Kutafakari kuhusu Lk 14: 25-33
Umati wa watu waliandamana
na Yesu, lakini sio wote waliokubaliana naye. Alipoitambua hali ya kutokuwa na ahadi
na makubaliano, aligeuka na kuwaelekeza baadhi ya maneno. Maneno yake yalikuwa
nafasi ya kutafakari kwa kweli maana ya safari yao. Ingawa Yesu alikuwa maarufu,
kwa sababu ya mambo mema aliyofanya kwa ajili ya watu, utume ambao Yesu alichagua
kutimiza mapenzi ya Mungu hauleti umaarufu. Watu waliamini kwamba Yesu alikuwa
mpinduzi lakini hawajafahamu aina ya mapinduzi Yeye aliyoleta ulimwenguni. Walitaka
kumfuata kwa njia yoyote.
Kama Yesu hakuwa na nia ya
kumdanganya yeyote, aliongea nao kwa uwazi sana kuhusu maana ya kumfuata na
matokeo ya uamuzi huu. Njia hii ya kusema ilikuwa tabia yake ya kawaida kama
alivyofanya kwa ajili ya wale kumi na wawili, yaani aliwajulisha masharti ili wawe
wanafunzi wake wa kweli. Kutoka kwao, Yesu hakutarajia werevu ama upumbavu,
bali upatikanaji, urafiki na imara. Hawawezi kumfuata Yesu kwa sababu walipokea
habari tu ya kuwa ni vizuri kufanya hivyo. Yesu anatarajia zaidi, yaani mabadiliko
ya ndani na kukubali mapendekezo yake kweli.
Andiko hili ni mwaliko wa
kuchukua ahadi ya kumfuata Kristo kwa kupanga mambo ya kesho, yaani kuwa na
uwezo wa kuona mbele ili kuepuka kufaragua na udanganyifu. Ni vizuri kuota
ndoto lakini ndoto hii inapaswa kuihusu hali halisi mtu anayoishi, vinginevyo
itakuwa udanganyifu tu. Yesu anataka kuepuka kwamba safari ya wafuasi wake iwe
pasipo maana ama ya udanganyifu. Ni lazima utambuzi, hekima, kupanga na uamuzi.
Mungu mwenyewe anatupa mfano
wa kuwa na mipango ya muda mrefu ili tupate mafanikio katika mambo yote
tunayofanya kama wafuasi wa Yesu. Yeye Mungu alipanga kumtuma mkombozi ili kuokoa
ulimwengu, kulingana na yaliyoandikwa: “... wakati maalum ulipotimia, Mungu
alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke... ili apate kuwakomboa waliokuwa
chini ya sheria.” (Wagalatia 4: 4-5). “Hata baadhi ya wakulima hutegemea mvua
inyeshe hata kama hawajaandaa shamba mahali pa kupanda mbegu kama za mahindi au
maharagwe.” Kupanga mambo ya kesho ni muhimu.
Yesu alisema, “Basi,
kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi
wangu.” Kama ilivyotekea katika vifungu vingine, Yesu aliwapendekezea watu mpango
wa maisha unaojumuisha kujinyima, kwa sababu yeyote anayekutana na Yesu kwa
kweli amekwisha pata hazina ya kweli kwa maisha yake wala hawezi kubaki alivyo,
yaani mambo mengine hayana maana tena kama kwanza. Kwa maneno mengine, Yesu
anataka kuwa kipaumbele maishani mwa wanaoamua kumfuata. Hakuna jambo lingine
ambalo liweze kuitoa maana ya kweli kwa maisha yao ila Yesu peke yake.
Wanafunzi wa Yesu wa kweli
walimtegemea Mungu katika mambo yote kama Yesu alivyo. Yeye alishiriki na wanafunzi
wake ufalme wa mbinguni na kuwajulisha njia ya msalaba ili waweze kufanya
mapenzi ya Baba yake. Kupitia njia hii, tunatambua kwamba Kumfuata Yesu
hakuuleti upendeleo au hadhi, bali mateso na kujisalimisha kwa ajili ya ufalme
wa Mungu. Basi, yeyote anayetaka kuishi bila ahadi hawezi kumfuata Yesu. Tena yeyote
ambaye anatamani kumfuata Kristo bila msalaba hatapata kumfuata kwa kweli
kamwe.
Kupitia njia ya unyenyekevu
na utupu Yesu alipata utukufu. Utambulisho wa wanafunzi wa mwalimu Yesu
unapaswa kufuata njia sawasawa naye. Kwa upande wa Kristo msalaba ulikuwa
sehemu muhimu katika mwendo wa kufanya mapenzi ya Mungu na kudhihirisha kwa
mpango wa upendo wake. Kwa upande wetu kama wanafunzi, kuchukua msalaba ni
ishara ya utayari wetu kwa mapenzi ya Mungu kwa kujitolea kama Kristo. Kwa
kufikia lengo hili tunapaswa kujikana sisi wenyewe ili Mungu aweze kujifunua
kwa nguvu yote ya upendo wake. Tunapaswa pia kujiondoka kutoka katikati, yaani mahali
muhimu ili wengine waweze kuwa na nafasi ya kwanza. Kwa maneno mengine, tunapaswa
kuwafikiria wengine ni wamuhimu kuliko sisi wenyewe. Kama haiwezekani kumfuata
Kristo bila msalaba, mfano wake wa uaminifu kwa mpango wa Mungu utuimarishe katika
safari yetu ya yetu ya kujitolea kwa ajili ya ufalme wa Mungu.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário