Kutafakari kutoka Luka 14,1.7-14
Yesu alialikwa kula chakula nyumbani mwa
Mfarisayo mmoja na, kwanza kabisa, yeye alisababisha usumbufu kwa sababu alimponya
mtu mmoja siku ya Sabato. Sheria ya Wayahudi inakataza hali hii, lakini Yesu
anapendelea kuwatunza watu kuliko kuifuata sheria ambayo haikufuata nia ya
Mungu ya asili. Akitarajia waweze kufikiri kama yeye aliwauliza swali: “Je, ni
halali au la kumponya mtu siku ya Sabato?” Lakini walinyamaza. Tukumbuke kwamba
Mafarisayo na Waandishi waliondoa maana ya kinabii ya sheria, wakitafsiri
kulingana na mawazo yao ya upungufu. Hao wanapenda sana kujiinua na kupendezwa
na watu. Mara nyingi Yesu alipokutana nao hakufikia mafanikio kuhusu
mapendekezo yake ya maisha mapya kwa sababu hao ni wanafiki na kupendelea
kumjaribu Yesu kuliko kubadilisha mawazo yao kulingana na matarajio yake. Kwa
hivyo mara nyingi mkutano wa Yesu nao ni maana ya mapambano.
Yesu yupo karamuni. Injili ya Luka inaonyesha
kwamba kushiriki katika milo mbalimbali kulikuwa muhimu sana kwa Yesu
aliyetumia vipindi hivi kama nafasi ya kuwafundisha watu. Karamu miongoni mwa
Wayahudi inathaminiwa sana. Pamoja na maana ya uzoefu wa familia, kielelezo cha
urafiki, mshikamano na hamu ya kukuwa pamoja, karamu pia ni mfano wa uhusiano wa
upendo kati ya Mungu na watu wake (Hos 2:1-23, Isa 54:4-8, Eze 16:7-8). Katika
mafundisho ya Agano la Kale, kushiriki katika Ufalme wa Mungu, mara nyingi
hulinganishwa na kushiriki katika karamu (Isa 34:5-7, Zek 9:15,1 Nya 12:38, Zek
14:15-24). “Karamu za namna hiyo mara nyingi zilikuwa na ujumbe wa kimasiha.
Zilisherehekea ushindi wa Mungu dhidi ya nguvu za uovu (Isa 25: 6-8),
zikaimarisha uhusiano kati ya Mungu na watu wake, na kuwaunganisha watu kati
yao.” Huu ni kweli, mfano kwenye karamu ya arusi. “Upendo wa Mungu ni kama ule
wa Bwana arusi, jinsi alivyolipenda na kulichagua Taifa la Israeli kama mali
yake mwenyewe. Wakristo wa kwanza, walifikiria pia juu ya uhusiano wao na
Kristo kama mfano (Yoh 3:39, 2Kor 11:2, Efe 5:23-32).”
Basi, katika injili ya leo, Yesu alishangaa
kwa sababu ya mashindano ya watu kwa ajili ya kuchukua mahali pa kwanza katika
karamu naye aliwapendekezea tabia tofauti. Mtu akipendelea kuwa wa mwisho, alichagua
kuwa mtumishi kama vile Kristo aliyeja sio kutumikiwa bali kutumikia. Katika jamii, kutafuta mahali pa kwanza,
msimamo, upendeleo na umaarufu ni hali ya kawaida inayosababisha mapambano,
chuki na ukatili kati ya watu. Hata katika Kanisa na jumuiya zetu tunaweza kukuta
hali sawasawa na hii. Yesu alikwisha ameonya kuhusu hatari za hali hii na kufundisha
unyenyekevu kama njia kamili. Unyenyekevu ni fadhila ambayo inampendeza Mungu
na watu. Kuwa mnyenyekevu ni kuchukua hali ya udhaifu ya kibinafsi kwa kushinda
mwelekeo wa kujiona mwema kuliko wengine. Inamaanisha kutumia nguvu zote za kibinafsi
ili kuwatumikia wengine kwa ukarimu na upendo hasa wakiwa ni maskini na walio
na shida ya kimwili ambao hawana cha kutulipa. Hii ni kipimo cha furaha ya
kweli kwetu. Hii ni njia ya kuonyesha kwamba upendo wa Mungu unatolewa kwa
hiari kwa ajili ya watu wote. Katika karamu ya arusi mbinguni, yeye
atawakaribisha wale wanaomwelekea kupitia matendo ya upendo.
Lengo la Yesu ni kuzaa ubinadamu mpya na aina
mpya ya uhusiano miongoni mwa watu. Msingi wa ubinadamu mpya ni unyenyekevu na
upendo. Thamani hizi zinapaswa kusaidiwa zaidi miongoni mwetu. Kupitia utumishi
wa kindugu na wa kinyenyekevu tunaweza kufikia lengo la Yesu ambaye ana mawazo
tofauti na yale ya jamii. Kwa Yesu, mtu ni mkuu ikiwa yeye ni mdogo; tena mtu
ni wa kwanza ikiwa yeye ni wa mwisho; pia mtu anakwezwa ikiwa yeye anajishusha.
Katika jumuiya zetu za wafuasi wa Yesu muhimu ni kutumikia wenzetu kama Mwalimu
Yesu alivyo. Yeye anatuhakikishia kwamba yoyote tunayofanya kwa ajili ya walio
na shida yatasahauliwa na Mungu. Maisha yake ya mtumishi ni kipimo kwetu. Hatuhitaji
mahali pa kwanza, bali kutumikia kwanza kwa unyenyekevu na ukarimu. Tujifunze
kutoka kwa Kristo aliyefahamika kama Mtumishi wa Bwana kwa namna ya kipekee ili
utumishi wetu uwe bila unafiki na kuweze kumpendeza Mungu.
Fr Ndega