili
ilikuwa namba ya mataifa yaliyojulikana katika mazingira yale, hii inamaanisha kwamba
mataifa yote yanaalikwa kuikaribisha na kuishuhudia habari njema ya injili na uwepo
wa ufalme wa Mungu. Ushuhuda wa wanafunzi utatokea kati ya nguvu ambazo zinaupinga
mpango wa Mungu unaowaletea wote maisha mapya. Basi, kutangaza ufalme wa Mungu na
kuwaponya wagonjwa ni kiini cha utume wa wafuasi wa Yesu. Ili waweze kupata
mafanikio katika kazi, walipaswa kumtegemea Mungu katika mambo yote kama sehemu
muhimu sana kati ya mwongozo waliopewa na Yesu ulio karibu sawa na ule wa
mitume Thenashara. Waliporudi kutoka kazi walimpasha Yesu habari kuhusu
mafanikio yao naye Yesu aliwahakikishia kwamba maana ya mafanikio hayo hayatoki
kwao, bali yatoka kwa Mungu kwa sababu utumishi wao ni ushiriki tu katika kazi zilizo
za Mungu mwenyewe.
Msingi wa namba sabini na mbili tunaweza kukuta
katika vitabu viwili vya Agano la Kale, yaani, cha Hesabu na cha Kutoka. Katika
kitabu cha Kutoka namba 70 inatajwa tu miongoni mwa walioalikwa kwenda milimani
Sinai pamoja na Musa. Katika kitabu cha Hesabu tuko na kuwekwa kwa wazee sabini wakati Musa alipolalamika kuhusu
mzigo wa kuwatunza watu wote, akisema: “Siwezi kuwatunza watu wote hawa peke
yangu; hilo ni jukumu kubwa mno kwangu!... Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia
Mose, “wakusanyeni wazee sabini wa
Israel, ambao wewe unajua wanaheshimiwa na kukubaliwa na watu kuwa viongozi...
Nitashuka sehemu ya roho niliyokupa, niwape watu hao. Nao watabeba jukumu la
kuwatunza watu hawa pamoja nawe (Hes 11, 14.16-117).” Pamoja na hao wazee
wengine wawili ambao walikuwa wamebaki kambini walipokea pia roho na kutabiri
bila kuacha (Hes 11, 26). Andiko hili linahitimika kuonyesha matarajio ya Musa
kuhusu wito wa Watu wa Mungu wawe manabii. Kama andiko hili, Maandiko
Matakatifu yote yanayashuhudia mahangaiko ya Mungu kuhusu maisha ya Watu wake
na furaha yake ya kuwashirikisha wanadamu katika kazi ya wokovu wao wenyewe.
Utume wa wanafunzi hawa unafanana na utume
wa Yohane Mbatizaji, yaani walipaswa kutangaza ukaribu wa ufalme wa Mungu wakimtangulia
Yesu ambaye alikuwapo na kutenda mema, lakini watu hawakumjua bado. Yesu akawatuma
wawili wawili kwa sababu utume wa kuutangaza Ufalme wa Mungu si kazi ya mtu
achukue peke yake. Ni kazi ya jumuiya nzima nayo ni lazima ichukuliwe pamoja. Yesu
alisema kwamba ni muhimu kusali kwa sababu sala ni msingi wa utume na siri ya
mafanikio yake. Aliushiriki uwezo wake nao pamoja na unyeti wake kuhusu hali ya
mateso ya watu ili waweze kuwatumikia. Utumishi kwa watu ambao ni wa Mungu ni
utumishi kwa Mungu. Kwa hivyo ni lazima kuwa macho kuepuka kuyatumia mamlaka hayo
kwa njia mbaya. Ni jukumu lao kutangaza maisha kamili ya ufalme wa Mungu,
lakini ikiwa watu hawalikubali pendekezo lao si jukumu lao tena. Wanafunzi wa
Yesu wanapaswa kutenda kama mwalimu wao alivyo, yaani wanapaswa kuuheshimu
uhuru wa watu. Habari ya ufalme inatokana na ukarimu wa Mungu nayo ni njema kwa
sababu ni matokeo ya huria/hiari.
Sisi ni wanafunzi wapya wa Yesu na siku ya
leo yeye anatarajia utayari sawa kutoka kwetu. Kwanza kabisa, tunapaswa kuwa
macho kwa msukumo wa Mungu na kuzifuata nyayo za Yesu, kuchukua njia yake ya
maisha, yaani njia ya unyenyekevu, na kufikiri tofauti na mwelekeo wa jamii.
Kulingana naye mafanikio ya utume wetu yanawezekana ikiwa uzoefu wa kutenda
pamoja unapata kushinda uzoefu wa kutenda kwa njia ya ubinafsi, kusaidiana
katika jumuiya na kwa wema wa jumuiya. Tunapochukua kazi pamoja tunasaidiwa na
wengine; hivi ni rahisi kufikia mafanikio yanayotarajiwa. Tunaweza kutangaza
halisi ukaribu wa ufalme kupitia utumishi wetu wa ukarimu na wa hiari,
kuheshimu wale wanaotenda tofauti nasi. Baadhi ya ugumu katika safari yetu
tunapaswa kukabiliana kupitia roho ya sala na kujirekebisha daima. Ukarimu wetu
katika safari ya wito uwe alama ya utayari wetu kwa mambo yote kwa ajili ya
ufalme wa Mungu.
Fr Ndega
Mapitio na marekebisho: Sarah
Nenhum comentário:
Postar um comentário