Kutafakari kuhusu Isa.
42:1-4, 6-7; Mdo. 10:34-38; Mt 13: 13-17
Tunasherehekea sikukuu ya
ubatizo wa Bwana Wetu Yesu Kristo. Hii ni mwisho wa Wakati wa Krismasi na
mwanzo wa Wakati wa Kawaida. Kama ubatizo ni mwanzo wa maisha yake hadharani, katika
liturjia hii ni nafasi ili tuandamane naye katika kazi yake ya kawaida huko
Palestina. Hii ni nafasi maalum pia ya kuukumbuka ubatizo wetu na kuweka upya
ahadi ya kuwa Wakristo, kwa kuishi wito wetu wa wana wa Mungu kama Kristo
alivyo.
Yesu ndiye mtumishi
wa Bwana, aliyetabiri na Isaya, kulingana na somo la kwanza. Mungu mwenyewe
anajulisha mtumishi wake kama yule ambaye anatenda kulingana na mapenzi yake
kwa sababu hatumii mamlaka yake kwa manufaa yake mwenyewe bali anapenda kuishi
kama “agano la watu na nuru ya mataifa.” Hivyo uwepo wake duniani ni mafanikio
ya wokovu wa Mungu kwa wote hasa kwa ajili ya walio na shida
nyingi.
Kulingana na kitabu
cha Matendo, Petro anatangaza amani kwa kupitia Yesu aliyefanya kazi njema kwa
maisha ya watu kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye. Vivyo hivyo kwa sisi sote
tuliobatizwa katika Kristo, yaani tunaalikwa kuishi kama Kristo kwa kuendelea
utume wake kwa manufaa ya Kanisa na wokovu wa binadamu kwa sababu yeye yuko
pamoja nasi. Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya ubatizo wetu ulio ushiriki katika
uhai wake wenyewe.
Katika Injili tuko
na mkutano maalum kati ya Yesu na Yohana ambaye alikuwa akibatiza. katika wakati
wa kwanza Yohane alikataa kumbatiza Yesu kwa sababu alijifikiria mwenyewe kama
sauti tu wala asiyestahili kufungua ukanda wa viatu vyake. Baadaye Yesu
mwenyewe atatambua ukuu wa Yohane akiweka unyenyekevu wake kama mfano kwa
safari yetu. Yohana aliwabatiza watu kwa maji kama ishara ya kugeuka kwao
kutoka dhambi. Lakini Yesu hakuwa na dhambi, basi, kwa nini alikubali kubatizwa?
Kwa Yesu ilikuwa
nafasi ya kuonyesha mshikamano wake kuhusu kazi ya ajabu ya Yohana, kuthibitisha
kwamba Mungu anatarajia watu wake warudi kwake. Wakati wa ubatizo wa Yesu Mungu
mwenyewe alimjulisha akisema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe”.
Sauti hii itasikika tena katika tukio la milima. Huko milimani Mungu Baba
alionyesha pendo lake kumhusu Mwanawe akiwaalika wote wamsikilize na kuishi
kama wapendwa kama Yesu. Matukio mawili yalenga kutuhusisha katika ushirika
wake na Baba.
Yesu alionyesha
pia unyenyekevu akijifananisha na binadamu ambaye ana udhaifu na kuhitaji
kuishi katika ushirika na Mungu. Yesu alikuja si kuishi kujitengwa na watu bali
aishi kuhusishwa katika safari yao. Kabla ya Yesu maji yalikuwa na nguvu ya
kutakasa mwili pekee yake. Kutokana na uzoefu huu Yesu aliyatakasa maji ili
yawe na nguvu ya kutakasa pia roho ya watu, yaani maji ya ubatizo.
Baada ya kupokea ubatizo wa Yohana na
kujulishwa kama Mwana mpendwa wa Mungu Yesu aliwezeshwa na Roho Mtakatifu ili
aanze kazi yake akipendekeza uzoefu huu kwa wote ambao wanataka kuwa watoto
wapendwa wa Mungu. Tunaweza kusema kwamba ubatizo ambao Yesu anapendekeza ni uwezo
wa kushiriki katika uzoefu wake wa Mwana wa Mungu. Ubatizo huu ni ishara ya
utambulisho wa Kikristo, yaani Ubatizo wa Roho Mtakatifu na kwa moto, kulingana
na maneno ya Yohane Mbatizaji.
Ubatizo huu una
nguvu ya kufanya mabadiliko katika maisha ya mtu yeyote kwa sababu unamfanya
kuzaliwa katika familia ya Mungu. Alama yetu kama watoto wa Mungu haiwezi
kufutika. Ipo daima! Tunaweza kuishi maisha mapya ambayo ni zawadi ya Kristo
mwenyewe na matokeo ya utume wake. Ubatizo wetu, pamoja na maondoleo ya dhambi,
unadhamini ushiriki katika uzima wa Mungu mwenyewe.
Kupitia alama hii
ya nje tunakufa kweli kwa maisha ya dhambi, na pia tunapitia ufufuko wa maisha
mapya katika Kristo aliye mshindi dhidi ya dhambi na mauti. Yeye ni mwanga wa
kweli ambao unamtia nuru kila mtu. Yeyote akimfuata hatatembea gizani bali atakuwa
na nuru ya milele. Kupitia mwendo huu tumekuwa wana wa nuru ili tutembee katika
mwanga wa Mungu kila siku ya maisha yetu. Ekaristi hii itusaidie kuishi lengo
hili la safari yetu ya Kikristo, walio wana wapendwa wa Mungu.
Fr Ndega
Nenhum comentário:
Postar um comentário